Home

Wednesday, October 31, 2012

Mzee wa Upako Asema – Tanzania ni Bora Kuliko Ukristo na Uislamu



Mchungaji Antony Lusekelo

KIONGOZI wa Kanisa la Maombezi la GRC na Ubungo, Dar es Salaam, Mchungaji Antony Lusekelo amewataka viongozi wa dini na Watanzania kwa jumla, kutambua kuwa Tanzania ni bora kuliko dini zao.
Mchungaji Lusekelo pia aliwataka viongozi wa dini kuendeleza vita dhidi ya rushwa huku akisema watoa rushwa na wapokeaji, wamejificha makanisani na kwenye misikiti.Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  ambapo alisema viongozi wa dini lazima lazima washiriki katika mapambano ya rushwa bila woga.

Katika mazungumzo hayo, mchungaji huyo pia alisema  Serikali inapaswa kuwajibika kwa kutumia nguvu zake za kisheria katika kulinda amani, huku akinyoshea kidole tukio la hivi karibuni lililoashira kuvunja kwa amani, huku Serikali ikiwa haijachukua hatua.Alisema hilo ni tatizo kubwa na kwamba  ni watu wengi wakiwamo viongozi wa dini kushindwa kusema ukweli kwa kuogopa maisha yao kuwa mafupi.

“Ni muhimu kila mwananchi kutambua kuwa  Tanzania ni bora kuliko Ukristo na Uislamu. Watu wengi wanaogopa kusema ukweli. Hata viongozi wa dini kwani watoa rushwa wamejificha misikitini na makanisani, tuendeleze mapambano dhidi ya rushwa ipo siku tutashinda,” alisema.Kuhusu vurugu nchini, alisema chanzo ni viongozi wa dini  kuhubiri siasa za chuki misikitini  na makanisani.

“Vurugu siyo asili ya binadamu inatengenezwa, Serikali ina wajibu wa kutumia nguvu yake kisheria kuilinda amani na amani haishuki kutoka mbinguni au kwa maombi, inatengenezwa pia. Tatizo cheche za kidini zilipoanza hazikudhibitiwa. Serikali ilikuwepo, aidha kwa makusudi au bahati mbaya imelea cheche hizo,” alisema Lusekelo.


No comments:

Post a Comment