Wednesday, November 14, 2012

Umoja wa Makanisa Tanga wasema “hatulidhishwi na Taarifa juu ya uchomaji wa Makanisa”



Waziri wa Mambo ya ndani Mh Dr Emmanuel Nchimbi

Umoja wa Wachungaji wa Makanisa ya Mkoa wa Tanga umesema hauridhishwi na taarifa zinazotolewa na serikali na viongozi wa siasa kuwa wanaohusika na uchomaji wa makanisa ni wahuni  na si Waislamu wakati wanazuoni na masheikh wa taasisi za kiislamu wanakiri vitendo hivyo vinafanywa na baadhi ya waumini wenzao.

Umoja huo umesema unashangazwa na kitendo Waziri wa Mambo ya Ndani,  Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye naye anavihusisha vitendo hivyo kufanywa na wahuni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mwenyekiti wa umoja huo, Dk. Jonathan Mwakimage, alisema serikali inapaswa kushughulikia kiini cha matatizo yanayopelekea kuwepo kwa vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaowashawishi vijana kufanya vitendo vya kihalifu.

Alisema hawajaridhishwa na namna ambayo serikali imekuwa ikishughulikia wahusika wa vitendo hivyo huku baadhi wakiendelea kuwa na kiburi na kujiona kuwa wako juu ya sheria.
Alisema kumeibuka kundi la watu ambao wamekuwa wakiwashawishi vijana kufanya vitendo vya kuhujumu vitabu vitakatifu jambo ambalo limekuwa likichukuliwa na serikali kama kitu cha kawaida.

“Hapa Tanga kuna makanisa manne yamechomwa moto na taarifa zilifika polisi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa, kuna biblia zilichanwa na kukojolewa mwezi uliopita lakini bado kimya na wahusika wanaendelea kujinadi tu mitaani, sisi haturidhishwi na namna ambayo serikali inachukua hatua,” alisema Askofu huyo.Alisema kuwa umoja huo wa makanisa unalaani vikali kitendo cha kukojolewa kwa Qurani, lakini pia unaona kuwa yule aliyemshawishi mwenzake kufanya kitendo hicho ni mkosaji wa kwanza na anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria sawa na huyo aliyetekeleza  kitendo hicho.

Hata hivyo, aliwaomba maaskofu na wachungaji kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kwa kuepuka kulipa kisasi na kuwasihi waumini wao hususan vijana kujiepusha na waovu  wanaowashawishi kukojolea, kuchoma au kuchana Quran.

“Katika hili niwaombe Mashehe, Maimam na viongozi wa kiroho wa dini ya Kiislamu kuwa na msimamo mkali kushughulikia waumini wao kwa kukemea vitendo hivyo kwa wazi ili kudhibiti wenye nia ovu…hii ni pamoja na misikiti inayoendelea kuchochea chuki dhidi ya ukristo na serikali na hasa suala la uchomaji wa makanisa” alisema Dk. Mwakimage.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Canon James Dominic, wa Kanisa la Anglikana, aliitaka jamii kutambua kuwa watu wote wana asili ya tumbo moja kutoka kwa Hawa na Adamu na kwa kutambua hilo Watanzania wanapaswa kuishi kwa umoja, utulivu, amani na upendo.

Alisema ni vigumu kuamini kuwa mtu mwenye dini ya kweli na kumwamini Mwenyezi Mungu kwa dhati anaweza kufanya vitendo hivyo na hasa kwa kutambua kuwa vita ya kidini haina mshindi na ni sumu mbaya kwa usalama wa Taifa.

Umoja huo unahusisha makanisa yote yaliyopo mkoani  Tanga kasoro la Roman Catholic na la Sabato.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...