Home

Sunday, July 24, 2011

Sunday Sermon: Namna Ya Kumtumia Roho Mtakatifu Kama Msaidizi Kupitia Kazi Zake


Yohana 14:16-18 … Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni, wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”.

Katika somo hili nataka kuandika juu ya kazi za Roho Mtakatifu na kukuonyesha namna unavyoweza kumtumia Roho Mtakataifu kama Msaidizi kupitia kazi zake. Labda niseme kwa lugha hii, kama unataka kuona msaada wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yako, ni lazima kwanza uzijue kazi zake, maana kazi zake ndizo zinazotuonyuesha maeneo ya msaada wake, kazi zake ndizo zinazofafanua kwa namna gani Roho Mtakatifu ni Msaidizi.

Roho Mtakatifu ni nani?
Roho Mtakatifu ni Mungu, mwenye nguvu zote, maarifa yote, anayepatikana kila mahali. Yeye anayo nafsi na ameamua kuishi ndani ya mwili wa mwanadamu. Kusudi kubwa la ujio wake ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu kwenye ulimwengu huu wa mwili, ili kumsaidia kuishi katika mapenzi ya Mungu.

Roho Mtakatifu amemamua kuishi ndani ya mwili wa mtu kwa sababu, Mungu hana namna ya  kutawala kwenye ulimwengu wa kimwili bila kuwa na mwili wa damu na nyama, kwa kuwa yeye ni Roho (Yohana 4:24). Hivyo hana budi kuingia kwenye mwili wa mtu na kufanya makao yake hapo, ili kutawala na kumuongoza mwanadamu katika mapenzi yake. (Yohana 14:23, Yohana 14:18, Ufunuo 3:20, 1Wakorinto 3:16-17, 6:19).

Kinachotusaidia kujua kwamba Roho Mtakatifu ana nafsi, ni tabia zake, maana kwenye kila nafsi kuna hisia, nia, kumbukumbu, akili nk. Baadhi ya sifa na tabia za Roho Mtakatifu ni;
1.      Anapatikana kila mahali (Omnipresence), Zaburi 139:7,
2.      Ana maarifa/anajua yote (Omniscient, Intelligence), 1 Wakorinto 2:10-11,
3.      Mwenye nguvu zote/wa umilele (Omnipotent), Mwanzo 1:2,
4.      Mtakatifu, Luka 11:13, ana hisia (Waefeso 4:30, Mwanzo 6:3) – Wala msimuhuzunishe Roho wa Mungu…, Roho yangu haitashindana na Mwanadamu milele, ana nia (will), 1Wakorinto 12:11 – Hutenda kazi kama apendavyo.

Kazi za Roho Mtakatifu
  • Kufundisha, Mwalimu (Yohana 14:26) … Atawafundisha yote…
  • Kuongoza, Kiongozi (Warumi 8:14, Yohana 16:13) – Atawaongoza awatie kwenye kweli yote, wote wanaoongozwa na Roho hao ndio … Mfano (Matendo ya Mitume 13:4, Acts 8:29)
  • Ni mfunuaji wa mambo/mafumbo/siri za Mungu (1Wakorinto 2:10) – Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote. Usipoteze muda kumtaka Mungu akufunulie siri zake, wewe mwambi Roho Mtakatifu hiyo ndiyo kazi yake.
  • Muombezi (Warumi 8:26) – Roho hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
  • Mtoa/mpasha habari za mambo yajayo (Yohana 16:13f) – Na mambo yajayo atawapasha habari yake.
  • Ni msemaji wa mambo ya Mungu/Yesu (Yohana 15:26, 2 Petro 1:21) – Yeye atanishuhudia (he will speak about me), Wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
  • Ni mtetezi/msemaji wa mambo yetu (Marko 13:11) – Kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu.
  • Ni mkumbushaji wa yale uliyojifunza au uliyoagizwa na Mungu (Yohana 14:26)… Atawakumbusha yote niliyowaambia.
  • Kutia/kuwapa nguvu watu wake nguvu/uwezo (Matendo1:8) – Lakini mtapokea nguvu akisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu…
  • Kuuhakikisha (convict, make aware, sadikisha) ulimwengu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu (Yohana 16:8) e.g unajuaje kwamba kuna hukumu? Warumi 8:16
Naam kazi hizi za Roho Mtakatifu zinatufikisha mahali pa kujua kwamba jukumu lake kubwa ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu. Kufanyika msaada wa mwanadamu katika mambo hayo hapo juu pale mwanadamu atakapohitaji msaada huo.  Hivyo ni jukumu lako kumpa nafasi kwa kuboresha mahusiano yako na yeye ili akusaidie. Hata hivyo Roho Mtakatifu kuitwa Msaidizi haina maana kwamba ndio umvunjie heshima, bali fahamu kwamba, Roho Mtakatifu ni Msaidizi kwa namna ambayo bila yeye mimi na wewe hatuwezi kutenda neno lolote.

Kazi hizi zinatupa kujua kwamba Roho Mtakatifu yupo tayari kutusaidia katika kila eneo la maisha yetu. Ni jukumu letu kumpa  nafasi hiyo na kutambua kwamba bila msaada wake sisi hatuwezi lolote. Watu wengi leo hawaoni msaada wa Mungu kwao kwa sababu ya kutokumpa Roho Mtakatifu nafasi ya kuwasaidia katika maisha yao na pia kwa kutokujua maeneo ya kumtumia Roho Mtakatifu kama Msaidizi.


Je, unahitaji msaada wa Roho Mtakatifu eneo gani la maisha yako?, ni ndoa, kazi, madeni, huduma, kanisa, utawala nk mpe nafasi akusaidie, akufundishe na kukuongoza katika kweli yote. Kumbuka yeye ni Mungu ambaye ni Mwalimu na Kiongozi pasina yeye mimi na wewe hatuwezi neno lolote. Unataka kumjua Mungu, kuwa na maombi yenye matokeo mazuri na kufanikiwa katika maisha yako kiroho na kimwili pia mwambie Roho Mtakatifu akusaidie.

Msaada wa Roho Mtakatifu hauna mipaka maadamu unahitaji msaada katika yale ambayo ni mapenzi ya Mungu. Hivyo haijalishi unapita katika jambo gani mpe nafasi Roho Mtakatifu akusaidie. Na ili uweze kuthamini msaada wa Roho Mtakatifu jifunze siku zote kufikiri kwa dhana kwamba bila msaada wake wewe huwezi lolote, na kwa sababu hiyo utaona umuhimu wa yeye kukusaidia katika maisha yako.

Usisubiri mambo yako yaharibike au usiachague mambo unayofikiri magumu ndio umshirikishe akusaidie, yeye anataka kuwa Bwana wa maisha yako, akusaidie kwa kila kitu hata mambo madogo kabisa kwenye maisha yako. Kina-muumiza Mungu kuona watoto wake chini ya jua wanahangaika katika maisha yao, wakati yeye amemleta Roho Mtakatifu ili awasaidie katika maisha hayo. Tumia vizuri fursa ya Roho Mtakatifu sasa maadam anapatikana, kuna wakati hatapatikana.

 Neema ya Kristo iwe nawe
 Na:Patrick Sanga

No comments:

Post a Comment