Home

Monday, June 6, 2011

K’BAZIL KUANZA ZIARA YA UZINDUZI WA ALBUM YAKE YA MUZIKI WA INJILI KATIKA MKOA WA IRINGA

Basil Kashumba maarufu kama K`Basil ni mwanamuziki wa nymbo za injili ambapo hapo awali alikuwa akiimba nyimbo za kawaida(kidunia). K`Basil ambaye ni mhitimu wa Chuo kikuu cha Dar es salaam(UD), nyimbo yake na Stara Thomas iitwayo Riziki ilimpatia ummarufu sana kisha akakaa kimya kwa muda wa takribani miaka mitano. Baadae mwaka 2008 akaamua Kumpa Yesu maisha yake(kuokoka). Kwa sasa yuko mbioni kutoa album yake ya kwanza ya muziki wa Injili.

Basil Kashumba
Album yake ya muziki wa Injili iko tayari na sasa ameanza kufanya matamasha ya uzinduzi wa album yake hiyo ya kwanza ya muziki wa Injili aliyoipa Jina la Yesu Ananipenda akizunguka mikoa karibuni yote aliyowahi kupita kutumbuiza wakati akiimba muziki wa Bongo Fleva.


K’Bazil, Yeye Binafsi anasema kuwa nia na dhumuni ya kupita mikoa yote hiyo aliyowahi kutumbuiza kipindi hicho ni kuchangisha michango ili kusaidia watu wasiojiweza na walio katika mazingira magumu kama watoto yatima, wazee, wajane , walemavu nk. Anasema hiyo ndio njia yake ya pekee ya yeye kumshukuru Mungu kwa neema ya wokovu aliyompatia. Lakini pia kuifuta ile historia yake ya muziki wa Bongo fleva na kuwatambulisha watu kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu sasa na amesimama kweli katika Imani yake na anampenda Yesu pia.

Tamasha lake la kwanza la Uzinduzi litafanyika mkoani Iringa, siku ya Jumapili ya  tarehe 5 Juni ya mwaka 2011 na baada ya hapo K’Bazil atazunguka mikoa mingine kama Mbeya, Morogoro, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro na mikoa mingine michache. Awali tamasha hilo lilipangwa kuanza kufanyika May 29 ila ratiba ilisogezwa mbele kwaajili ya maandalizi zaidi. Tamasha hilo ambalo linaandaliwa na kuratibishwa na Blog site ya Ufufuo Music & News litakuja kumalizika katika mkoa wa Dar es salaam kipindi cha mwezi wa July baada ya kupita mikoa karibuni yote.

Nae mkurugenzi mtendaji wa Blog site ya Ufufuo Music & News inayojishughulisha na kazi ya kuwatangaza waimbaji wa Muziki wa Injili kwa kuandika habari zao pamoja na kutoa sapoti nyingine tofauti tofauti, ndugu Crispin Challe amesema kwamba ni furaha ya pekee na neema ya Bwana Yesu kwa K’Bazil kuitwa kuwa mtumishi wake. Nae kama mpendwa na mwokovu pia anafurahia kumtia moyo na kumuunga mkono K’Bazil kwa hatua aliyoifikia ya kuamua kumtumikia Mungu kwa moyo na kweli, kama mlivyosikia ya kwamba mbali na uimbaji K’Bazil pia ni mchungaji, alisema Crispin.

Kutoka kushoto ni Christina Shusho, Upendo Nkone na Stara Thomas,Stara Thomas nae inasemekana miezi kadhaa iliyopita aliyasalimisha maisha yake kwa Yesu.
Akamalizia kwa kusema kuwa kama vile Blog site yao ya Ufufuo Music & News inavyosimamia andiko la Zaburi 136 ambalo limeandikwa kumshukuru Mungu na kutangaza ukuu wake kupitia shukrani hizo kama mstari wa kwanza unavyoonyesha kwa kusema “ Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele” Kwa hivyo matamasha hayo yameandaliwa kumshukuru Mungu kwa matendo yake makuu kwetu sisi wanadamu, kwa kumbadilisha ndugu yetu K’Bazil na pia kwa neema yake ya wokovu aliyotupatia na anayowapatia watu tofautitofauti kila kukicha.

Album ya Injili ya K’Bazil inakwenda kwa jina la “Yesu Ananipenda” yenye nyimbo takribani 10 ambazo majina yake ni Namjua, Wakati Na Bahati, Wewe Ni Baba, Rudisha, Utukuzwe, Moyo, Asante Yesu, Tusonge Mbele, Mama na Yesu Ananipenda ndio nyimbo iliyobeba jina la album.

No comments:

Post a Comment