Home

Sunday, March 27, 2011

NJAA HUNYIMA UHURU WA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI

Mara nyingi unapokua katika uhitaji sana wa jambo Fulani, usipokua makini unaweza kujikuta umefanya jambo ambalo hukulitarajia ilimradi tu ufikie lengo ulilolihitaji.Njaa haina ustarabu, ukiwa na njaa ni lazima upime kila wazo linalokuja akilini mwako kabla hujaamua kitu cha kufanya ili usijelamba shubili ukiamini ni choklate. Hii ni kwa kua Biblia inasema katika Mithali 27:7 Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali, bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kua kitamu.
Maamuzi yoyote huanzisha safari
Leo hili kuna wasomi wengi walioko maofisini lakini ukiwauliza wamepataje kazi hawawezi kusema, kwa kua walipokaa mtaani na digrii kwa miaka kadhaa bila kazi wakibaki nyumbani wakiangalia Tv na kufanya harakati nyingine, au waliingia  katika kufanya kazi zisizo za Professional yao huku wakinyanyasika na kudharauliwa. Mwishoni wakiona kazi imetangazwa na wanaihitaji kwa dhati, ifikapo hapa huwa radhi kufanya lolote watakaloambiwa hata kama liko kinyume na Biblia ilimradi tu kazi ipatikane. Hii ni kwa kua njaa humnyima mtu uhuru wa kufanya jambo kwa usahihi pasipo madhara hapo baadaye. Na tunapokutana kanisani ni mwendo wa mapambio pamoja na  kusifu na kuabudu tukiamini flani kapata kazi kwa kuwa Bwana ametenda ila ukweli unabaki kwa mhusika kwa kua ajuaye mkizi alipo ni mvuvi.

Kuna watu wengi leo wanatafuta uponyaji wa Magonjwa walio nayo,na yamepelekea kupoteza pesa zao nyingi huku wakifanya mambo mbalimbali ilimradi wapone. Kulingana na utandawazi siku hizi ni jambo la kawaida kusikia watumishi wanalipisha pesa kama unataka kupona Kiharusi, Kansa au gonjwa lolote sugu toa kwanza Gari lako , kiwanja au kiasi Fulani cha pesa ili upone na watu wamekua wakifanya. 

Ufahamu wa kujua  Biblia inasema nini juu ya uponyaji palipo na njaa huwekwa kando, kupona kwanza ndiyo kauli mbiu. Kila mtu kwa sehemu kwa kua tunaishi chini ya jua huingia katika hatua hiyo, na wengi waliofanikiwa katika Mungu ni wale waliofanya maamuzi Mazuri pindi wakiwa na njaa. Mara  nyingi tunapokua na uhitaji mkubwa sana wa kufanya jambo hasa linalohusu hatima yetu ya kesho tunatofautinana namna ya kuivumilia njaa tunayopitanayo muda huo na namna ya kuziweka presha zote pembeni na kurudi kwa Mungu na kutafuta usahihi. Wakati huo ni wakati ambapo unaweza kutengeneza tatizo kubwa zaidi kuliko tatizo lililopo.   

Utulivu wa kimungu katika Maamuzi huitajika kabla ya kula kiapo
Ibrahimu wakati anataka kutoa fungu la kumi jiulize kwa nini aliamua kuipeleka kwa Modekai na sio kwa Mwingine?, na huwezi niambia Taifa zima kuhani alikua Modekai pekee!!.Sasa kwa jiulize kwa nini afanye uamuzi wa kwenda kwa Modekai? Kimsingi Ibrahimu alitaka kumtolea Mungu na ndani yake hiyo ndiyo ilikua kiu kubwa. Mbele yake alitakiwa afanye maamuzi ni nani anastahili kupokea hiyo sadaka. Alipotulia na kurudi kwa MUNGU alipata madhabahu ya kupeleka na Mungu AKAIRIDHIA. Jiulize angekosea) madhabahu (asingeipeleka kwa Modekai) ina maana angekua amepoteza zile nguvu za kuitafuta hiyo sadaka kwa kua aliitolea jasho hivyo hakuipata bure, pia angepoteza ule muda aliotumia kuitafuta. 

Ili Ibrahimu amkute tena Mungu na sadaka yake kama angekosea ingemgharimu kwanza kuitafuta tena hiyo sadaka kwa jasho, akishaipata aingie tena kwenye uwanja mwingine mpya(sio ule wa akina Modekai kwa kua ulishapita) na afanye maamuzi sahihi katika Mungu ndipo MUNGU aipokee sadaka hiyo kama alivyoipokea kupitia Modekai. Hivyo unaweza kuona jinsi maamuzi sahihi ya Ibrahimu yalivyofupisha huo mlolongo. Musa kwa Hasira alipozivunja zile amri kumi hakua na namna, ilimbidi arudi kwa Mungu siku arobaini tena na kuzileta

Maamuzi yanayofanywa wakati unanjaa ni sawa na kutembea katikati ya jiji huku ukiwa umevaa kiatu kinachokubana sana mguuni. Hamu ya kuendelea na safari hua inakua ndogo, Furaha moyoni na tabasamu usoni hupungua kwa kua kiatu kinasumbua. Utakumbuka mambo mazuri yaliyowahi kutokea kwenye maisha yako baada ya dakika mbili akili itakurudisha kwenye kiatu, utakumbuka wajibu Fulani ulionao siku hiyo au zijazo kisha akili itasema kiatu! Kiatu! Kiatu!. Ikifika hapo usishangae kuona mtu akiweka viatu kwenye begi na kunuua ndala. Hatojali watu watamuangaliaje pindi wakimuona na Suti kali chini ndala. Baada ya kiatu kutoka ataona sherehe its fyn mno, bali utata huanza pindi safari mpya na ndala itakaposhika kasi.

