Home

Wednesday, October 31, 2012

Soma Barua Ya Wazi Kwa Rais Wa Zanzibar Kutoka Kwa Kiongozi Wa Maimamu Zanzibar,Farid Hadi Ahmed



Kiongozi Wa Maimamu Zanzibar,Farid Hadi Ahmed

Kila sifa njema zinamstahikia Allah, Subhanah wa Taala, isofichikakwake dhulma wala harudishi dua ya mwenye kudhulumiwa. Rehma na amani zimshukie Mtume Muhmmad (s.a.w) kipenzi chake na cha umma, mtetezi wa waliodhulimiwa hata kabla ya kupewa Utume.Mhishimiwa Rais,Kwa mapenzi makubwa, baada ya kuisoma kwa utulivu khutuba yako ya siku tukufu ya Iddil Alfitri, nimelazimika kuandika barua hii kufuatana na kauli mbiu ya Mtume Muhammad (s.a.w) inayosema:


“…Dini ni nasaha…nasaha kwa Allah (S.w.T) na ni nasaha kwa Mtume (s.a.w.) na kwa viongozi wa Waislamu na kwa watu wote…”

Mh. Rais;
Ni kweli nchi yeti ya Zanzibar imechafuliwa jina lake kuwa ni nchi ya amani kama ilivyogeuzwa nchi yetu na ndugu zetu na kufanywa kuwa ni koloni lao baada ya mkoloni Mwingereza kutupa uhuru mwaka 1963 na kuwa na kiti chetu Umoja wa Mataifa huku walimwengu wote wakishuhudia; kiti ambacho kwa uwezo wake Allah atakirejesha karibuni na wewe ukiwa rais wa Zanzibar au uliyemwakilisha kuweza kuketi juu yake Insha’allah na sisi wananchi wako wa Zanzibar tukifurahikia jambo hilo adhimu.

Mh.Rais;
Ni kweli nchi yetu inatiwa dosari lakini si kweli kuwa wananchi wa Zanzibar ndio wanaosababisha dosari hiyo na doa hilo la uvunjifu wa amani; ushahidi wa maneno haya tutaupata tukirejea na kutizama kwa jicho la uadilifu na insafu katika matukio tafauti. Kwa hakika tukifanya hivyo tutagundua bila ya taabu kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania ndio wahusika wakuu na waanzilishi wa vurugu na uvunjifu wa amani ya nchi yetu ya Zanzibar kwa mara zote tatu, nikimaanisha machafuko yaliyotokea tarehe 25-26/5/2012 mjini Zanzibar na yale ya kuhujumu waumini na kunajisi misiskiti tarehe 17/6/2012, Donge, Mahonda na Mkokotoni pamoja na hujuma ya tarehe 20/7/2012 msikitin pia dhidi ya Waislamu walokusanyika msikiti wa Mbuyuni kuwasalia ndugu zao waliofariki kwa ajali ya meli ya Mv. Skaget. Waislamu tulihujumiwa ndani ya msikiti.

Jeshi la polisi halikusita hapo bali liliwaingilia  wananchi wanyonge mpaka ndani ya nyumba zao na kuwatendea matendo haramiya ya chuki na uhuni na katika waliotendewa matendo hayo maovu walikuwa wanawake na watoto wachanga. Polisi hao wakhalifu wa sharia waharibifu wa amani walifika hadi ya kutupa mabomu ya madawa makali ndani ya majumba ya raia bila ya kujali athari zitakazowasibu watoto wachanga na wanawake wenye kunyonyesha.Iwapo jeshi la polisi lililopewa jukumu la kulinda sharia, kuweka amani na kuwahami wananchi na mali zao ndio wenye kuvunja shariakwa kuwahujumu watu bila ya

sababu, wananchi na haki zao zitalindwa na nani?

Mh.Rais;
Matokeo ya ukiukwaji wa sharia na haki za binadamu yaliyopelekea kuiharibia nchi yetu ya Zanzibar sifa yake ya amani na utulivu yamesababishwa na jeshi la polisi la Tanzania lililoacha kutekeleza wajibu wake wa kutunza amani ya nchi yetu Zanzibar . La kusikitisha zaidi ni kuwepo baadhi ya watendaji wako wa karibu wanaopotosha ukweli na kuifanyia khiyana nchi yetu ya Zanzibar kwa kufikisha kwako taarifa za uongo zilizopelekea kuitia doa na kuiharibu khutuba yako ilojaa maneno matukufu ya Allah Subhanah wa Taala pamoja na mafunzo kutoka Sunna za Mtume (s.a.w), khutuba ambayo ilitarajiwa kukemea dhulma za jeshi la polisi dhidi ya Waiislam na nyumba tukufu za Allah (S.w.T) iliyohujumiwa pamoja na wanawake na watoto wachanga ndani ya majumba kama ulivotetea makanisa na kubainisha hatari na ubaya wa walioyachoma makanisa hayo kwa lengo la kutaka kuanzisha fitna baina ya Waislam na jirani zao Wakristo waliokaribishwa nchini Zanzibar na kuishi pamoja nao miaka mingi kwa amani kiasi ambacho haijawahi kutokea Muislamu kulitusi kanisa licha kulichoma moto, kwani hayo ni kinyume na mafunzo
ya dini yetu tukufu ya Kiislamu.


Mh.Rais;   Watu wanaokuwa karibu na Rais ni watu muhimu sana katika kufanikisha dhana ya uadilifu na utawala bora na wa haki usioogopa kukemea maovu hata kama walotenda au kuteleza ni Jeshi la Polisi kwani pia wao ni binaadamu siajabu kutenda makosa kwa maksudi seuze kuteleza, Allah Sbhanah wa Taala anatwambia: “…Enyi mloamini kuweni wasimamizi wa Allah wenye kushuhudia ukweli hata kama ni dhidi ya nafsi zenu…” Kwa hivyo, kosa kubwa zaidi ni kuuficha ukweli au kumpotosha kiongozi wa nchi hadi kufikia kuwashushia sifa wasiostahiki, wahuni ambao waliwatendea ya uhuni na dhulma kubwa hata wanawake na watoto.

Ni khatari wadhulumiwa wanapofikishwa kumshtakia Mfalme wa Mbingu na Ardhi juu ya dhulma wanazotendewa. Isitoshe, khiyana ya watu kamaa hao wa karibu na viongozi kila inapojikariri khiyana hiyo inajenga hisiya kwa wenyeji wa nchi hii ambao wengi wao ni Waislamu kuwa wanabaguliwa,  na sio wao tu bali hata kudharauliwa nyumba zao tukufu za ibada na kuthaminiwa makanisa peke yake. Sisi Waislamu hatutaki nyumba zozote za ibada zidharauliwe.Nyumba zote za ibada lazima ziwekewe hishima zinazostahiki.


Mh.Rais;
Kwa heshma zote naomba zichunguzwe sana sifa mbili kwa watu wote wa karibu na viongozi, sifa mbazo ni hatari kuzikosa tena zinaweza kuiangamiza nchi yetu tukufu ya Zanzibar . Sifa hizo si nyengine illa  ni ukweli na uaminifu ambazo ni kinyume na uwongo na khiyana.


Yarabbi Muumba Mbingu na Ardhi, usieshindwa na jambo, tunakuomba muhifadhi Rais wetu, turejeshee nchi yetu kwa salama na amani, DOLA HURU YA ZANZIBAR, wastiri wanawake na watoto wachanga majumbani na Wazanzibari wote tunaodhulumiwa kwa kudai uhuru wa nchi yetu ya

Zanzibar uloporwa na jirani zetu, ndugu zetu baada ya kutoka kwa wakoloni.

Amir Mkuu,
Jumuiya ya Maimamu Zanzibar

Farid Hadi Ahmed


Source: Chediel Charles wa Rundugai

No comments:

Post a Comment