Sunday, February 27, 2011

MIKESHA YA LEO NA MTAZAMO WA BIBLIA KUHUSU MAOMBI YA MAPATANO

Maombi ya mikesha msingi wake mkubwa ni mapatano ya watu hao walioamua kutafuta suluhisho toka kwa Mungu Juu ya kile kilicho mbele yao.Kwanza nieleweke kua hapa nazungumzia maombi na sio kuombewa yaani maombezi. Biblia inatuonyesha namna ambavyo baba zetu walifanya wakati wanatafuta majibu yao toka kwa Mungu wakiwa kama timu au kundi la watu. Tunawaona kina shadraki ,Meshak ,Ebednego pamoja na Daniel namna walivyoenda kwa Mungu kwa umoja Daniel 2:17-23 pia tunawaona Paulo na Silasi walivyomlilia Mungu katika taabu yao.
Makamu wa Rais wa Tanzania Mh Omar Gharib Bilal akiwa mgeni rasmi katika moja ya mikesha ya kuliombea Taifa uliofanyika uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam
Kwa habari ya Kina Daniel kwa pamoja vijana hao waliona uzito wa hoja iliyo mbele yao na wakania kwa dhati kuingia katika maombi. Unaweza kugundua kua vijana hawa hawakujiuliza watajibiwa lini hilo kwao halikuwasumbua bali walijiapiza kua hawatatoka usoni pa MUNGU mpaka wajibiwe. Kwa mtazamo huo ukapelekea akili zao,nguvu zao,nia zao za ndani zilenge kuhakikisha MUNGU anatokeza na kuwapa ndoto na  tafsiri ya yake. Na kwa kadri ambavyo walionyesha kudhamiria kwa pamoja katika maombi yao ndipo MUNGU hakukaa kimya. Mwishoni baada ya kupata jibu toka kwa Mungu na kuliwakilisha ndipo inatoka amri kwa Mfalme Nebukadreza kua asiabudiwe MUNGU mwingine isipokua MUNGU wa akina Daniel.
                                                                          
 Naporudi kanisani leo nakutana na maombi mengi ya mapatano ikiwemo mikesha, hapa naijumlisha mikesha yote ile inayofanywa ndani makanisani iwe ya vikundi vya vijana, wamama, kwaya nk pamoja na ile ifanyikayo nje katika viwanja vya wazi. Watumishi wanaaoanda mikesha hiyo hua na malengo maalumu ambayo mwisho wa mikesha hutaka kuona kila aliyehudhulia kafikia lengo la mkesha huo. Inapofikia hapo pa kuangalia ufanisi wa mikesha yetu leo nakua na maswali mengi kichwani. Kama tumeamua kufanya maombi ya mapatano kwa kifupi hii ni timu, na mara nyingine uzembe wa mchezaji mmoja huigharimu timu nzima.

Hivyo tunapoenda katika mkesha tunaweza kua sehemu ya kuufanikisha mkesha huo au kuudhohofisha. Siamini kama Mungu alikua makini kuisikiliza sauti ya Daniel pekee wakati wale vijana wote wanne walipokua wakiomba. Hivyo kujibiwa kwa vijana hao ni matokeo ya wao wote kwenda mbele za uso wa Mungu kwa pamoja na kwa nia moja wakiwa na dhamira ya dhati kumsihi Mungu asikilize maombi yao. Dhamira ya dhati kutafuta majibu toka kwa Mungu kwa pamoja ndio msingi mkubwa wa Maombi ya mapatano.
Watumishi wakimlilia Mungu kwa Pamoja kama timu
 
Waumini au washiriki wa mikesha hiyo siamini kama hua tuna picha halisi ya lengo la mikesha hiyo na hata kama tunayo basi ni kwa kiasi kidogo mno, nashawishika kusema hatujui nini kilicho nyuma ya mikesha hiyo. Katika maombi ya pamoja kwanza ni mapatano ya kutafuta suluhu toka kwa MUNGU kama tulivyoona kwa kina Daniel.Tunapokua katika mikesha ya namna hiyo binafsi hua inanisumbua pindi nnapojiuliza Je ni wote tuliohudhuria tunahitaji majibu ya maombi hayo kwa dhati?
      
Nachokiona leo, wokovu na maombi ya mikesha vinaenda kimazoea zaidi, ni kama hua tunajisemea kwa kua hua tunaenda kwenye mikesha oookyy basi na leo twende !!!. Tunafanya maamuzi ya haraka haraka ili yafumbue matatiyo yaliyodumu kwa muda mrefu, mwisho wa siku tunaishia kupaka rangi bahari. Ni wazi kua mikesha ya leo ni kama fashion ile kiu ya kwenda kwenye mkesha kwa nia ya kukutana na MUNGU ni ndogo kuliko kiu ya kukutana na marafiki, ndugu jamaa. Hivyo tunajikuta tunaenda mikeshani ili kusocialize na kidoooogo kuutafuta uso wa Mungu. Wapo pia wanaoenda kwenye mikesha kwa sababu tu labda ni viongozi Fulani makanisani au ni viongozi katika kikundi Fulani hivyo cheo ndio mzizi wa uwepo wao mikeshani. Ni watu wachache sana ambao hudhamiria toka wakiwa makwao kua napoenda katika mkesha wa leo ntapaza Sauti yangu kwa MUNGU kwa kumaanisha kama alivyofanya Anna katika 1Sam 10-19.
      
