Home

Saturday, September 17, 2011

Njia za Kumtia Moyo Mchungaji Wako


Uchungaji ni huduma mojawapo kati ya huduma tano zilizoainishwa kwenye biblia. Mchungaji anajukumu la kulitunza, kulilisha na kuliangalia kundi lake ili liweze kustawi na kuwa mbali na adui. Kumtumikia Mungu kama mchungaji ni huduma njema sana na yenye kuheshimika lakini wachungaji wengi wamekuwa katika wakati mgumu kutokana na lawama na kukatishwa tamaa na wale wanaowachunga bila kujali ugumu wa kazi yao na jinsi gani wanajitoa kwa ajili ya makanisa wanayoyachunga.

Ni vizuri mshirika ukajifunza njia mbali mbali za kumtia moyo mchungaji wako na kujitahidi kuwa kondoo mwema ili kupunguza kugumu wa kazi kwa mchungaji wako na kumwezesha kuifanya kazi hii kwa furaha bila majuto. Kuna njia nyingi za kufanya hivi ila leo nitaziongelea njia chache ili kukukumbusha pale uliposahau kwa ajili ya ustawi wa kazi ya Mungu.


1. Kuwa Sehemu ya Huduma yake
Hudhuria ibada kwa uaminifu na onyesha kuwa upo tayari kufuata uongozi wake. Hii kwanza itabariki maisha yako na itamtia moyo mchungaji wako pia. Tumia karama zako na vipawa katika kanisa unapoabudu na uwe tayari kutumika bila kutarajia kupata chochote kutoka kwa mchungaji. Uwe mwepesi kuwashuhudia wenye dhambi neno la Mungu na kuwatia moyo wale waliovunjia moyo na kukata tamaa.

2. Onyesha Uhai Wakati wa Ibada
Huwa inamtia moyo sana mhubiri pale anapokuwa akihubiri na watu kuonyesha kuwa wapo pamoja naye iwe kwa kupiga makofi au kusema Amen pale wanapoguswa na ujumbe fulani. Kwanza atajua kuwa kuna watu wanamsikiliza na sio kusikiliza tu bali wanapokea kila anahowahubiria.

3. Onyesha Utii Kwenye Uongozi Wake
Biblia inaonyesha wazi kuwa ni lazima kuwaheshimu viongozi wetu wa kiroho. Ebrania 13:17 inasema “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi” Haipendezi wala haibariki kuwa kinyume na mchungaji wako kwa yale ambayo anakuagiza kutenda maana yeye ndiye anayekesha kwa ajili ya roho yako.

Mchungaji na mkewe wakikata keki walioandaliwa na washirika kama sehemu ya kuthamini huduma yao

4. Mheshimu
Mheshimu mchungaji wako hata zaidi ya  unavyomheshimu mtu mwingine anayekuongoza. Ndio unaweza ukawa unamazoea ya karibu na mchungaji wako lakini hii haikufanyi ukose heshima, muonyeshe heshima kwa maneno na kwa vitendo iwe ni kanisani au mahali pengine popote hata kama umemzidi kipato, elimu, umri n.k

1 Thesalonike 5:12-13 Lakini, Ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni; mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi.

5. Muombee Mchungaji Wako
Mchungaji wako anakutana na upinzani mkali sana katika utendaji wa kazi ya Mungu na anahitaji sana maombi yako maana kwa kwa kibinadamu ni ngumu sana. Muombee Mungu amtie nguvu, ampe ujasiri, na kuzidi kumfunulia siri za mbinguni kwa ajili yenu ambao mpo chini ya uchungaji wake.

2 Thesalonike 3:1-2 Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani.

6. Simama Pamoja Naye Katika Nyakati Ngumu
Rafiki wa kweli ni yule anayesimama nawe katika hali zote za maisha, sio yule anayekuacha pale mambo yanapokuwa magumu. Simama na mchungaji wako katika hali zote, usiwe mshirika wa matukio na mafanikio bali simama naye katika nyakati zote. Mtie moyo pale anapopitia magumu iwe ni katika huduma au kifamilia na sio kusimama pembeni na kumsengenya au kumlaumu.

7. Acha Kumlinganisha na Wengine
Mchungaji wako ni wa kipekee na ana karama, vipawa na utashi tofauti na wachungajiwengine uliopata kuhudumiwa nao hivyo usimlinganishe na yeyote kwa nia ya kumuonyesha kuwa yeye siyo bora au amepungukiwa. Kumbuka mchungaji wako sio malaika hivyo anaweza kuwa na mambo fulani ya kibinadamu tofauti na wengine, mwache mchungajiwako awe yeye, usimweke kwenye kipimo nakutarajia awe kama vile unavyotaka wewe.

8. Kuwa Mvumilivu na Mwelewa
Kuwa mwelewa na mvumilivu na mchungaji wako, mke wake na yeyote katika familia yake, usitegemee wawe wakamilifu maana wote ni wanadamu. Usiweke matarajio fulani kutoka kwa mke wake au watoto wake, wakubali kama walivyo mradi hawakiuki misingi ya neno la Mungu. Sio lazima mke wa mchungaji na watoto wako nao wawe watumishi ‘active’ kanisani, waache wafanye yale ambayo Bwana ameweka mioyoni mwao, wakubali na wapende jinsi walivyo.

9. Mtegemeze Kiuchumi
Mtu asipoweza kuitunza familia yake vizuri hawezi kuwa na muda wa kujitoa kwa ajili ya kanisa maana atakuwa anatafuta jinsi ya kuihudumia familia yake. Onyesha upendo kwa kumtegemeza mchungaji wako pale unapoweza iwe ni mafuta ya gari, vocha za simu, ada ya watoto shule n.k.


10. Usiwe Mwepesi Kumhukumu
Usiwe mwepesi kumhukumu mchungaji wako hata pale unapokuwa na mashaka na maswali kuhusu maamuzi fulani aliyoyafanya. Mara nyingine kutokana na sababu za kiuongozi na kiroho hawezi kuelezea kila kitu kwa watu wote. Katika maamuzi yote magumu, kuwa upande wake na epuka kabisa kumhukumu au kumsema pembeni, kumbuka miriam na aaron walipomsema Musa baada ya kuoa mwanamke asiye muisraeli.

11. Usimseme Pembeni
Kama kuna jambo ambalo halijakupendeza au unataka kupata ufafanuzi ni vyema ukatafuta wakati muafaka na kwa heshima ukaongea naye mwenyewe kuliko kumsema pembeni na kwa watu hasa wale ambao sio washirika wake. Kufanya hivyo kutamvunjia heshima na kumwondolea kibali mbele za watu. Usimsengenye wala kusikiliza watu wanaomsengenya mchungaji wako, kama umesikia habari ambayo imepotoshwa isahihishe na kama unaona watu wanafurahia kumsengenya wewe kaa mbali nao!

Ubarikiwe!

 Posted by womanofchrist

3 comments:

  1. Hey Ya'll,

    I've created a list of the highest ranking FOREX brokers:
    1. Best Forex Broker
    2. eToro - $50 min. deposit.

    Here is a list of money making forex instruments:
    1. ForexTrendy - Recommended Odds Software.
    2. EA Builder - Custom Strategies Autotrading.
    3. Fast FX Profit - Secret Forex Strategy.

    I hope you find these lists helpful.

    ReplyDelete
  2. Shukurani sana kwa somo nzuri kuhusu njia za kumutia moyo mchungaji wako

    ReplyDelete