2Falme 1. Tunamuona mfalme Ahazia aliyerithi kiti baada ya ya kufa kwa Ahabu, Biblia inaeleza vizuri baada ya Ahazia kuanguka katika dirisha lake alipokua Orofani alitafuta namna ya kuweza kujua atapona au atakufa. Kwake yeye hofu ilimjaa madaraka aliyataka na ugonjwa ukapoteza raha yote ya utawala. Katika njia panda hii alifanya maamuzi ya kwenda kuuliza hatima yake kwa Baal-zebubu mungu wa ekloni na sio JEHOVA. Maamuzi mabaya aliyoyafanya Ahazia wakatiwa shida hiyo yalipelekea Mungu amtangazie mauti kupitia mtumishi wake Eliya .Kwa hali ya kawaida unaweza kumshangaa Ahazia lakini ukiingia uwanjani kwa staili yako na kwa vipimo vyako usipokaa sawasawa na Mungu utajikuta unaingia kwenye mkondo wa Ahazia. 

Utulivu katika MUNGU huitajika katika kufanya maamuzi yanayogusa hatima ya Mwanadamu
Kuna watu leo wako kwenye ndoa na ndoa zao zimekua kifungo na sio Baraka kwao, matumaini ya kupata furaha, amani na utulivu ndani ya ndoa vimeyeyuka kwa kua baada ya ndoa wakajikuta maamuzi waliyo yafanya wakati wa kumtafuta mwenzi pasipo utulivu yamewaingiza katika majuto. Hii ni kwa kua walisubiri kuoa au kuolewa kwa muda mrefu pasipo tumaini na alipotokea aliyeonyesha dalili kiulaini alikubaliwa  mwisho wa siku mateso. Maamuzi yalifanywa ya kuingia katika ndoa ili kuondoa aibu au upweke matokeo yake yanaongeza aibu,Upweke na hata kuisaliti ndoa yenyewe.

Njaa ya kupata chakula ilimpelekea Lazaro kula sahani moja na mbwa wa mfalme, Lazaro aliweka utu wake kando ilimradi aishibishe nafsi yake hilo ndilo lilikua hitaji kubwa kwa lazaro. Kuna jamaa mmoja yeyea lipomaliza elimu yake ya juu, alifanikiwa kupata kazi iliyokua ikimlipa ujira kidogo. Lakini bada ya muda alisikia tangazo la kazi katika ofisi flani na akafanya application. Mungu ni mwema akafanikiwa kuajiliwa, siku wanaenda kupanga alipwe kiasi gain alitajiwa kiasi na waajili wake. 

Kwa kua kiasi alichoambiwa kuwa atapewa kilionekana ni mara mbili ya kile alichokua akikipata kule alikotoka aliitikia kwa haraka kua its oky. Baada ya siku kadhaa akiwa ameanza kuizoea kazi wakati wa stori mbili tatu ofisini akagungua kua wote wenye elimu kama yake mshahara wao ni mkubwa kuliko wake, alipododosa kwa nini yeye wake uwe chini aliambiwa wakati wamakubaliano bargaining power yako ilikua ndogo, ulikubali kirahisi. Hivyo hakua na jinsi na mkataba kasha sign.

Kiu ya kusikia Neno la Mungu huwapelekea wakristo kula kila kitu kitokacho kwa mtu aliye mbele yao pasipo kuchucha 
Unapokua katika uhitaji fulani kisha ukatakiwa kufanya maamuzi, ni vizuri kuondoa kila aina ya presha wakati unafanya maaamuzi hayo. Utulivu na Biblia inasema nini juu ya hilo eneo ndio viwe vigezo vikuu vya kuyaendea maamuzi hayo. Leo hii MUNGU kaachilia uamsho wa aina yake nchini Tanzania, watu wana kiu ya kumtafuta MUNGU kwa gharama kubwa,Wokovu sio ushamba,umasikini au ujinga tena, wokovu umeanza kuonekana kuwa kitu cha thamani mno, hata ambao hawajaokoa wanautamani wokovu. Leo kuna magazeti mengi,majarida,Tv Programes, tovuti mbalimbali vyote vikitangaza Neno la Mungu nab ado watu kila kukicha wakinatafuta habari za Ufalme waMungu.

Kwa waliomakini na hili wanaona dhahiri katika njaa hii ya Neno wakristo wamekua hawana desturi ya kupembua kati ya Neno la MUNGU na personal Interests za watumishi wa Mungu wanaosimama mbele yao. Wao kwa sababu ya njaa ya Neno wanakula kila kitu. Sasa kimbembe kinakuja pale utake kuwarudisha kwenye mstari lazima patachimbika. Kumbuka nia na lengo la wale wasabato Masalia kutoka Mbeya kutaka kwenda Mashariki ya kati kumuhubiri kristo pasipo viza wala tiketi haikua dhambi, na sio kosa na ni kibiblia kabisa kumtangaza kristo kwa kua ndio agizo kuu tulilonalo leo.Tatizo linakuja wakati wa hiyo njaa ya kumuhubiri kristo, Biblia inasema nini kuhusu taratibu na Mamlaka zilizopo duniani?. Utulivu katika MUNGU ni wa msingi mno kabla ya kufanya uamuzi wowote uliobeba hatima ya maisha ya mwanadamu.


V.Mboya                       

No comments:

Post a Comment