Home

Thursday, April 19, 2012

Mch Edward Amri asema ni Marufuku Kuilaumu serikali

Mchungaji Edward Amri

Mchungaji Edward Amri wa huduma ya Amri Kuu za Mungu (AKUZAMU) amewapiga marufuku waumini wake kuacha kuilaumu Serikali kwani haisaidii chochote katika maisha yao na kufanya hivyo ni kinyume na Neno la Mungu.

Akifundisha Neno la Mungu katika ibada kanisani hapo alisema ifikie mahali Watanzania wajiulize nini wataifanyia nchi yao, kwani sisi kama Kanisa lazima tuwe Baraka kwa Taifa na siyo kugeuka wapinzania kwa kuilaumu serikali; kinachotakiwa kila Kanisa liwe na utaratibu wa kuwasaidia waumini wake kwa kuwapa mafundisho ya namna ya kujikwamua kiuchumi, likiwepo suala la kuwahamasisha waweze kujiajiri ili waweze kuisaidia serikali katika kutoa ajira na kulipa kodi kwa usashihi.

“Kazi ya Kanisa ni kuisaidia serikali na siyo kuipinga na kuwatengeneza watu wake yaani waumini kuwa raia wema wenye kuipenda nchi yao likiwepo suala la kuwakwamua watu kiuchumi kwa kuwafundisha mafundisho sahihi ya uchumi katika ufalme wa Mungu, kama ambavyo kanisa letu linafanya ambapo muda si mrefu sisi tutakuwa Baraka katika Taifa kwani waumini wetu wengi wataajiri na watakuwa na walipakodi wazuri katika nchi yetu”.

Akiongea kwa kujiamini alisema kwa sasa uchumi wa dunia nzima umekwama na sababu yake ni kwamba ni vigumu sana uchumi wa mfumo huu kufaulu kwa sababu hauna mbadala, yaani ziada kwani masomo hayo ya uchumi yanayofundishwa shuleni miaka 20 iliyopita ndio hayo hayo yanafundishwa hivyo wachumi wetu hawawezi kuwa na la ziada zaidi ya kujifunza masomo ambayo wenzao waliyagundua zamani na ndio maana hadi hivi sasa hawawezi kutoa majibu ya kuboresha maisha ya wananchi.

Akitoa mfano alisema kwa sasa nchini kwetu hatuna vitu ambavyo tumegundua. Kwa mfumo wa uchumi wa kwenye makaratasi hauwezi kutoa majibu kwani hata hao wachumi endapo masomo yangekuwa na hatimiliki nadhani sisi tusingekuwa na kitu kwani masomo hayo tunakopi kutoka kwa wenzetu ambapo hatuwezi kuwa na mbadala na ndio maana unaweza kukuta tunao wasomi wengi wa uchumi wasipoajiriwa hawawezi kuishi wanachanganyikiwa maana hawana mbadala
Akieleza mikakati ya Kanisa lake amesema wao wameamua kuisaidia serikali badala ya kuilaumu kwa kuwaelimisha waumini wao masuala ya uchumi katika ufalme wa Mungu kwa kutumia Neno la Mungu, pamoja na kuwahamasisha juu ya umuhimu wa kujiajiri ili waweze kuwaajiri wengine.

Rev Edward Amri  akiwa na mkewe mama Susanne

Akijitolea mfano yeye alisema kabla hajaanza kumtumikia Mungu alijiajiri kwa kufungua biashara ambapo miaka hivi sasa anao wafanyakazi wasiopungua mia moja wanaofanyakazi katika biashara zake hivyo amekua msaada kwa serikali kwa kuipunguzia kero ya ajira kwani ameajiri na analipa kodi serikalini hivyo amekua Baraka kwa nchi.

Mbali na hilo amekuwa na mkakati wa kuwahamasisha wale aliowaajiri kutojisahahu badala yake nao wafungue biashara zao nao waweze kuajiri watu wengine kwani ifikie hatua tuipunguzie mzigo serikali badala ya kuilaumu.
Amekemea tabia ya baadhi ya watumishi pamoja na waumini kuilaumu serikali kwa kusema eti inasababisha hali ngumu jambo ambalo amesema si kweli kwani mazingira ya sasa karibu nchi zote zimekwama ni wakati wa Kanisa kuisaidia serikali kwa kuwafundisha waumini Neno la Mungu kwa usahihi pamoja na kuwasaidia kujiajiri badala ya kutumia muda mwingi kuilaumu serikali jambo ambalo si sahihi.

Tangu mwaka 2012 Kanisa la Akuzamu chini ya kiongozi wake Mchungaji Edward Amri limeanzisha kampeni kabambe kuisaidia serikali kwa kuiombea pamoja na kuwahamasisha waumini wake kujiajiri na kuwaajiri wale ambao bado hawana ajira ambapo pia limekuwa likitoa mafundisho ya uchumi kila siku katika ukumbi wa IPS Jijini Dar es salaam na kila mwezi, ambapo mwezi ujao linatarajia kuendesha semina kubwa itakayofanyika katika ukumbi wa Nadd’s ulioko salender bridge jijini Dar es salaam tarehe ishirini na tano mwezi ujao ambapo wengi wamekuwa wakihudhuria na mara baada ya mafundisho wengi wamebadilika katika ufahamu wao na wameanza kuchukua hatua ya kujiajiri.

No comments:

Post a Comment