Home

Friday, April 27, 2012

Kufuatia Uvumi wa kuwepo dhahabu Madhabahuni,Uchimbuaji dhahabu kanisani wakwama



Zoezi la kuchimbua dhahabu inayodaiwa imefukiwa ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli (KKKT), Dayosisi ya Kusini Usharika wa Brandt wilayani Mbarali mkoani Mbeya, hatimaye limesitishwa kufuatia kutokea vurugu za wananchi na kuhatarisha amani hali iliyopelekea polisi kuingilia kati ili kuepusha ghasia zaidi.
Kusitishwa kwa zoezi hilo kuliamuliwa jana na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele na imeelezwa kuwa shughuli hiyo itaweza kuendelea  ama kutokuendelea kadri uongozi wa kanisa hilo utakapojadili yaliyojiri katika zoezi hilo.

Mchungaji wa Kanisa la KKKT Usharika wa Brandt, Emanuel Lunda, akizungumza na NIPASHE iliyofika katika kanisa hilo lililopo kijiji cha Ihahi, alisema uchimbaji wa  madini hayo  uliokuwa ukifanywa ndani ya kanisa hilo karibu na madhabahu ulilenga kutafuta dhahabu ambazo kama zingepatikana  zingeuzwa na fedha zingetumika kujenga kanisa jipya la kisasa.

Alex Malasusa Askofu mkuu wa kanisa la KKKT nchini
Alisema kabla ya vurugu hizo kutokea na kutolewa amri ya kusitishwa kwa zoezi la uchimbaji, tayari walikuwa wamechimba urefu wa zaidi ya futi 10, lakini hakuna dhahabu iliyokuwa imepatikana.
Mchungaji Lunda alisema pia fedha hizo ambazo zingetokana na mauzo ya dhahabu, zingetumika kujenga nyumba ya mchungaji na ya Mwinjilisiti wa mtaa wa kanisa hilo pamoja na kuweka huduma ya umeme katka kanisa jipya ambalo lingejengwa kwa gharama ya Sh. milioni 40 ambayo ilikuwa imetathiminiwa.

Alisema tetesi za kuwepo dhahabu ndani ya kanisa hilo lililojengwa miaka ya 1905 na Wajerumani, kwa muda mrefu zilikuwa zikienezwa na baadhi ya wakazi wa kjijiji cha Ihahi ambapo Mkuu wa Jimbo la Chimala, Laulent Ng’umbi naye alidokezwa suala hilo ambaye naye aliwaeleza viongozi wa Dayosisi ya Kusini na hivyo ikaamuliwa ufanyike utafiti wa madini hayo kwa kuchimba ndani ya kanisa.

Alisema mwanzoni mwa Aprili mwaka huu uongozi wa Dayosisi, Jimbo na Usharika baada ya majadiliano ya suala hilo, waliitwa wataalam wa madini ambao walipima ndani ya kanisa kwa kutumia vifaa maalum vya kutafuta madini ambao walipima mara tatu kwa nyakati tofauti na kugundua  kulikuwa na madini ndani ya kanisa hilo.
Mchungaji Lunda alisema mara ya tatu wataalam hao walipofika katika kanisa hilo kwa ajili ya kupima madini hayo waliambatana na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kusini, Mwamisole, Mkuu wa Jimbo la Chimala, Laulenti Ng’umbi, Mchungaji Mbilinyi wa Jimbo la Chunya na Mkuu wa Jimbo la Mtwara-Lindi, Mchungaji Mbedule.

“Ilipofika Aprili 18 niliitwa makao makuu ya Dayosisi Njombe ambapo Askofu Mengele wa Dayosisi ya Kusini, alinieleza kuwa suala la kuwepo dhahabu ndani kanisa la KKKT Usharika wa Brandt limejadiliwa kwenye mkutano mkuu wa Dayosisi na kwamba hakuna jinsi ni lazima utafiti ufanyike,” alisema Mchungaji Lunda.

Aliongeza kuwa kabla ya zoezi la kuchimba dhahabu ndani ya kanisa kuanza, kuliitishwa kikao cha wazee wa kanisa na viongozi ambacho kilihudhuliwa na wajumbe 14 wakiwemo wazee wa kanisa, wajumbe kutoka kamati ya majengo, idara ya vijana, idara ya wanawake na wazee maarufu wa kijiji cha Ihahi.

Alisema wajumbe wa kikao hicho walipendekeza kuwa wakati wa zoezi la kuchimba dhahabu ndani ya kanisa kuwe na usimamizi wa viongozi na waumini ili kusitokee ujanja wa kuibiwa madini na pia madini yatakayopatikana yauzwe na fedha zitakazopatikana zitumike kujenga kanisa jipya la kisasa, nyumba ya mchungaji, nyumba ya mwinjilisti na kuweka huduma ya umeme.

Mchungaji Lunda alisema siku ya Jumatatu Aprili 23, wachimbaji madini waliokuwa wametafutwa na kanisa walianza kazi kwa usimamizi wa karibu na Katibu Mkuu wa Dayosisi, Mwamisole, Mkuu wa Jimbo la Chimala, Ng’umbi Mkuu wa Jimbo la Mtwara-Lindi, Mbedule Mchungaji wa Usharika wa Brandt (Lunda) na Mwinjilisti wa Mtaa, Martin Msigwa.

Alisema zoezi la kuchimba dhahabu lilianza kati ya majira ya saa 7:00 na saa 8:00 mchana ambapo makubaliano ilikuwa kazi hiyo iwe inafanyika hadi nyakati za usiku, ilipofika siku ya Jumanne saa 12:00 jioni alikifika Mwenyekiti wa Kijiji cha Isitu aliyefahamika kwa jina la Mama Mkwembe ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Ihahi alianza kuhoji ni kwanini kanisa linachimbuliwa.
“Huyu Mwenyekiti wa kijiji cha Isitu alipokuja alianza kufoka na kueleza kuwa ninyi mna uroho wa utajiri na kutishia kutoa taarifa polisi lakini hakuna aliyemjibu kwasababu tulijua suala hili limefuata taratibu zote na kuruhusiwa na viongozi wa kanisa,” alisema Mchungaji Lunda.
Aliongeza kuwa baadaye Diwani wa kata ya Ihahi, Mtendaji wa kata ya Ihahi na Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihahi nao walifika katika kanisa hilo lakini walipopewa maelezo ya jinsi zoezi hilo linavyoendeshwa walilidhika na kukubali kuwa liendelee sababu limefuata taratibu zote za kanisa hilo.

Mchungaji Lunda alisema siku hiyo ya Jumanne majira ya  saa 6:30 usiku Mwenyekiti wa Kijiji cha Isitu akiwa na askari mmoja aliyetajwa kwa jina la Allen Mwamaja walifika katika kanisa hilo na askari huyo alianza kufoka kutokana na zoezi hilo na kisha kumnyang’anya simu ya mkononi na kuondoka nayo.

Kwa mujibu wa mchungaji huyo, ilipofika saa 8:00 usiku walifika askari wengine zaidi ambao waliingia ndani ya kanisa hilo na kuchukua kamera ya video, kamera ya kawaida, sururu, beleshi (sepetu), tochi, redio na viatu vya mmoja wa wachimbaji na kuondoka navyo hadi kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Chimala.
Mchungaji Lunda alisema kutokana na vurugu hizo, Askofu Mengele wa Dayosisi ya Kusini, alitoa amri zoezi hilo lisitishwe na shimo lifukiwe kazi ambayo tayari imekwishatekelezwa.

Hii ni mara ya kwanza kanisa kuchimbuliwa kusaka dhahabu inayodaiwa kufukiwa ndani yake. Ingawa maeneo mbalimbali nchini kwa sasa yanadaiwa kuwa na dhahabu hakuna kokote ambako inadaiwa kuwa yamefukiwa na mtu.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment