Home

Friday, February 3, 2012

NATOA LAKINI SIPOKEI – NIFANYEJE? -1


Mwl Christopher Mwakasege

Kuna wakati fulani, mtu mmoja alinifuata baada ya kipindi nilichokuwa nafundisha Neno la Mungu juu ya utoaji, na akaniuliza hivi; “Kwa nini mimi nimekuwa natoa zaka na sadaka nyingi lakini sipokei? Hata miradi niliyo nayo haifanikiwi nilivyokusudia – ni kwa nini iwe hivyo.

            Inawezekana na wewe unayesoma ujumbe huu sasa una maswali kama haya. Hayo ni maswali ya msingi na ni muhimu tupate ufumbuzi wake. Hata mkulima ambaye alipanda mbegu katika shamba, na asipate kitu au apate mavuno machache, atajiuliza maswali kumetokea kitu gani.

           Tukumbuke ya kuwa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini – tuwe na hali ngumu kimavazi, chakula na kiafya. Pia, tukumbuke ya kuwa ni tabia ya kiuungu mtu kutoa na kutegemea kupokea. Ingawa si lazima upate toka kwa mtu huyo huyo uliyempa, - maana Mungu anaweza kumgusa mtu mwingine akupe – lakini utaratibu wa Mungu unabaki pale pale, ukitoa tegemea kupokea. 

            Ni kitu gani kinasababisha mtu asipokee na huku amekuwa akijitahidi kutoa? Biblia inatuambia ya kuwa tukiwa waaminifu katika utoaji, Mungu atatumwagia baraka, “hata isiwepo nafasi ya kutosha ya kuziweka” – Je! umewahi kumsikia mkristo yo yote akisema amepata baraka nyingi mno hata amekosa mahali pa kuziweka? 

Sababu zifuatazo zitatusaidia kujua ni kwa nini hatufanikiwi katika utoaji wetu – na hata hatupokei kama tulivyotegemea na kutarajia;
1. KUVUNJA MIIKO AU UTARATIBU WA UTOAJI

            Kila jambo lina utaratibu wake – usipoufuata usitegemee mavuno mazuri. Kilimo cha mahindi kina utaratibu wake wa upandaji na palizi tofauti na kilimo cha ngano au cha kabichi. Ndiyo maana wataalamu wa kilimo, walianzisha kampeni za kuwafundisha wakulima juu ya “kilimo cha kisasa” ili kiwasaidie wakulima kupata “mavuno” zaidi toka katika mashamba yao. 

        Hata katika “kupanda na kuvuna” au “kutoa na kupokea” katika mambo ya Mungu kuna utaratibu wake. Ukienda kinyume na utaratibu huo, usitegemee mavuno ya kuridhisha toka katika utoaji wako 

Kwa mfano hebu soma na kutafakari maneno haya yafuatayo:
            “Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama ilivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana   Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2Wakorintho 9:6,7). 
“….wala si kama kitu kitolewacho kwa unyimivu” (2Wakorintho 9:5). 

          Utaona katika mistari hiyo Mungu ametueleza kwa kiasi fulani utaratibu ambao anataka ufuatwe mtu akitaka kuvuna katika utoaji wake. Je! unafuata utaratibu huu katika utoaji wako? 

          Utaratibu huo ni huu; utoaji wako uwe si haba (au kidogo) bali uwe kwaukarimu. Ukitoa kidogo utapata kidogo – bali ukitoa vingi utapatavingi. Ndiyo maana imeandikwa;

            “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. KWA KUWA KIPIMO KILE KILE MPIMACHO NDICHO MTAKACHOPIMIWA” (Luka 6:38) 

          Kama unataka kutoa sadaka tu “ kama ulivyokusudia moyoni mwako”. Kama ulikusudia kutoa shilingi 100/= toa shilingi 100/=. Fanya hivi siku zote na utafanikiwa.
          Tena, utoaji unatakiwa ufanyike “si kwa huzuni; wala si kwa lazima;maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu “… na wala si kwa unyimivu”.
          Michango mingi iliyomo makanisani siku hizi wakati mwingine inafanyika kwa kulazimishana. Mtu anatakiwaatoe kwa kupenda kwake toka moyoni mwake – SI KWA LAZIMA.Kumlazimisha mtu kutoa ni kwenda kinyume cha utaratibu wa utoaji.

          Wakristo wengi wamekosa baraka au mafanikio katika utoaji kwa sababuwanatoa huku WANAHUZUNIKA AU WANALALAMIKA! Wengi wanawanung’unikiaviongozi wa makanisa yao kuwa wanatumia fedha au vitu vibaya. Kama unawasiwasi na matumizi ya matoleo yako – yaombee kwa Mungu ayalindeyatumike kwa utukufu wake kuliko kulalamika.

          Wengine wanahuzunika na kulalamika kuwa michango imezidi. Je! umewahi kumsikia mkulima akihuzunika au kulalamika kwa kuwa ameongezewa shamba la kulima na kupanda? Hakuna. Mkulima halalamiki bali anafurahi kwa kuwa amepata eneo kubwa zaidi la kupanda umeongezewa eneo la KUPANDA ili AVUNE ZAIDI. Ni eneo la kukusaidia kutoa zaidi ili UPOKEE ZAIDI!

Na Mwl Christopher Mwakasege

1 comment: