Home

Tuesday, May 29, 2012

Kanisa Lingine Lachomwa Zainzibar


Rais wa Zanzibar Dr Ali Mohamed  Shein
BAADA ya Kanisa la Assemblies of God kuchomwa moto katika vurugu zilizoanza mwishoni mwa wiki iliyopita, jana Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae nalo limechomwa moto.

Akizungumzia hali hiyo jana, kiongozi wa Kanisa hilo, Ambaros Mkenda, alidai kwamba Kanisa hilo lilichomwa moto na watu wasiojulikana na kusababisha uharibifu mkubwa.

Alidai Kanisa hilo lilichomwa moto jana saa 8.30 mchana na watu wanaohisiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho, waliokuwa wakitoka katika Mahakama ya Mwanakwerekwe kusikiliza kesi ya wenzao waliokamatwa juzi.

Mkenda alidai kuwa watu hao waliwazidi nguvu walinzi wawili wa Kanisa hilo na kuvunja lango kuu la kuingilia ndani ya Kanisa na kuchoma moto na waliharibu madirisha na vifaa kadhaa vyenye thamani ya Sh milioni 20.

“Tunasikitika sana na uharibifu mkubwa uliofanywa katika Kanisa letu ambalo lilikuwa tegemeo kubwa kwa wafuasi wapatao 2,000 wa eneo la Parokia ya Mpendae na jirani,” alisema Mkenda.

Mkenda alidai kuanzia juzi, viongozi wa makanisa mbalimbali waliwasilisha maombi yao Polisi kuhusu kupewa ulinzi katika nyumba za ibada, baada ya kupokea vitisho. Hata hivyo, Mkenda alidai ombi lao hilo halikutekelezwa na Polisi na uharibifu mkubwa ukatokea katika Kanisa la Assemblies of God la Kariakoo.

Wafuasi na waumini wa Kanisa hilo walikusanyika nje ya jengo hilo, huku vijana wakishikwa na hasira wakitaka kwenda kulipiza kisasi katika maeneo ya jirani wakidai wanawatambua vijana waliofanya vitendo hivyo.

Mmoja wa waumini wa Kanisa hilo ambaye ni mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Susan Kunambi alilazimika kuwatuliza wafuasi vijana wa Kanisa hilo waliopandwa na jazba wakitaka kulipa kisasi.

“Hakuna sababu ya kupandisha jazba na kutaka kufanya vitendo ambavyo vitasababisha hasara na uharibifu ... Kanisa siku zote linahimiza amani na upendo na si chuki,” alisema Kunambi

Polisi walifika haraka katika eneo la tukio na kurusha mabomu ya machozi ili kutawanya makundi ya vijana waliojikusanya na wengine kurusha mawe.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alithibitisha kuchomwa moto Kanisa hilo na kusema ulinzi umeimarishwa katika baadhi ya maeneo ya nyumba za ibada yakiwamo makanisa. Baadhi ya mitaa ya Jang’ombe na Mwanakwerekwe njia zimewekwa mawe na vikundi vya vijana waliochoma mipira ya gari na kusababisha moshi mkubwa.



Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment