Tuesday, April 5, 2011

KANISA LA TANZANIA LINAJIFUNZA NINI KWA YANAYOTOKEA LOLIONDO?

Ndani ya kanisa la Tanzania ni mengi yamesemwa juu ya tiba ya Babu wa loliodo, kimsingi kuna makundi makubwa matatu. Kundi la  kwanza linakiri wazi kua babu hatokani na Mungu na hili linavyo vigezo vyake, kundi la pili ni lile linaloamini kua Babu ni Mtumishi wa Mungu, na Mungu ndio muasisi wa dawa hiyo hivyo dawa hiyo ni ya kiMungu. Kundi la tatu na la mwisho hili sio kubwa sana kama hayo hapo juu, bali hili  limetawaliwa na ukimya, ni watumishi wa Mungu ambao hawako upande wowote kati ya hizo pande mbili kifupi hawakubali au kukataa uungu au upepo wa tiba ya babu, bali kundi hili husema tumpe muda kila kitu kitakua wazi.

Pamoja na hayo yote ya kukubali au kukataa kanisa kama kanisa tunajifunza nini na mchakato mzima wa Loliondo? Ikiwa maelfu ya watanzania kila kukicha wanaenda kwa Babu, pia wapo raia wa kigeni kutwa wanaenda kwa babu, wengine wameanza kuja toka bara la Asia wote kwa Babu. Msululu wa viongozi wa Serikali na familia zao wote kwa babu. Babu kafunika mjadala wa katiba, Babu kafunika presha za maandamano ya Chadema, Babu kawasahaulisha watanzania machungu wanayopitanayo sasa ya kukosa umeme, Babu kafunika habari za machungu ya mabomu ya Mbagala kwa sasa utafikiri mbagala hakukutokea kitu.Yaani mtaani babu,kwenye media Babu Madhabahuni watumishi babu, watoto mpaka wazee babu kila kukicha babu, babu, babu.


Kuna kasi ambayo kanisa la Tanzania tunayo kwa sasa, ila changamoto iliopo ni Kukimbia  kulingana na kasi ambayo Mungu anatuhitaji kukimbia katika hiyo ili kuliokoa Taifa.

Shida ndio motive kubwa ya maelfu watu kwenda kwa babu, Kama kanisa foleni za kwa babu na sio kuwatafuta watumishi wa Mungu zinatukumbusha kwa vitendo kuwa jamii nzima ina matatizo mbalimbali na yanalihitaji kanisa kuyatatua. Ikiwa kanisa leo likijipanga vizuri na MUNGU na kutatua matatizo ya wanadamu Jina la kristo haliwezi tukanwa kama ilivyo sasa kwani ndilo litoalo msaada kwa watu na shida zao. Ikiwa serikali imeweza kupeleka Bilioni moja Loliondo ina maana imetii kile kitokeacho Loliondo. Hii ina maana endapo kanisa lingeweza kutatua matatizo ya watu lingekua na kauli dhidi ya maamuzi mbalimbali ya Taifa kama ilivyokua kwa wafalme wa Israeli hawakwenda vitani mpaka wakaulize kwa watumishi wa MUNGU ndipo wakwee katika vita.

Babu hayuko mji yuko kijijini lakini bado watu wanakwenda, Biblia inasema Yohana aliamua kukaa porini akijifunga ngozi kiunoni lakini watu walitoka mjini na kumfuata porini, jiulize walifata nini, Jibu liko wazi ni nguvu ya MUNGU zilizokua juu ya Yohana. Hivyo ikiwa leo watu wote tunaosema tumeokoka (kanisa) tukizitafuta nguvu za Mungu kwa bidii Tunaweza kuwa chumvi halisi kwa Taifa letu katika kumrudia Mungu. Hii ni kwa kua suluhisho la matatizo litakua ni Mungu wa walokole kwa kua walokole wamepruv Mungu wao hashindwi jambo.

Kanisa pasipo udhihirisho wa Nguvu za Mungu hiyo nayo ni dini nyingine, uwepo wa kanisa pasipo utatuzi wa matatizo yanayozunguka jamii ya kanisa hilo huu ni ufa unaoliondolea Nguvu kanisa dhidi ya maamuzi mbalimbali ya viongozi wanaoongoza jamii hiyo. Kimsingi hapo ndipo kanisa la Tanzania lilipo, kanisa limefanikiwa kuwa na shule, hospitali na mambo mengine lakini vipi kuhusu magonjwa yaliyoshindikana je ni kweli MUNGU wetu ameshindwa kuyatatua au tuliookoka tumeshindwa kukaa vizuri na Mungu ili afumbue mafumbo yaliyopo?. Mimi nafikiri imetosha kuishia kuimba mapambio, kwenda kwenye matamasha ya injili, kubadilisha mabenchi makanisani na kuweka sofa badala yake tujikite katika kumtafuta MUNGU ili Mungu akutane na matatizo ya watanzania. 

Kwa kua yanayotokea Loriondo ni ushahidi tosha kua jamii inamatatizo na kanisa kama mfumbuzi wa matatizo kwa kiasi kikubwa limelala. Siwaongelei hao waliojitokeza wengine wenye kutibu kama babu, kwa kua jamii inamuamini babu kuliko wao na wanaonekana kwenye macho ya watanzania wengi kama wanaiga ujio wa babu. Ok labda niseme hivi yumkini tiba ya Loliondo ni sahihi vipi kuhusu watanzania waishio Mtwara je ni wote wenye ubavu wa kufika kwa Babu na kupata kikombe?. Au wale waishio kigoma wote wanajeuri yakufika Loliondo?, Tukifika hapo utaona  mahali pekee penye kutatua matatizo ya watu ni kanisani, endapo watumishi wa Mungu nchi nzima wakijipanga sawasawa haina haja ya loliondo kila mtu atahudumiwa na kanisa la mahali pake huku Jina la kristo likiinuliwa kwa viwango vya juu.

     Ikiwa leo Viongozi wakubwa serikalini wanaweza weka shughuli  na dini zao kando na kwenda kwa babu, kanisa likijipanga wanaweza acha mambo yao kando na kumtafuta Kristo kwa gharama yeyote.


Imetosha kulumbana na kuinua vita kila kukicha baina yetu kua fulani kakosea pale au hapa, yule ni mchawi hana lolote kila siku Nigeria kuongeza nguvu, ooh hawa nao! wako modern sana ni Mashalobalo wakilokole, Yule nae ni nabii wa uongo hivi vyote kama kanisa vinatuchelewesha na kutuondolea focus yetu mbele za Mungu. Kifupi tupige kazi, sikatai changamoto zipo na sio Tanzania hata kwa watumishi wakubwa Duniani hizi zipo lakini wenzetu hawaziatamii kama tufanyavyo sisi. Tukirudi kwenye Biblia wakati Mtume Paul anamweleza Petro madhaifu yake biblia haisemi walibaki katika eneo hilo mpaka mwisho, walirudi kazini wakiwa wamewekana sawa na kazi ikasonga na sio kuifanya ndio Topic kila madhabahu inapopatikana kama itokeavyo leo. Matokeo yake watanzania wanabaki na wakihaha na matatizo yao hawana pa kuya peleka  kwa kua kanisa limepoteza focus, halifumbui matatizo bali linaishi katika matatizo na kunyoosheana vidole.

Wakati viongozi mbalimbali wanakwenda kila kukicha kwa babu ni viongozi wangapi wanaokuja kanisani kutafuta msaada?, ok tuwaondoe viongozi wakikristo, ulishasikia ni kiongozi gani wa dini ya mama mdogo(muslims) aliyemkwenda mwenyewe kwenye kanisa la kikristo pasipo kualikwa na kuomba aombewe aondokane na matatizo yake? na kama wapo ni wangapi? Au Yesu wetu ni kwa ajili ya wakristo pekee?. Leo utaona msululu wa waislamu na dini nyingine kwenda kwa babu ni mkubwa kuliko msululu wa waislamu kwenda kanisani kutafuta msaada, moja inamaana Mungu anakaa kwa babu pekee na kwa wakristo wengine hayuko? mbili ina maana babu anaupako wa kuondoa matatizo ya watu wa dini na rangi mbalimbali kuliko watumishi wengine?.

Kanisa linahitaji kujifunza mengi kwa hayo yatokeayo loliondo. Ikiwa mbunge anaamini tiba ya Loliondo kiasi cha kupeleka wapigakura wake, ina maana kanisa likikaa mahali pake na kudhihirisha Kristo kwa vitendo wabunge wanaweza kuwapeleka maelfu ya wapiga kura wao kanisani pia,ikifikia hatua hiyo hata idadi ya wabunge wanaokwenda Bagamoyo kutafuta ubunge itaondoka na kanisa litakua ndio kimbilio la kila mtanzania.

Kwa mtazamo huo badala ya kanisa  kuanza kujiuliza kwa habari ya Tiba ya Babu kama ni yakimungu ama la!!!, kwanza tujiulize ufanisi wa nguvu za kristo tunazotembea nazo leo kama kanisa ,je ni ule ufanisi ambao Mungu ameuachilia kwa kanisa litembee nao? Swali hili litatupa picha nini tufanye kama kanisa na itatupa kubalilisha kauli badala ya kanisa kuimba wimbo unaoimbwa na watanzania wote  watoto kwa wakubwa wa loliondo loliondo loliondo kuanzia asubuhi mpaka jioni loliondo. 

