Ukisoma katika warumi 8:14 Biblia inasema “kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” na pia Paulo kwa wagalatia anasema” Basi nasema Enendeni kwa Roho,wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili Wagalatia 5:16.
Hapa tunaona jinsi Paulo anavyosisitiza kwa makanisa ya Rumi na korinto kuhusu suala zima la kuongozwa na Roho Mtakatifu. Anawaambia warumi kwa kuwa wote wanaongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu maana yake haijalishi ana umri gani, ni wa dhehebu gani, jinsia gani maadamu anaongozwa na Roho wa Mungu huyo ni mwana wa Mungu na bado anawaagiza wagalatia akisema Basi nasema enendeni kwa Roho………….. anaposema enendeni maana yake mkiongozwa na Roho, au mkimfuata Roho katika yale anayowaagiza.
Maneno haya yanaonyesha zipo sababu za msingi kwa nini tunatakiwa kuongozwa na Roho sasa hapa sizungumzii kazi za Roho mtakatifu najua zipo kazi nyingi anazozifanya Roho Mtakatifu lakini mimi nazumgumzia sababu za kuongozwa na Roho Mtakatifu, ambaye ndio agano jipya la Mungu kwetu (Yeremia 31:31) katika hiyo Yeremia Neno linasema “Angalia siku zinakuja asema Bwana nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israel. Sasa ukiendelea kusoma mistari inayofuata utaona anazungumzia habari za kutia sheria yake katika mioyo ya watu.
Sasa hili ndilo agano jipya la Mungu pamoja na wanadamu. Sasa usipojua kwa nini unatakiwa kuongozwa na Roho na siyo akili zako, au mazoea, au taratibu za kwako n.k. hautajua umuhimu wa kuongozwa na Roho Mtakatifu na pili hautaona sababu za kuongoza na Roho Mtakatifu. Sasa lengo la ujumbe huu ni kukufundisha sababu za msingi za kwa nini unatakiwa kuongozwa na Roho Mtakatifu na siyo akili zako au mawazo yako. Sasa baada ya utangulizi huo mfupi na tuangalie sababu hizo za msingi.
Moja,
Ili tusizitimize tamaa za mwili wagalatia 5:16
“Basi nasema enendeni kwa Roho , wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.Tunatakiwa tuenende kwa Roho ili tusizitimize tamaa za mwili. Siku zote mwili na Roho ni maadui nia ya mwili ni mauti na nia ya Roho ni uzima na amani (Warumi 8:7). Maana yake siku zote mwili utakuongoza kufanya mambo ambayo mwisho wake ni mauti ya kiroho na hata kimwili pia.
Utakuongoza katika tamaa zake, sasa usipoongozwa na Roho huwezi kujizuia kutekeleza tamaa za mwili na kwa sababu hiyo wewe si mwana wa Mungu na mtu wa namna hii hataingia mbinguni kamwe. Katika 1Wakorinto 6:9-10 anasema “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanyanyike, waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala walevi, wala watamanio, wala walevi wala watukanaji, wala wanyang’anyi.Sasa utakapoongozwa na Roho Mtakatifu utaratibu wake utakuacha huru mbali na hayo mambo ya mwili au nia ya mwili na utakuongoza katika uzima na amani na kulitenda tunda la Roho ambalo ni upendo, furaha, amani, uvumilivu utu wema , fadhii, uaminifu, upole na kiasi “Wagalatia 5:22-23”.
Mbili,
Ili tupate kuyaelewa mafumbo ya Mungu na kuyafasiri mambo ya Rohoni kwa maneno ya Rohoni.
1Wakorinto 2:10 inasema “ Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho, maana Roho huchunguza yote hasa mafumbo ya Mungu” na ule mstari wa 13 unasema “ Nayo twayanena , si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya Rohoni kwa maneno ya Rohoni. Hapa najua walio wachungaji, walimu wa neno la Mungu au viongozi wa vikundi mbalimbali vya kiroho watanielewa zaidi.
sikiliza Roho Mtakatifu ndiye mwenye uwezo wa kuchunguza kilichopo kwenye ufahamu wa Mungu kuhusu wewe, ndoa yako, kanisa lako, biashara yako, masomo yako, nchi yako n.k. sasa akishachunguza ndiyo anakujulisha maana wewe ulikuwa hujui. Pia Roho Mtakatifu ndiye anayekusaidia kuyanena, kuyafundisha au kuyafafanua maneno ya Mungu kwa watu wake, anaposema kuyafasiri maana yake kuyafundisha mambo ya Rohoni kwa jinsi / namna ya Rohoni.
Hivyo kama wewe ni kiongozi au mwalimu wa neno la Mungu, ukiongozwa na Roho, yeye atakuongoza / atakusaidia kuwafundisha hao watu neno la Mungu kwa jinsi ya Rohoni yaani kwa mfumo wa Rohoni kulingana na watu ulio nao, maana yeye ndio mtunzi wa hilo Neno,soma mwenyewe 2Petro 2:21” maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu, bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
Na; Patrick Sanga.
No comments:
Post a Comment