Marko
9:14-29.
Hii ni habari
ya yule baba aliyekuwa na mwana mwenye pepo bubu na kiziwi, akamleta kwa
wanafunzi wasiweze kumtoa. Wakati huo Yesu alikuwa mlimani akiomba na wanafunzi
wengine watatu, aliposhuka baba mwenye mtoto akamwambia, Mwalimu nimemleta
mwanangu kwako , ana pepo bubu, na kila ampagaapo humbwaga chini , naye hutoka
povu na kusaga meno na kukonda , nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo
wasiweze, akawajibu akasema enyi
kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi
hata lini? Mleteni kwangu akamponya.
Ukisoma ule
mstari wa 28 Biblia inasema “ Hata alipongia nyumbani, wanafunzi wake
wakamwuliza, mbona sisi hatukuweza kumtoa? Akawaambia namna hii haiwezi kutoka
kwa neno lolote , isipokuwa kwa kuomba.
Mpenzi
msomaji ni vema nikushirikishe mojawapo
ya siri nyingi za ajabu katika fungu hili la maneno, nayo ni ‘Maombi peke yake bila imani
hayatoshi kutengeneza jibu la mahitaji yako’.
Katika habari
hii, huyu baba alimleta mwanawe kwa Yesu ili amponye, sasa kwa bahati nzuri
hakumkuta Yesu bali wanafunzi tisa na watu wengine. Nasema kwa
bahati nzuri kwa sababu Yesu angekuwepo huenda tusingejifunza kutokana na
makosa ya wanafunzi wale tisa.
Wale
wanafunzi walijaribu kumuombea yule kijana mgonjwa lakini wakashindwa kumtoa
yule pepo. Yesu alipowasili na kupewa taarifa hizo aliumia sana akawauliza enyi
kizazi kisicho amini nikae nanyi hata lini, kwa lugha rahisi alikuwa akiwaambia
kukosa kwenu imani kumesababisha mshindwe kutoa huyu pepo na si kitu kingine.
Sasa swali
walilomuuliza Yesu kwenye mstari wa 28 linaonyesha wanafunzi hawakuelewa kwa
nini wao walishindwa kumtoa pepo? Ndipo Yesu akawajibu namna hii haiwezi kutoka
kwa neno lolote, isipokuwa kwa kuomba.
Ukiliangalia
jibu la Yesu si rahisi sana kumuelewa. Unaweza kufikiri aliwachanganya zaidi
wanfunzii kwa jibu lake. Kwa sababu aliposema namna hii haitoki isipokuwa kwa
kuomba alimaanisha nini? Je ina maana wanafunzi walikuwa hawaoombi? Kwa
vyovyote vile walikuwa wanaomba, Je nini kilipungua kwenye maombi yao? Mstari
wa 19 unatoa jibu pale aliposema enyi
kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Na hapa ndipo
tunapojua kumbe maombi peke yake bila imani hayatoshi kutengeneza jibu la
mahitaji yatu.
Imani ni
nini? Waebrania 11:1 inajibu “ Imani
ni kuwa na uhakika wa mambo yatarijiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”.
Ule mstai wa sita pia unasema “Lakini
pasipo imani haiwezekani kumpendeza , kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima
aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao”.
Kitu gani
tunajifunza hapa? wakati wanafunzi wanaomba ndani yao walikosa uhakika wa mambo yatarijiwayo,
kwa lugha rahisi maombi yo yalikosa au kupungukiwa imani, yaani ndani yao
uhakika wa yule pepo kutoka haukuwepo wakati wanaomba.
Neno linasema
kila amwendeaye/aombaye lazima aamini kwamba yeye yupo.
Hivyo
wanafunzi walitakiwa kuomba + imani = jibu la hitaji la yule baba.
Au walitakiwa
kuomba/kukemea/kutaja hitaji lao + uhakika kwamba yule pepo atatoka = Pepo
kutoka na kijana kufunguliwa.
Mpenzi
msomaji nimalize kwa kusema hata wewe najua unakutana na changamoto nyingi sana
ambzo unazipeleka mbele za Mungu kila siku kwa maombi sasa jifunze katika mwezi
huu kuwa maombi pekee bila imani hayatengenezi jibu lako. Hivyo kwa kila unalo
omba hakikisha umejumlisha na imani ndani yake nawe utaona jibu lako.
Na
Patrick Sanga
No comments:
Post a Comment