Inatupasa kanisa kurudi kwa MUNGU kwa upya kutafuta nguvu na rehema za Mungu juu ya watanzania na matatizo yao kulingana na Biblia isemavyo katikakitabu cha 2Nyakati 7:14  ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu wakijinyenyekesha na kutii na kuacha njia zao mbaya mimi nitasikia kilio chao na kuiponya nchi yao. Tumaini la watanzania halipaswi kua loliondo kama ilivyo sasa bali tumaini la watanzania liko katika kristo Yesu

Kwa yanayotokea loliondo siku za hivi karibuni, kanisa lazima likubali kutoka kwenye lope la usingizi lililo nao, kwa kua kila aliyeokoka leo anaonekana yuko bize mno na changamoto za maisha hususani eneo la uchumi kunzia kwa washirika mpaka wachungaji, sio dhambi lakini yatupasa tubadili hii dhana kutoka katika hali ya kujiangalia wenyewe(self centered) na kwenda kuangalia na wengine. Leo hii kanisa linasaka kuendesha jeep, Nyumba nzuri, maombi ya kila kukicha kutafuta wenzi wa maisha na post za juu maofisini. Kifupi materiority  ndio first priority Kitu ambacho sio sahihi kwa kua wokovu ni zaidi ya Jeep ni zaidi ya nyumba ni zaidi ya hayo yote Kikubwa tutafute kwanza maarifa ya kimungu yatayopelekea sio tu kuyaondoa matatizo yetu bali na matatizo ya watanzania wenzetu. Kwa kua suluhisho la matatizo ya watu kibiblia liko kwa watu wa Mungu. Pale ambapo jamii imekosa majibu ya matatizo yao ndipo Mungu wetu huingia kazini kama ilivyokua kwa Eliya, Daniel, Mikaya, Esta, na wengineo wengi.

 Watanzania wanakiu na Mungu ila uwezo wa Kanisa katika kumfunua  Mungu bado ni mdogo

Kanisa linaposhindwa kuonyesha msaada watu hutafuta msaada pasipo kujali umetoka wapi na  kwa nani na matokeo yake kesho yatakuaje. Leo asilimia sabini (70%) ya watumishi wa Mungu wanakiri wazi na wengine kwa mlango wa pili kua Tiba ya Babu si ya Kimungu achana na wale wanaojipa majibu wenyewe kimoyomoyo pasipo kumwambia mtu. Sina ugomvi na hili lakini mbona watu wametoka makanisani wakaenda kwa babu alafu tukiulizwa tunaanza oooh eehh ahhh kifupi injilisiasa? Kama babu ni pepo lakini ameponya magonjwa sugu na madaktari wamethibitisha uponyaji huo basi turudi kwako mtumishi pamoja nakumpinga Babu mbona hujawahi kuponya gonjwa lolote sugu ilihali kristo yuko ndani yako?. Inamaana mapepo yananguvu kuliko kristo?! La hasha!! 

Endapo kanisa litafanikiwa kuondokana na ku-relax kuliopo na kutafuta nguvu za Mungu na kuzikuta, watu wa kila aina watafurika kwenye makanisa, kwa kua ndiko ufumbuzi uliko!!!, hata kama kanisa liko kijijini kiasi gani watu watafika tu. Ikiwa watu walitoka mijini kwenda kumfuata Yohana porini naamini watu watafika popote ambapo kanisa la Mungu limekuwa msaada katika kutatua matatizo yaliyopo katika jamii husika yawe ya kiroho au kimwili.

Mambo ambayo jamii inayasubiri toka kwa kanisa ni makubwa kuliko yale ambayo kanisa inayatoa kwa jamii

Usingizi tuliolala kama kanisa umetosha turudi kwa Mungu kwa namna nyingine tukiwa na akili tofauti kwa ajili ya kutatua matatizo ya watanzania. Lazima tukubali nguvu ya uponyaji iliyo katika Kristo Yesu hatujaweza  kui-Utilize chini ya jua hata kwa asilimia tano(5%). Tumeshindwa kukonect kati ya nguvu za Mungu alizoziachilia kwa ajili ya uponyaji wa kila namna na magonjwa yenyewe. Matokeo yake wagonjwa wanaokuja kanisani leo hata wao hawana uhakika kama watapona, ni kama wanajaribu bahati kitu ambacho si sahihi katika Mungu. 

Sisemi tulifanya dhambi hapana bali kwa yanayotokea Loliondo kanisa lishtuke na kurudi kwenye mstari. Tusiishie kama kanisa kuutafuta uungu ulio ndani ya tiba ya babu au upepo(ugiza) ulio ndani ya tiba hiyo, bali tuvuke duara hilo na kuangalia nini tunajifunza katika Mungu kwa habari ya Loliondo



 V.Mboya

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...