Ni kawaida kabisa leo kuona watu wakienda katika mikesha kama wanakwenda kwenye Burudani, ile hali ya kuugua ndani/mzigo juu lile linalokwenda kutokea kwenye mkesha haipo. Mwanafunzi bora ni yule anayejiandaa kabla ya kuingia katika mitihani na sio anayekurupuka. Kabla ya kwenda kwa  MUNGU pia ni vivyo hivyo ile nia ya dhati tunayokua nayo ya kukutana na MUNGU, huchochea humuweka MUNGU karibu yetu. Daudi akasema nafsi yangu yakutamani kama ayala atafutavyo maji ya mto, hapa nafsi ya Daudi ina kiu naweza sema haja ya kina ya  kukutana na MUNGU nahii ni moja kati ya sababu zilizomfanya Mungu awe rafiki mkubwa wa Daudi.
                                           
Vijana wakiwa katika mkesha
Luka 14:28-30 "Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama? " Kabla hatujaenda kwenye mikesha ni wangapi kati yetu wenye desturi ya kukaa chini kwanza na kujiuliza naenda kukutana na nani, Na huyo Mungu anauzito gani kwangu hadi nikaongee nae. Pasipo kujiuliza maswali kama hayo utakuta kwenye mikesha mingi watu wanakua hai wakati wa kusifu na kuabudu ikifika wakati wa kiini ncha mikesha hiyo yaani maombi watu wanapotea kwa kutoka nje kama ni kanisani, na kama ni uwanja wa wazi basi wanaanza kupiga stori.

Ni vizuri tunaposema tunaenda katika mikesha makanisani au viwanja vya wazi kuomba au kwenda kwenye tukio lolote tunalolifanya usiku mzima kwa ajili ya MUNGU tujipange kwa kua katika makusanyiko hayo MUNGU hua yuko serious  kuliko tunavyofikiria. Leo vijana makanisani au vyuoni utakuta wanaenda kwenye Campus Nights kama wanaenda Mlimani city au Nyumbani Hotel (Mwanza) kuangalia sinema. Hata kama ni tamasha la kusifu na kuabudu weka malengo na tamasha hilo Kua ntamsifu Mungu wangu pasipo mzaha kwa kua katika kumsifu yeye ndiko aliko. kadri ambavyo tupatavyo neema ya kua karibu zaidi na Mungu kwa njia ya maombi au kusifu na kuabudu yeye hushuka na kukaa nasi kisha vile vitu vyote ambavyo si vya kimungu(Vimelea) vilivyo kati yetu huondoka. Hii ni kwa kua vifungo hivyo hushindwa kustahimili nguvu ambazo MUNGU hushuka nazo hatimaye tunawekwa huru, ndio mana kunashuhuda nyingi leo za watu kuponywa na nguvu za Mungu au MUNGU kutupatia mahitaji yetu kupitia mikesha pindi tupojipanga sawasawa.

Wanafunzi wa vyuo vya Elimu ya juu toka jijini Dar-es-salaam wakiwa kwenye Campus Night ya mwaka 2009 iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa
Kwenye matamasha ya kusifu na kuabudu nako kunahitajika hekima ya Mungu katika kujipanga kabla ya kuhudhuria, kwa kua kuna tofauti kati ya mwanafunzi anayekwenda shule na yule anayekwenda shuleni kusoma. kiini cha matamasha hayo ndicho kitupelekee kuhudhuria na sio kwa sababu msanii Fulani yupo. Tukisema kumsifu Mungu ni lazima msanii Fulani mkubwa awepo ndio tamasha lifanyike au mkesha unoge huu ni ufa mwingine ambao leo unaojijenga katikati ya kanisa. Kimsingi muziki ni sanaa tusipojipanga kabla ya kuhudhuria tutajikuta tunaenda kuburudishwa tu na tunarudi wakavu majumbani kwetu. Leo ukilichukua gitaa la John Lissu tukawapa Twanga pepeta litapiga vizuri tu kwa kua muziki ni sanaa, hivyo muziki wa ki-Mungu unaweza pia kukuburudisha vile vile unaweza kukuweka karibu na MUNGU endapo ukikamia lolote kati ya hayo mawili
Moja ya matamasha ya kusifu na kuabudu
Katika mikesha nguvu za MUNGU na msaada wake huwepo hivyo ni jukumu la mgonjwa kusogea mwenyewe na kutumbukia katika kisima cha uponyaji kwa kua malaika tayari anakua keshatibua maji. Pindi MUNGU anapoleta msaada katikati yetu kisha sisi tukabaki kushangaa au kupiga stori ule msaada uliokuwepo usiku huo unakua hauna maana, hii hali ya kutothamini nguvu zaMungu mara nyingine inaunda ghadhabu ya MUNGU juu yetu. Ni jambo la kawaida leo kuona watu wanaenda mikeshani na matatizo yao na wanarudi nayo nyumbani. Hii haimaanishi Mungu hakuwako mkeshani au mahali pa kusanyiko, kimsingi alikuweko na alikua akitafuta yule anayemtafuta kwa dhati ili ampe msaada ila wakachengana.

Ni vizuri kila anayehudhuria mkesha wowote kwa ajili ya Mungu kabla hajavaa tai,tshirt,sketi,viatu nk maana skuizi kuna mbwembwe nyingi za uvaaji pindi tunapoenda mikeshani tutambue uzito wa yule yunayekwenda kutafuta majibu kwake na tujiulize maswali mengi kuhusu yeye. Kwa kua yeye MUNGU yuko serious sana na Mikesha hiyo kuliko sisi.


V.N Mboya
                                                                                                      

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...