Home

Thursday, January 12, 2012

MOYO WAKO UNASEMA NINI?

roses
DesiComments.com |


Zaburi ya 14:1 “Mpumbavu amesema moyoni, hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, hakuna atendaye mema”.


Zaburi 14:1 b,c ni matokeo ya kauli ya kipengele a. Kwa sababu mtu huyu ambaye ni mpumbavu ameshasema moyoni mwake kwamba hakuna Mungu, hivyo suala la kutenda dhambi kwake  ni kawaida.

Ukisoma pia  Zaburi 36:1 Biblia inasema  “Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake’. Sikiliza mtu huyu hawezi kuwa na hofu ya Mungu kwa sababu tayari moyoni mwake ameshasema hakuna Mungu.
Kwa nini inakuwa hivi? Ni kwa sababu awazavyo nafsini mwake ndivyo alivyo na pia ni kwa sababu maamuzi yake ndiyo yanaamua maisha yake. Soma Zaburi 36:4 na Mithali 23:7a.

Mpumbavu ni mtu anayejua kitu au kweli halafu anafanya maksudi kuvunja hiyo sheria au kukiuka hiyo kweli.
Je, nawe msomaji wangu unapopita kwenye hali ngumu kiuchumi, moyo wako unaema nini?
Unapojaribiwa, unapoachwa, unapochelewa kuoa/kuolewa, kuzaa, kupata kazi moyo wako unasema nini?, unapowekwa na Mungu kwenye nafasi ya uongozi, unapobarikiwa, unapokosewa na ndugu yako, je moyo wako unasema nini?.

Katika mazingira yoyote unayopita lolote utakalolisema moyoni lina matokeo yake, yanaweza kuwa ni mazuri au mabaya tegemeana na ulivyosema.

Lolote utakalolinena moyoni mwako kinyume na ahadi za Mungu juu yako, hii ina maana na wewe umesema hakuna Mungu katika hilo. Kwa lugha nyepesi umekataa wazo au msaada wa Mungu kwenye hilo unalolipitia hadi ukasema hakuna Mungu. Na ukisema hakuna Mungu tegemea kutopata msaada wa Mungu bali kuonewa zaidi na utawala wa Shetani.

Tuangalie mifano kadhaa kwenye Biblia;
      Mwanamke aliyetokwa na damu kwa miaka 12, Mathayo 9:20-22
      Anania na safira , Matendo 5:1-4.
      Yuda Iskariote, Yohana 13:2
      Mikali binti Sauli, mke wa Daudi, 2samweli 6; 16, 20-23.
Katika hii mifano yote hawa watu hawakusema kwa vinywa vyao, bali ni mawazo/kusema kwa mioyo yao.
Na ndiyo maana Yeremia 17:9 inasema;

Moyo huwa mdanganyifu sana kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha, nani awezaye kuujua? Mimi Bwana , nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.

Jifunze kuwa makini na namna unavyosema moyoni mwako, ukihakikisha unasema sawasawa na ahadi/mapenzi ya Mungu kwenye maisha yako.

Bwana Mungu akubariki.

Na: Sanga P.S


No comments:

Post a Comment