Home

Tuesday, March 6, 2012

Ushuhuda:Namna Askofu Philemon Tibanenason alivyotoka Bukoba na Kuhamia Jijini Dar es salaam.


Mch Dr Philemoni Tibanenason

Mch Dr Philemoni Tibanenason ni Mwangalizi mkuu wa Kanisa la Pentekoste Tanzania(KLPT),na kwa sasa ni mchungaji wa kanisa la KLPT lililoko Mnazi mmoja jijini Dar es salaam.Hapa Mch Dr Philemoni Tibanenason anaeleza namna alivyotoka Bukoba hadi kufika jijini Dar es salaam.

“Katika Miaka ya Sabini Nilikaa Bukoba nikifanya Huduma kwa miaka miwili,Bukoba(Kagera) ndio mkoa nilioanzia huduma, katika kipindi hicho nilikuwa na miaka 26,na mke wangu alikuwa na miaka 20.Siku moja nikiwa nimelala  yalikuja maono yakinitaka niondoke Bukoba niende eneo lingine ambalo ni mbali sana na Bukoba yaani Dar es salaam.Nilipoyaona hayo niliwaambia watu waliokuwa karibu nami ikiwa ni pamoja na waumini kwamba Imenipasa kwenda kule Mungu alikotaka niende”

Sikulijua hilo kama lingepokelewa kwa hisia tofauti na waumini niliokuwa nao kipindi hicho,hasa ikizingatiwa walikuwa wakinipenda kwa namna ambayo sikuwa najua kwa sababu gani.Nilijua huenda wangefurahia  na kunipa mkono wa kwa heri , lakini walisema wasingependa kunipoteza kwamba niende mbali na wao.Ilinilazimu kuwa na subira kukaa na kumwachia Bwana ili yeye kwa uwezo wake afanye mwenyewe, lakini nikizidi kumsihi Mungu kwamba mapenzi ya Mungu yatimizwe na si kama nitakavyo mimi bali kama atakavyo yeye.

Jambo la kushangaza baada ya kupita muda fulani mke wangu alienda kwenye maombi  na huko kulikuwa na watumishi wengine. Alipofika huko hakukuwa na mtu aliyekuwa akijua maono yangu ambayo Bwana alisema na mimi ya kwamba nihame Bukoma na kuelekea Dar es salaam. Na kipindi hicho washirika wangu walikuwa hawataki nihame.

Dar es salaam Ilivyo sasa
Wakati mke wangu na watumishi hao wakiendelea na maombi,mara wakaanza kunena kwa Lugha,kitendo hicho kilichukua Muda mrefu, na walipokuwa wanakaribia kumaliza maombi, yule aliyekuwa akisimamia maombi alimwambia Mke wangu kuna jambo gani Mungu amesema na nyie? Mke wangu alishituka kidogo kisha  Mke wangu akamwambia Bwana anatutaka twende Dar es salaam, yule mtumishi akamwambia “Sasa kuna jambo gani ambalo linawazuia kufanya kile ambacho Bwana anawataka kufanya?

Baada ya Swali hilo mke wangu alikuwa kimya kisha na baada ya kumaliza maombi alirudi nyumbani na kunishirikisha.Aliponiambia habari hizo nikasema kwa kweli  kwa namna yeyote ile, iwe kwa Miguu,au gari ni lazima nianze safari mara moja ya kwenda Dar es salaam.Washirika niliokuwa nao wao waliendelea kushikilia  msimamo wao kuwa kuwa hawataki niondoke.Kwa mazingira hayo hawakuwa tayari kunipa nauli walikazania niendelee kuhubiri eneo hilo.

Nilikaa chini na kujiambia ikiwa nitawasikiliza wao nitakuwa simsikilizi Mungu aliye hai,niliangalia namna nitavyoweza  kupata pesa za nauli za kunitoa Bukoba hadi Dar es salaam, lakini sikuweza kuiona.Hivyo nikashauriana na mke wangu kuwa tuuze kitanda  ili tuanze safari mara moja, kwa Neema ya Mungu nilifanikiwa kupata shilingi 100,kwa kipindi hicho pesa hiyo  ilikuwa ni kubwa kiasi kwamba hadi kufika Dar es salaam ilitughalimu kiasi cha shilingi 45/= tu.

Tulipofika Dar es salaam na mke wangu tuliwakuta wamishionari tuliofanya nao kazi na wakati wanaondoka walituachia waumini 10, nakumbuka kipindi hicho hakukuwa na wahubiri wengi kama kipindi hiki.Kipindi hicho Askofu Moses Kulola,Masalu,Emmanuel Lazaro sambamba na Titus Mkama ndio waliokuwa wakijitoa mhanga kuihubiri injili jijini Dar es salaam.Kipindi hicho Jiji la Dar es salaam lilikuwa limefunikwa na Uislamu na wakati Mwingine ilikuwa ni hatari kutembea huku ukiwa umeshika Biblia.

Katika Miaka hiyo ya Sabini makanisa ya wokovu jijini Dar es salaam yalikuwa Temeke na Ilala na tulikuwa tukifaanya kazi ya Mungu kwa Nguvu,Upendo na Ushirikiano mkubwa.Tulifanya kazi hiyo kwa muda mrefu ilipofikia Miaka ya Themanini ndipo Mikutano ya Injili ilianza.


No comments:

Post a Comment