Home

Monday, February 27, 2012

Mtumishi Atosha Kissava kutoka Iringa kushiriki tamasha la Pasaka Mwaka huu


Atosha Kissava

TAMASHA la Pasaka linalofanyika kila mwaka kwa kuandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions ya Dar es Salaam, linazidi kupanuliwa wigo mwaka huu kwa kushirikisha wasanii nguli na wanaoinukia.

Akizungumza na mwanahabari wa jambo leo jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema mwimbaji Atosha Kissava kutoka Mkoa wa Iringa amekuwa wa tatu kuthibitisha kushiriki tamasha hilo. "Kissava ambaye ana kundi lake la muziki wa injili, anakuwa mshiriki wa tatu kuthibitisha kushiriki tamasha la Pasaka baada ya Upendo Kilahiro na Upendo Nkone," alisema Msama.

Tamasha hilo linatarajiwa kurindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 8 mwaka huu na pia litafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu. Kissava hivi sasa anatamba na albamu ya Nainua Macho Yangu Juu yenye nyimbo za Alpha na Omega, Unaweza, Nifanane na Wewe, Nibariki na Mimi, Kwake Yesu, Njooni Njooni, Yatima na Nainua Macho uliobeba jina la albamu.

"Tunaboresha mambo mengi kuliko miaka iliyopita, waimbaji mwaka huu watakuwa wachache kiasi wakiwamo wa kutoka mataifa mengine ya Afrika... hiyo yote tumefanya ili kukidhi matakwa ya wapenzi wa muziki wa injili. "Mbali na Tanzania, pia tutakuwa na waimbiaji kutoka Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika tamasha hilo la nyimbo za injili za kumsifu Mungu.

No comments:

Post a Comment