Tuesday, May 8, 2012

Linda Sana Nafasi Aliyokupa Mungu Kwa Ajili Ya Kusudi Lake



Wimbo ulio bora 1:6 Msinichunguze kwa kuwa ni mweusi-mweusi, kwa sababu jua limeniunguza.Wana wa mamangu walinikasirikia, Waliniweka niwe mlinzi wa mashamba  ya mizabibu; Bali shamba langu mwenyewe sikulilinda’.

Haya ni maelezo ya Mtumishi ambaye alikuwa akiwajibu watu waliokuwa wanashangaa hali yake ya kimwili kwa sababu ya weusi wake. Kwa hiyo akaanza kuwaelezea kilichopelekea akawa hivyo, kwamba ni ugomvi baina yake na ndugu zake. Ugomvi huo uliamuriwa kwa makubaliano kwamba ndugu huyu apewe kazi ya kulinda mashamba yao ya mizabibu. Kwa maelezo yake binafsi tunagundua pia, kwamba yeye naye alikuwa na shamba lake la mizabibu.

Licha ya kwamba huyu ndugu mwili wake uliharibika kiasi cha watu kumshangaa lakini pia shamba lake binafsi ili hali yeye ni mlinzi wa mashamba liliharibiwa. Hii ni kwa sababu alilinda mashamba ya wengine lakini shamba lake  hakulilinda. Naam alitumia muda wote kulinda mashamba ya wengine la kwake akasahau.
Ukisoma toleo ya biblia ya Good News Bible (GNB)  katika mstari huu inasema ‘Don’t look down on me because of my color, because the sun has tanned me. My brothers were angry with me and made me work in the vineyard. I had no time to care for myself (Son 1:6)’.


Sasa kutoka katika tafsiri hii ndio tunagundua kwamba kumbe shamba linalozungumziwa hapa ni lugha ya picha ikiwakilisha maisha binafsi ya mtu (nafsi/mwili/roho). Hii ni kwa sababu katika maandiko haya huyu ndugu anatuambia sababu ya kuharibika kwa shamba lake binafsi ni kukosa muda wa kuilinda nafsi yake (no time to care for myself). Na kwa hiyo tunaweza kusema hali yake ya mwisho kimwili na kiroho ilitokana na yeye kukosa muda wa kulinda maisha yake binafsi.

Fahamu kwamba  Mungu amekuleta duniani kwa ajili ya kusudi lake. Kusudi lake ni wajibu ambao  unapaswa kuutekeleza ukiwa hapa duniani. Naam wajibu wako ambao unao katika ulimwengu wa mwili ndio unaoamua nafasi yako katika ulimwengu wa roho katika kulitumikia kusudi la Mungu.

Haijalishi Mungu amekupa nafasi gani katika ulimwengu wa mwili, yumkini ni Mchungaji, Mwalimu, Muimbaji, Mtawala, Mfanyabiashara, kiongozi wa kiroho nk, jambo la msingi na la muhimu kwako ni kuhakikisha unaitunza sana nafasi uliyopewa na Mungu kwa kulinda maisha yako binafsi. Kwa kutunza hatua zako katika Bwana, kuenenda kwa roho na kutokuifuatisha namna ya dunia hii yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima. Naam kulinda maisha yako kwa kuishi maisha ya utakatifu na yenye ushuhuda mbele za Mungu na wanadamu pia.

Naam ili uweze kuyatenda haya sharti ujifunze kutenga muda wa kuomba, kusoma na kulitafakari neno la Bwana kila siku. Ukijisahau ukabakia kutumikia, kuhubiria wengine bila wewe mwenyewe kuyafanyia tathmini maisha yako binafsi ya kiroho, uwe na uhakika hutachukua muda nawe utakuja kuwaambia wale watakaokuja kukushaangaa kwa sababu ya hali yako mbaya ya kiroho ukisema ‘ Msinishangae kwa kuwa hali yangu ya kiroho ni mbaya, kilichonifikisha hapa ni kukosa muda wa kuyalinda maisha yangu binafsi ya kiroho, naam sikuwa makini na maisha yangu, niombeeni tu wapendwa’.

Fahamu kwamba Shetani anapoandaa vita kwenye ulikwengu wa roho, anazingatia sana nafasi ambazo watu wamepewa. Hivyo anapigana ili kuipata nafasi yako kwa lengo la kufanya mambo/mapenzi yake kupitia kwenye nafasi yako.

Huu ni wito kwako wewe  Mtumishi wa Mungu katika nyanja yoyote ile, kwamba ni muhimu sana ukaitunza nafasi yako,  kwa kuwa makini na kulinda sana maisha yako binafsi ya kiroho. Kumbuka u halali wa Mungu kukutumia ni wewe kuwa mwaminifu na kuilinda nafasi uliyopewa. Naam thamani ya siku zako  ipo kwa wewe kuishi na kutumika ndani ya kusudi la Mungu.


Bwana awabariki.
Na: Patrick Sanga
0755-816800


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...