Home

Saturday, April 2, 2011

Msama Promotion yaandaa Tamasha la Pasaka kwa mwaka 2011

Mkurugenzi wa Msama Promotion Alex Msama
MWENYEKITI wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama amesema ukumbi wa Diamond Jubilee, utatikisika kwa nyimbo za injili zitakazoimbwa wakati wa Tamasha la Pasaka Aprili 24, mwaka huu.Akizungumza ofisini kwake Kinondoni jana, Msama amesema kila mwimbaji aliyethibitisha kushiriki tamasha hilo, anajiandaa kuhakikisha anafikisha vizuri neno la Mungu kupitia nyimbo zake.

“Nimezungumza na waimbaji wote waliothibitisha kupanda jukwaani Aprili 24, wanasema wanajipanga vizuri kuhakikisha neno la Mungu linawaingia wale watakaohudhuria tamasha hilo,” amesema.

Msama ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotion ambao ni waandaaji wa tamasha hilo, amesema waimbaji nyota wengi wamethibitisha kuimba katika tamasha hilo. Amesema anatarajia wengine ambao bado hawajathibitisha, watathibitisha mapema kabla ya tarehe hiyo kufika.Juzi, mwimbaji Christina Shusho, alithibitisha kushiriki tamasha hilo ambalo hufanyika mara moka kwa mwaka.

Christina Shusho ataimba siku hiyo
Wengine waliothibitisha kushiriki Tamasha la Pasaka hilo ni Rose Muhando, Upendo Nkone, Bonny Mwaitege wote wa Tanzania. Kutoka Zambia ni Ephraim Sekeleti, wakati Kenya ni Anastazia Mukabwa, Solomon Mukubwa na Pamela Wanderwa.Mwenyekiti huyo amesema tamasha hilo baada ya kufanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Aprili 24, litahamia mkoani Dodoma Aprili 25, na Aprili 26, litafanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Ephraimu Sekeleti toka Zambia atakuwepo siku hiyo
 Kiingilio katika tamasha hilo ambalo mgeni rasmi atakuwa Rais Jakaya Kikwete ni sh. 4,000 kwa viti vya kawaida, sh. 10,000 viti maalum (B) na viti maalum (A) itakuwa sh. 20,000.Lengo la tamasha hilo ni kusaidia kusomesha watoto yatima, kuwapa mitaji wanawake wajane na kuwasaidia waathirika wa mabomu yaliyolipuka katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kambi ya Gongo la Mboto.

Tamasha la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa muziki wa injili kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia, Rwanda, Afrika Kusini, Uganda na Kenya.

Anastazia Mukabwa toka Kenya atakuwepo siku hiyo

No comments:

Post a Comment