Home

Tuesday, April 3, 2012

Kwa Nini Bwana Yesu Alituombea Umoja? Mwl C. Mwakasege 1


Mwl Christopher Mwakasege

Mungu tunayemwamini katika Yesu Kristo, ni Mungu wa mipango na makusudi kamili. Tangu vizazi na vizazi tabia hii ya Baba yetu, imejidhihirisha wazi.Baba yetu huyu, ambaye pia, ni Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, hawezi kufanya kitu au kusema kitu, bila ya kuwa na sababu.

Mungu aliumba dunia hii, kwa kusudi kamili, ili ikaliwe na watu isiwe tupu.Mungu aliumba jua, mwezi, sayari na nyota mbali mbali, kwa makusudi kamili, ili viwe ndiyo dalili za majira na siku na miaka na tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi.

Mungu alimtokea Musa katika kijiti kilichokuwa kikiwaka moto, kwa kusudi kamili, ili apate kuwatoa watu wake, wana wa Israeli kutoka Misri.Mungu alimtoa Mwana wake wa pekee Yesu Kristo, kwa kusudi kamili, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Mungu alimwaga Roho wake Mtakatifu juu ya watu wake, kwa kusudi kamili, ili wapate nguvu ya kuwawezesha kuwa mashahidi wa Kristo katika ulimwengu mzima.
Ni kweli kabisa ya kwamba, Mungu tunayemwamini katika Yesu Kristo, ni Mungu wa mipango na makusudi kamili. Hafanyi kitu bila ya kuwa na sababu nacho.Kwa hiyo alipokuwa akisema na watumishi wake, alikuwa na kusudi na ujumbe kamili kwa ajili ya watu wake.

Na aliponiita kwenye utumishi wake alikuwa na mipango na makusudi kamili kwa ajili ya watu wake. Kwa hiyo niliposikia sauti yake ndani ya roho yangu nilipokuwa kwenye mkutano wa ‘Easter Crusade’, Tukuyu, Mbeya Aprili 1987, nilijua hakika ya kuwa kuna jambo la muhimu.
Nilisikia sauti ya Bwana ndani ya roho yangu ikisema; “NATAKA KUSEMA NA WATU WANGU”.

Si kwamba nilisikia sauti kama ya mtu akiongea; hapana; bali kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu, nilisikia sauti hiyo ndani ya roho yangu. Na nilijua hakika ya kuwa hiyo ni sauti ya Bwana wangu na Mwokozi wangu. Hata Yeye alisema kuwa ndiye pekee aliye mchungaji mwema, walio wake anawajua, na wao wanamjua, na sauti yake wanaijua (Yohana 10:1-6).

Mkutano huo wa kiroho ulikuwa umejumuisha watu wa Mikoa mbali mbali na pia watu wa madhehebu mbali mbali. Na Bwana aliposema nami kwamba anataka kusema na watu wake ilikuwa ni mchana wa siku ya pili ya mkutano.
Kwa hiyo baada ya kusikia hivyo, nilitafuta mahali pa faragha katika chumba kimoja; nikapiga magoti, na nikawa tayari kusikia lile ambalo Bwana alikuwa anataka lisikike kwa watu wake.Maneno aliyoniambia yalihusu juu ya UMOJA WA WATU WAKE. Na waliokuwapo kwenye mkutano huo walipata nafasi ya kusikia kwa muhtasari tu, juu ya Umoja wa watu wa Mungu.

Maneno hayo ya Bwana  juu ya umoja wetu ni muhimu sana. Na kwa ajili hiyo, Roho wa Bwana ameniongoza kuyaandika kwa undani zaidi, ili watu wengi waweze kuyapata na kuyafanyia kazi.Jambo ambalo Bwana analiona katikati yetu, katikati ya wakristo, ni kukosa Umoja wa kweli. Na jambo hili linamhuzunisha sana Mungu. Hii ni kwa sababu watu wake ndiyo mwili wake (1Wakorintho 12:27). Kwa hiyo kukiwa na nyufa katika uhusiano wa mkristo na mkristo mwingine, maana yake mwili wake umepata nyufa.

Kusudi lake kubwa la kutulinda, kututunza, kutulisha, kututakasa na kutuongoza ni ili atulete mbele za Baba yetu aliye mbinguni, bila waa na wala kunyanzi.

Lakini, hali inayoonekana sasa ni ya kusikitisha. ‘Fellowships’ nyingi hazina umoja na zimetawaliwa na mafarakano. Viongozi wa Kanisa nao pia hawana umoja kila mmoja anafanya mambo yake mwenyewe, ambayo anayaona ni bora kuliko ya mwenzake. Vikundi vingi vya huduma za kikristo havina umoja wa kweli.

Yesu Kristo alituombea umoja. Je! Maombi yake yamejibiwa au bado? Na alikuwa na sababu gani alipokuwa anatuombea? Je! Yesu Kristo alikuwa na mpango wowote aliouandaa juu ya umoja wa mwili wake, ambalo ni Kanisa?Ni nini chanzo cha mafarakano na kukosa umoja katikati ya watu wa Mungu? Tufanye nini ili tupate kusimama katika umoja wa kweli?

Maswali hayo na mengine yanajibiwa katika somo hili.

Sasa, ngoja niseme jambo moja muhimu:

Mungu huyu tunayemtumika ni Mungu aliye na kusudi kamili, katika kila jambo analolifanya na kulisema. Na kwa mtazamo huu, nakuambia hivi, Mungu ameweka maandiko ya somo hili mikononi mwako kwa kusudi kamili, kwa ajili ya utukufu wa Jina lake Takatifu.
Kwanza: Kwa sababu anakupenda upeo, hapendi   upotee.
Pili: Kwa sababu wewe ni kiungo cha mwili wake, ambao ndilo Kanisa
Tatu: Kwa sababu anataka uhusike moja kwa moja katika kushirikiana na Roho wake Mtakatifu, ili kuwashirikisha wengine ujumbe huu.
Ni maombi yangu kwa Mungu katika Jina la Yesu Kristo aliye hai, ya kuwa Roho wake akutie nuru katika utu wako wa ndani upate kuyaelewa yote na kuyafanyia kazi ipasavyo. Na ukiishayasoma uwashirikishe wengine bila kuyapindua pindua.

Hizi ni siku za mwisho, na tunatakiwa tuwe waangalifu katika yote tunayoyasikia au kuyasoma. Tunatakiwa tuyachambue, na kuyapima, halafu tuyachukue yaliyo mema yanayotujenga pamoja na siyo kutubomoa.
Kwa hiyo nakushauri, katika Jina la Yesu Kristo, ya kwamba unapoyasoma yaliyomo humu, uwe na BIBLIA yako karibu upate kuifuatilia mistari yote niliyoinukulu. Bwana na akuwezeshe kuyatafakari na kuyafanyia kazi ili wote tuwe na Umoja kama Baba na Kristo walivyo umoja.
Sifa na Utukufu na uweza, na nguvu vina Mungu wetu katika Kristo Yesu, milele na milele – Amina.

Itaendelea

Mwl C Mwakasege

No comments:

Post a Comment