ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amezungumzia mambo kadhaa ya kitaifa akisema, ongezeko la posho kwa viongozi wa umma ni ubinafsi na kuonya kama Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 utafanyika bila ya kuwako kwa Katiba Mpya, utagubikwa na ghasia.Pengo alitoa angalizo hilo jijini Dares Salaam jana alipokuwa akitoa ujumbe kwa taifa kuhusu Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru, Sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo |
Kuhusu posho, Kadinali Pengo alisema viongozi wa Serikali na umma wakiwamo wabunge, wanapaswa kuacha ubinafsi na badala yake wafanye kazi kwa kuwafikiria zaidi wananchi kuliko maslahi binafsi.
“Sisi Wakristu tunaamini kuwa, Kristu licha ya kuwa alitumwa na Mungu Baba kuja kutukomboa wanadamu alifanyika mwili na kuzaliwa katika hali ya umaskini na ufukara ili atukomboe. Viongozi wa Serikali, dini na watumishi wa umma, inatupaswa kuiga mfano huo,”alisema Pengo.
Aliongeza, “Nasisitiza hili kwa viongozi sababu hivi karibuni kumezuka mzozo kati ya wabunge na wananchi ambao wamejiongeza posho kwa madai maisha kuwa magumu. Viongozi hatupaswi kufikiria marupurupu yetu na maslahi yetu kwanza kabla ya kuwafikiria wananchi tunaowaongoza.”
Hivi karibuni Spika wa Bunge alitangaza kwamba wabunge wameongezewa posho ya vikao kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku kutokana na ugumu wa maisha wakiwa Dodoma. Mbali na posho ya vikao, wabunge hupewa fedha ya kujikimu Sh80,000 na Sh50,000 ya usafiri kwa siku hivyo kuwafanya kupata Sh330,000 kwa siku.
Pengo aliwataka viongozi wa Serikali na umma kuiga mfano wa mwokozi wao, Yesu Kristu aliyesema kuwa, licha ya kuwa na nguvu za Kimungu, alipotumwa na Mungu Baba kwenda duniani kuwakomboa wanadamu, alijishusha na kuzaliwa katika mazingira ya kimasikini na ufukara ili aweze kufanikisha kazi hiyo.
Katiba na siasa .
Akizungumzia Katiba Mpya, Kardinali Pengo alisema ni chombo muhimu kinachotakiwa kufanya kazi kwa umakini na kuhakikisha inapatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.Pengo alionya kuwa bila Katiba Mpya, taifa linaweza kuingia matatizoni kwa kuwa katiba ndio inayoelekeza wananchi kuchagua viongozi.
“Tukicheza na Katiba, taifa litaingia matatani. Hivi sasa watu wameshailalamikia Katiba iliyopo kuwa ni mbovu na wakati huo huo Rais anachaguliwa kwa mpangilio ulio kwenye Katiba na anaapa kulinda Katiba na kuitetea,”alisema Pengo na kuongeza:
Spika wa Bunge la Tanzania mama Anna Makinda akiingia kuendesha Shughuli za Bunge |
“Tumeshasema Katiba iliyopo kwa sasa ni mbovu, tuchukulie suala hili “very serious (kwa uzito), tukamilishe kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vinginevyo tutaingia matatizoni”.Akizungumzia hali ya kisiasa, alisema hadi sasa Watanzania bado wanajifunza namna ya kuishi ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa baada ya kutoka ndani ya mfumo wa chama kimoja. Alisema jibu la kufikia kwenye siasa bora ni, kulifanyia kazi suala la Katiba, ambayo ndio itakayoamua wananchi wanataka kutawaliwa na watu wa namna gani.
“Kwa sasa bado tunaishi ndani ya mawazo na mtazamo wa chama kimoja cha siasa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ndio sababu, mawazo ya chama ndio yanayochukuliwa kama mwongozo wa Serikali. Lakini tukiweka mkazo katika Katiba, tunapaswa kutambua tunatengeneza katiba ya nchi na si ya chama kimoja,”alisema Kardinali Pengo.
Sherehe za miaka 50 ya uhuruKuhusu sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Kardinali Pengo alipongeza hatua tuliyofikia akisema ni nzuri na kutaka furaha hiyo iendelee kubaki miongoni mwa Watanzania.“Desemba 9 mwaka huu tulikuwa na Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Ujumbe wangu, tuendelee na furaha hiyo, lakini suali la kujiuliza sijui ni wangapi tulifurahia sherehe hiyo? Swali hili pia hata viongozi wanapaswa kujiuliza,”alisema.
Katika ujumbe wake huo, Pengo alisema Uhuru wa kweli hauji kwa kubahatisha bali kwa kufanyakazi. “Mwalimu Nyerere alisema Uhuru ni Kazi. Sisi tukasema Uhuru na Kazi. Lakini ujumbe unabaki kama ulivyo, nami leo ujumbe wangu kwa Watanzania ni kutambua bila kazi hakuna maendeleo,”alisema Kardinali Pengo.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment