Friday, November 4, 2011

Serikali ya Tanzania yakataa ushoga


Waziri wa Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Kimataifa Mh Benard Membe

TANZANIA imesema ipo tayari kukosa misaada yote kutoka Serikali ya Uingereza na kamwe haiwezi kuruhusu sheria inayotambua mashoga na kuhalalisha ndoa za jinsia moja.Msimamo huo mzito wa serikali umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutamka kwamba nchi yake ina mpango wa kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria na katiba zao, hazitambui mashoga na ndoa za jinsia moja.
Cameron alikaririwa akithibitisha kuwa tayari amewajulisha juu ya suala hilo Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola waliokuwa wakihudhuria mkutano wa Jumuiya hiyo uliomalizika siku nne zilizopita, mjini Perth, Austaralia ambao pia ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete. 

Waziri Mkuu huyo kutoka chama cha Conservative ambacho kilishinda uchaguzi Mei mwaka jana, alisema suala hilo la mashoga na ndoa za jinsi moja ni moja ya mambo yanayoongoza sera ya serikali yake kuhusu misaada kwa mataifa mbalimbali na kwamba tayari imeanza kutekelezwa katika maeneo kadhaa duniani.

Kauli ya Cameron imechukuliwa kama kielelezo cha ukoloni mamboleo ambao Uingereza inajaribu kuupandisha daraja kwa mataifa yanayoendelea kwa kigezo cha misaada
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alisema pamoja na umasikini wake, Tanzania kamwe haitaruhusu upuuzi huo kwa kigezo cha misaada.
“ Tanzania ni nchi maskini lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti kwa sababu ya misaada yake na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni wetu, hata sheria zetu zinakataa,” alisema Membe.

Alifafanua kuwa katika kuonesha msimamo wa kutokukubaliana na masharti hayo, Tanzania imeshikilia msimamo thabiti kupinga upuuzi huo ambapo Januari mwaka huu, ilimkataa balozi shoga ambaye aliteuliwa na nchi yake kuja kuiwakilisha hapa nchini. Hata hivyo Waziri Membe hakutaja jina la balozi huyo wala nchi anayotoka. 

“Niwape siri moja ambayo tuliificha lakini leo ngoja niwaambie, mwanzoni mwa mwaka jana nililetewa barua kunijulisha ujio wa balozi mmoja anayekuja kuiwakilisha nchi yake, mwanamume mwenye ndoa ya jinsia moja. Nilikwenda kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuhusu wasifu wa balozi huyo mtarajiwa naye akajibu kwa maneno matatu, yarabi toba! Mkatae!” 

Waziri Membe alifafanua kuwa serikali ilimkataa balozi huyo kwa kuwa ni kinyume cha utamaduni wetu na sheria za nchi kuwa na watu wenye tabia hizo.
Alisema alimjulisha waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kwamba balozi huyo haruhusiwi kuja kufanya kazi nchini kwa kuwa ni kinyume na utamaduni wetu. “Waliendelea kuniomba kwamba balozi huyo akija hatatoka kwenye makazi yake akiwa na mwenza wake hivyo watu hawatamuona lakini tulimkataa kabisa, wakatuelewa,” alisema Membe.
Alieleza kuwa tamko hilo la Waziri Mkuu Cameron linaweza kusababisha hatari ya kuvunjika kwa uhusiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na koloni mama Uingereza na waziri huyo atabeba lawama hizo 

Akisisitiza msimamo huo wa serikali, Membe, alisema Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha tisa, kinatambua ndoa ya jinsia mbili tofauti, yaani mume na mke. “Sheria hizi tunazozitumia hivi sasa tumezirithi kutoka Uingereza ambako leo wanatukuza ndoa za jinsia moja na ushoga,” alisema Membe. 

Suala la kile kinachoitwa haki za binadamu kuhusu ushoga ilikuwa moja ya ajenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana katika mkutano Perth. Hoja ya kukomesha vizuizi dhidi ya ushoga na ndoa za jinsi moja lilikuwa moja ya mapendekezo yaliyokuwamo katika ripoti ya ndani kuhusu matarajio ya baadaye ya Jumuiya hiyo ya Madola.

Itakumbukwa kwamba, Malawi tayari imeathirika na mpango huo wa Uingereza kwa sehemu ya misaada yake kusitishwa kutokana na msimamo wa nchi hiyo kuhusu kile Uingereza na nchi za Magharibi zinazokiita haki za mashoga. Ikumbukwe pia kuwa, mjadala mzito ulioibuka katika Bunge la Uganda mwaka 2009 kuhusu ndoa za jinsi moja ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo ya Uingereza na washirika wake.

Ajenda zingine Mkutano wa Perth Waziri Membe alisema viongozi wa Jumuiya ya Madola walikubaliana suala la mabadiliko ya tabia nchi kuwa ajenda kuu katika nchi hizo. Alisema ajenda hiyo sasa inakuwa muhimu kutokana na nchi nyingi wanachama wa jumuiya hiyo kuwa katika tishio kubwa la uharibifu wa mazingira. 

Aidha, Membe alisema nchi hizo zimekubaliana kuandaa kanuni na mwongozo ambao utatakiwa kufuatwa na nchi za jumuiya hiyo.
“ Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Jumuiya ya Madola tutakutana Aprili mwakani kuandaa miongozo na kanuni hizo,” alisema Membe.

Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...