Home

Sunday, January 8, 2012

Sunday Sermon: Je, Maamuzi Ya Nani Atakuwa Mwenzi Wako Wa Maisha Ni Ya Mungu Au Ya Kwako?



Mithali 19:14 “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; bali mke mwenye busara mtu hupewa na Bwana”.

Ni matumaini yangu kwamba u-mzima kijana mwenzangu na una maendeleo mazuri kiroho na kimwili. Katika waraka huu mfupi kwa vijana nataka kujibu swali hili ambalo vijana wengi wamekuwa wakijiuliza. Wengine kutokana na kutojua ukweli wake wamejikuta wakifanya maamuzi ambayo hadi leo wanayajutia .

Kibiblia, tunajua kabisa ni mpango wa Mungu tuweze kuoa au kuolewa. Sasa swali linakuja, je ni lazima Mungu anionyeshe, anipe mke au mume wa maisha yangu? Kwani mimi kijana sina uwezo wa kuangalia mtu kisha nikaomba Mungu na mwisho nikajichagulia mwenyewe? Au kifupi maamuzi ya nani atakua mume/mke wangu ni ya nani?

Hili ni swali ambalo vijana wengi limekuwa likiwachanganya. Wengine wanaamini maamuzi hayo ni ya Mungu kunipa mke/mume na wengine wanaamini Mungu hahusiki, bali wao ndio wenye nafasi na wanaohusika. Sasa hayo ni mawazo yao wala mimi sitaki kuyapinga lakini ngoja nikuonyeshe Biblia inasema nini halafu utajua ukweli ni upi:-

Kwenye kitabu cha Mithali 19:14 , Mungu anasema suala la nyumba, mashamba, maduka na vyote vifafanavyo na hivi nimewapa uwezo na ruhusa wazazi wako baba & mama) wa mwili wakupe lakini suala la mke au mume mwenye busara mimi pekee ndiye ninaye wajibika kukupa .Sikiliza kama unataka mke/mume kwa ajili ya kulitumikia kusudi la Mungu alilokuumbia basi huna budi ni lazima upige goti kuomba na kisha ungoje Mungu akuonyeshe/ akupe mke/mume wa kusudi lake.

Vijana wengi wanafikiri eti kwa sababu wameokoka, na wamejzwa roho mtakatifu basi wanao – uwezo wa kujichagulia mke/mume wa kuishi nao. Sikiliza kama una amini umeumbwa kwa kusudi la Mungu na unataka kutembea katika njia yake basi mruhusu Mungu akupe mke/mume mwenye busara ya kukaa na wewe.

Mke au mume ana sehemu kubwa katika maisha yako. Anaweza akabadilisha maisha yako, ya kiroho, kiuchumi, kimwili, kihuduma na kima husiano na watu wengine.Hivyo kibiblia maamuzi ya nani atakuwa mkeo au mumeo ni ya Mungu na si ya kwako. Hii ina maana ukimuomba Mungu hakika atakuletea mtu halisi wa kukaa na wewe. Lakini maamuzi ya kumkubali au kumkataa ni ya kwako na si ya Mungu. Ukikubali shauri la Bwana litatumikiwa, ukimkataa, umejikaribishia laana.
Zifuatazo ni sababu za msingi zinazomfanya Mungu akuchagulie/akupe mke/mume na sio kukuruhusu wewe/wazazi/ukoo wako/mchungaji wako kukuchagulia mke.

(a)Kusudi la uumbaji (kuwaunganisha) .
Sikiliza hakuna mtu aliyeumbwa kwa bahati mbaya, Mungu ndiyo aliyekuchagua na siyo wewe uliyemchagua na akakuweka duniani ili umtumikie sasa yeye ndiye anayejua nikimuunganisha huyu kaka na yule dada watalitumikia kusudi langu.  Warumi 8:28-29.  Mungu anapofanya maamuzi anafanya kwa kuangalia kusudi lake na muda na wahusika wa hilo kusudi. Yeye ni Mungu na anafanya kwa utikufu jifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie na si ya kwako.



(b) Mungu ndiye ana-fahamu nani mwenye busara ya kukaa na wewe.
Mithali 19:14b Busara ni uwezo uliomo ndani ya mtu (mke/mume) unaomsaidia kujizuia kufanya jambo ambalo liko nje ya mpango/mapenzi ya Mungu kwa kufanya lile lilio katika mapenzi ya Mungu.Hivyo Mungu pekee ndiye anaye mjua mke/mume mwenye busara ya kukaa na wewe, kamwe wewe hutaweza mjua bila uongozi wa Mungu.


(c) Sababu za ki-Agano.
Zaburi: 32:8 Siku uliyofanya maamuzi ya kuokoka maana yake uliyakabidhi maisha yako kwa Yesu, ukamwambia nafungua moyo wangu uingie uyatawale na kuyaongoza maisha yangu sasa hilo ni Agano lako kwa Mungu. Kwa sababu hiyo Yesu anawajibika kwako kukufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, hii ikiwa ni pamoja na kukupa mke/mume wa kukufaa.


(d)Mawazo yake, si mawazo yako.
Isaya 55:8 Sikiliza Mungu anayo mawazo (mipango) na njia (mikakati) ya kukufanikisha kimaisha. Sasa katika kutekeleza mipango yake kwako na kupitia wewe lazima atumie mikakati yake ili kutekeleza mawazo yake. Sasa moja ya mikakati yake ni kukupa mke au mume wa kusudi lake .


Sasa, sikatai huenda kwa jinsi ya mwili ni kweli huyo mtu anayekupa Mungu ana upungufu fulani. Huenda umbile lake, sura yake, kabila lake, rangi yake, dhehebu lake, haliko kama ulivyo kuwa unavyotaka wewe. Mungu anakupa mke au mume kutokana na sababu hizo ambazo nimekuekezea hapo juu na ninakuhakikishia ukimkubali atakupa neema ya kukaa naye huyo mtu na kukufanya uridhike naye na kumpenda huyo mwenzako .


Nakutakia uongozi wa Mungu katika eneo la maamuzi ya nani atakua mumeo au mkeo .

 Na: Patrick Samson Sanga.

No comments:

Post a Comment