I yohana 2:14
Kila kundi katika kanisa, jamii na hata nchi Mungu amelipa nafasi na wajibu wake maalumu wa kutekeleza. Pia Mungu anao mtazamo wake binafsi na matarajio yake kwa hayo makundi
mbali mbali ndani ya nchi. Vijana, watoto, wababa, wazee, wanawake, viongozi wote / yote yana mtazamo wake mbele za Mungu.
Ukimuuliza Mungu nini mtazamo wako kwa vijana, atakujibu soma vizuri IYohana 2:14 maana yake Mungu anawatazama vijana kama watu wenye nguvu, watu ambao neno la Mungu linakaa ndani yao na pia wamemshinda mwovu.
Sasa ukirudi mazingira halisi unaona kwa asilimia kubwa vijana wengi hawako kwenye nafasi ambazo Mungu aliwakusudia. Lengo la somo hili ni :-- Kueleza sababu za kwa nini vijana wengi hawajakaa katika nafasi zao.- Kumweleza kijana mambo ya kujiepusha nayo ili aweze kukaa kwenye nafasi yake.- Kumpa kijana maarifa yatakayomsaidia kurejea kwenye nafasi yake na ili aweze kutekeleza matarajio ya Mungu kwake.
Zaidi ujumbe huu umekusudia kulenga na kuelewesha vijana waliokoka, nazungumza na vijana waliookoka maana hawa ndio ambao Mungu amewatamkia maneno haya au kuwa namtazamo huu juu yao. Zipo sababu nyingi lakini hizi zifuatazo ni za msingi na zimesababisha wengi kuishi maisha nje ya kusudi la Mungu na kufa bila kutekeleza matarajio ya Mungu kwao sababu hizo ni:-
- Moja vijana wengi hawajajazwa nguvu za Roho Mtakatifu.
Biblia inasema katika matendo ya Mitume 1:8 kwamba “lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika uyahudi wote, na samaria, na hata mwisho wa nchi”. Hivyo vijana wengi hawajakaa katika nafasi zao kwasababu wengi wa vijana leo makanisani hawajajazwa nguvu za Roho Mtakatifu si kwamba Mungu hataki kuwajaza lakini shida ipo kwa vijana wenyewe wengine kutotaka kujazwa nguvu hizo, lakini wengine hawajui nini wafanye wajazwe nguvu za Roho Mtakatifu na wengine wanajua lakini hawana kiu ya kujazwa nguvu hizo.
Pili vijana wengi hawajui namna ya kuenenda kwa Roho .
Paulo kwa warumi anasema” kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” Warumi 8:14 na pia kwa wagatia anasema” Basi nasema enendeni kwa Roho hamtatimiza kamwe tamaa za mwili “Gal 5:16. Kuna wengi waliojazwa lakini si wote wanaoenenda au wanaoishi wa Roho. Vijana wengi Mungu amewapa vitu vizuri sana ndani yao lakini kwa sababu ya kukosa utiifu na kutoenenda kwa Roho wameshindwa kusimama kwenye nafasi zao.
Tatu vijana wengi wameshindwa kushirikiana na upako wa Mungu uliodhihirishwa kwao.
Hili ni tatizo kubwa kwa kweli, Mara nyingi Mungu amekuwa akiwapa upako, nguvu au uweza wa kufanya mambo mbalimbali vijana. Sasa si vijana wote wanaojua namna ya kushirikiana na huo upako ambao Mungu aliwapa kwa jambo fulani Mfano, Mungu anaweza akampa kijana upako wa kuomba lakini kijana huyo badala ya kuomba yeye anaangalia mpira, au ni mwanafunzi anatakiwa kusoma na Mungu ameleta upako huo sasa yeye anaenda kuomba mambo huwa hayakai hivyo. Upako lazima utumike kwa kusudi lile uliotumiwa. Upako wowote unaokuja kwako unakuja kwa kusudi maalumu.
Nne Kukosa maarifa ya Mungu.
