Home

Monday, April 16, 2012

NAMNA YA KUJENGA MAHUSIANO MAZURI NA ROHO MTAKATIFU.



Yohana 14:16-17. Biblia inasema “ Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele, ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni, wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”. Ukiaangalia vema mistari hiyo miwili hapo juu utagundua Yesu alikuwa akiwaambia wanafunzi wake mambo yafuatayo;Moja, alikuwa akiwaaga na kwa hiyo akawaambia nitamwomba Baba awape msaidizi mwingine ambaye ndiye Roho wa kweli yani Roho mtakatifu.
Mbili, huyo msaidizi ulimwengu hauwezi kumpokea kwa kuwa haumwoni na wala haumtambui.


Tatu, wanafunzi wake watampokea kwa sababu kwanza wanamtambua na kisha atakuwa ndani yao. Ukisoma kile kipengele cha mwisho kinasema “Bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”
Sasa leo nataka nizungumzie kipengele cha mwisho kinachosema “naye atakuwa ndani yenu”. Biblia inasema atakuwa, maana yake ni tendo la wakati ujao, au si la sasa au kwa lugha nyingine ni baada ya vitu fulani kufanyika. Roho mtakatifu kukaa ndani yako ni kwa ajili yako wewe binafsi. Hii ina maana atakua ndani yako kwa ajili ya kukusaidia uweze kulitumika shauri la Bwana katika kizazi chako.

Ili Roho mtakatifu aweze kuwa ndani yako na kukuongoza vema katika njia unayopasa kuiendea ni lazima ufanye maamuzi ya ndani ya kumruhusu akae ndani yako kwa kujenga mahusiano mazuri katika maisha yako au kiwango cha yeye kukusaidia katika maisha yako binafsi.Mambo yafuatayo yatakusaidia kujenga mahusiano mazuri na Roho mtakatifu ili akusaidie;
*Kuliweka neno la kristo kwa wingi ndani yako.

Wakolosai 3:16.Hakikisha kila siku unatenga muda wa kutosha wa kusoma na kulitafakari neno la Mungu. Unapolitafakari neno la Mungu, ndivyo jinsi linavyokaa kwa wingi moyoni mwako.
*Kutenga muda wa kuwa pamoja naye.

Jifunze kujenga mahusiano na Roho mtakatifu kama rafiki yao, usimuone kama ni adui. Kumbuka yeye ni msaidizi na bila yeye huwezi lolote. Mara nyingi marafiki wazuri huwa wanakuwa na muda wa kutosha wa kuwa pamoja. Hivyo jifunze siku zote kutenga muda wa kuongea naye kwa maombi na pia kutulia tu ili na wewe usikie kutoka kwake.
*Kutafakari mambo ya Rohoni.


Warumi 8:5bSiku zote jifunze kutafakari mambo ya roho. Kutafakari mambo ya roho ni ile hali ya kutumia muda wako mara kwa mara kutafakari zaidi juu ya Roho mtakatifu na kazi zake na kisha kukaa kwenye mkao wa kusikiliza kila analokuagiza.
*Kuwa mtiifu kwake.

Yesu alipomtambulisha Roho mtakatifu kwa wanafunzi wake aliwaambia moja ya kazi zake itakuwa ni kuwafundisha na kuwakumbusha yale yote aliyowaambia (Yohana 14:26). Sasa kitu cha muhimu kuliko vyote ili kuboresha mahusiano yako na Roho mtakatifu ni wewe kuwa mtiifu kwake kwa kila analokuagiza.
Watu wengi wameshindwa kumpa Roho mtakatifu heshima kisa lile neon linalosema yeye ni msaidizi. 

Nisikilize kama umesoma mstari wa mwanzo kabisa vizuri utagundua kwamba hata Yesu alikuwa ni msaidizi, Neno msaidizi halina maana yuko chini yako kibiblia. Ina maana unahitaji msaada wake ili uweze kufika unakotakiwa kwenda na bila yeye hutaweza. Hivyo mpe Roho mtakatifu nafasi ile ile uliyompa na Yesu pia.

Asikiaye na afahamu
  Ndimi Sanga P.S.

No comments:

Post a Comment