Mungu anasema katika Hosea 4:6 kila kipengele cha kwanza watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa na pia katika Zaburi 119:9 anasema “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii akilifuata neno lake”. Sasa kwa sababu nazungumza na vijana naweza nikaweka mistari huu hivi “Vijana wangu wanaagamizwa kwa kukosa maarifa. Maarifa yanayozungumzia hapa ni mafundisho ya neno la Mungu.
Vijana wengi wako tayari kuangalia mechi mbili mfululizo kuanzia saa nne kasoro usiku hadi saa nane kwa masaa ya Kitanzania, lakini hawako tayari kusoma Biblia kwa saa moja, wako tayari kuangalia “Movie” za kinigeria, au za kizungu hata masaa matatu (3) lakini si kuangalia na kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu. Na Biblia inasema Apendaye mafundisho hupenda maarifa. Sasa kwa vile vijana wengi hawapendi mafundisho ndiyo maana hawako kwenye kusudi la Mungu.
Tano, vijana wengi bado wanaipenda dunia,
Mzee Yohana katika 1Yohana 2:15” Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia, mtu akiipena dunia kumpenda Baba hakupo ndani yake”. Na pia Daudi anasema katika Zaburi 1:1 Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki wala kusimama katika njia ya wakosaji wala hakuketi barazani pa wenye mzaha.
Ni vijana wachache sana katika kanisa la leo ambao wako tayari kujikana nafsi zao kwa ajili ya Mungu wengi wanapenda kupoteza muda kwa habari zisizo za Msingi, wengi wanapenda mzaha na utani, ni vijana wachache ambao wanaweza kuacha kuangalia mchezo kwenye TV, au akakataa kwenda kutembea ufukweni kwa lengo la kuomba, au kusoma Neno, ninachojaribu kusema hapa ni hiki, najua kila jambo lina wakati wake, lakini ni vijana wachache sana waliojizuia katika mambo ya mwili kwa ajili ya kufanya yaliyo mapenzi ya Mungu.
Sita, Vijana wengi hawajazivaa silaha za vita.
Waefeso 6:11 Vaeni Silaha zote za Mungu, mpate kuzipinga hila za shetani.Viajana wengi wameshindwa kumshinda mwovu kwa sababu hawazajivaa silaha za vita. Wengine hawajui silaha za vita ni zipi? Lakini wengine wanajua lakini hawajazivaa. Ile sura ya sita ya waefeso 6:10-18 Paulo anazungumzia silaha za vita, ambazo ni kwlei, haki, amani, Imani, wokovu na Neno la Mungu. Sasa hizi ni silaha na kama ni silaha zina namna zinavyovaliwa na namna zinavyotumika. Sasa si vijana wote waliozivaa silaha, wengi hawasomi neno la Mungu, hawatendi haki, wengi wana imani ya maneno isiyo ya Matendo.
Saba, Vijana wengi wanaishi bila kuwa na malengo katika maisha yao / maono.
Mithali 29:18. Inasema “Pasipo maono watu huacha kujizuia bali ana heri mtu yule aishikaye sheria”. Hivi leo ukiwauliza vijana wengi kwamba una maono au hasa malengo gani katika maisha yako? Asilimia kubwa watakujibu sina malengo yeyote yale.Wakati huo huo hakuna aliyeumbwa kwa bahati mbaya Yeremia 29 :12.
Kwa kila mtu Mungu analokusudi maalum la kumuumba na pia anayo malengo na mikakati ya kumpa huyu mtu atekeleze katika maisha yake. Sasa kwa sababu vijana wengi hawana na hawajajua hayo malengo ndio maana wanafanya kila kinachotokea mbele yao bila kujua kama ni kusudi la Mungu.
Naamini baada ya kuwa umesoma ujumbe huu umepata maarifa ya kukusaidia kukaa katika nafasi yako kama kijana kwa sababu umeshajua sababu za kuktokukaa kwenye nafasi yako.
Na : Patrick Sanga.
No comments:
Post a Comment