Monday, September 5, 2011

Kufanikiwa Kwa Kusudi La Mungu Kunategemea Namna Unavyotumia Fursa Ulizopewa (Part 2)

 
Hebu niendelee kwa ndoto hii ambayo ndio chanzo cha ujumbe huu unaousoma…
 Siku moja nikiwa Dodoma, naliota ndoto nipo kwenye makutano ya barabara ya Buguruni, nami nilikuwa usawa wa juu wa yale makutano, kwa hiyo nikawa naona vizuri mgari ya pande zote nne.

Baada ya muda nikamwona dada mmoja anaendesha gari akitokea Tazara na lengo lake ni kwenda Buguruni. Sasa taa ndio zilikuwa zinaongoza magari. Taa zilipomruhusu yule dada kupita yeye hakupita, ni kama alikuwa anaongea na mtu kwa nje. Baadae taa ya kumzuia iliwaka na magari ya upande mwingine yakaruhusiwa kupita.Yule dada akaamua kupita wakati siyo zamu/muda wake kupita. Alipoondoka akasababisha ajali ambayo ilizuia magari ya pande karibu zote nne za yale makutano.

Watu walikaa kwenye ile foleni kwa wastani wa masaa kama matatu, kisha nikasikia sauti kwenye ufahamu wangu ikiniuliza unajua huyu dada amekwamisha makusudi/watu wangapi kuwahi maeneo waliyotakiwa kwenda?. Niliposhutuka na kuanza kutafakari ndipo nilipopata ujumbe huu kwamba ‘kufanikiawa kwa kusudi la Mungu kunategemea namna unavyotumia vizuri fursa unazopewa’.


Tunajifunza nini katika ndoto hii? Zile taa ni mfano wa fursa ambazo Mungu anampa mtu ili kufanikisha kusudi lake kupitia mtu huyo. Taa nyekundu ni mfano wa changamoto/jaribu/kikwazo maana inakunyima fursa ya kupita. Taa ya njano ni ya taarifa kwamba lipo tumaini la kutoka kwenye hicho kikwazo/kizuizi yaani taa nyekundu. 

Na taa ya kijani ndiyo amani ambayo ndani yake inakupa fursa/nafasi ya wewe kupita. Yule dada alishindwa kutumia fursa aliyopewa, akataka atoke kwa akili zake na mazoea wakati taa nyekundu inayomzuia kupita inawaka.
Kwa uzembe wake alisababisha ajali, akazuia watu wengi sana waliotakiwa kuwahi kwenda kufanikisha makusudi mbalimbali waliyokuwa nayo. Kwenye ile foleni kulikuwa kuna makundi mengi ya watu, wanafunzi, wafanyakazi, wafanyabishara, magari ya wagonjwa, nk.

Hawa watu makusudi yao yalifungwa kwenye muda na kwa matumizi mabaya ya fursa yaliyosababishwa na huyu dada kuna wagonjwa walifia pale kwenye foleni, kuna watu walichelewa kupanda ndege/treni, kuna watu walichlewa kufanya mitihani nk.

Hata kiroho ndivyo hali ilivyo kwa makosa ya viongozi wetu, washirika wetu, mtu binafsi kushindwa kutumia vizuri fursa tulizopewa, tumeathiri kusudi la Mungu juuyetu na kwa wengine . Kwa kosa hili tumepelekea pia mdhara mengi  kutokea kwetu wenyewe na kwa watu wengine ambao wameunganishwa na sisi katika mafanikio ya maisha yao.

Kanisa sikia amani ya nyumba yako, kazi yako, taifa lako nk vinategemea namna unavyozitumia fursa zilizoko nyuma ya hiyo amani. Fahamu kwamba amani ya kila kitu kwenye maisha yako itategemea namna unavyotumia fursa zilizoshikilia amani kwenye hilo eneo. Na hii ina maana amani ya kila kitu inaletwa/inategemea kitu kingine. Sasa hicho kinachoshikilia au kuleta hiyo amani kinaitwa fursa(opportunity).

Ni mpaka uitumie vizuri hiyo fursa ndipo utaona amani/mafanikio kwenye maisha yako, vinginevyo usitegemee amani. Amani ni fuko la fursa (Peace is a package of opportunities) ndani ya amani kuna fursa nyingi ambazo unapaswa kuzitumia. Fursa zinaweza kuwa pamoja na taaluma, madaraka,muda,marafiki,uhuru,utawala,uchumi,biashara, kazi yako, ndoa yako nk. Jaribu kufikiri siku ukifa unakutana na Yesu anakuuliza nilikupa fursa nyingi duniani uzitumie kwa utukufu wangu, je ulizitumia sawsawa na kusudi langu kwako? Je, ungemjibuje ?  Wewe unazitumiaje fursa ambazo Mungu amekupa ndani ya amani.


Je, unathamini kwa kiwango gani kazi ya Yesu pale msalabani hasa kwa upendo wake kwako, kwa muda ulionao na mafanikio uliyonayo?. Tambua kwamba amani uliyonayo ni kazi ya kifo chake pale msalabani. Na hiyo amani ni fursa anayokupa Mungu uitumie kukamilisha kusudi lake hapa chini ya jua.

Mpenzi msomaji Mungu hakukuumba kwa lengo la kuijaza dunia tu. Umekuja duniani kwa kusudi lake maalum. Hivyo ili kuhakikisha kusudi lake linafanikiwa Mungu hutengeneza mazingira ya kuhakikisha kusudi lake kupitia wewe linafanikiwa. Mkakati mmoja wa hayo mazingira ni kukuletea fursa za wewe kuokoka, kusoma, uandishi, kuoa/kuolewa, madaraka, uongozi, fedha, muda, vipawa au vipaji mbalimbali nk. Si watu wengi leo wanaojua namna ya kutumia fursa hizo zilizoko ndani ya amani kwa faida ya ufalme wa Mungu.

Usije ukadhani utajiri, elimu, au madaraka uliyonayo ni kutokana na nguvu zako au wazazi wako au kwa kuwa mna asili ya utajiri. Je, umeshawahi kujiuliza kwa nini wewe uwe hivyo na si mwingine awe kama wewe. Siri ni hii, ipo sababu ya Mungu kukupa vyote ulivyo navyo sasa, kama fursa/nafasi ya kukamilisha kusudi lake hapa duniani kupitia wewe. Unapaswa kuishi na kuyakabidhi maisha yako kwa Bwana kwa mfumo ambao atakuwa tayari kukutumia wewe kupitia fursa alizokupa kwa wakati atakao yeye na si wewe ili kufanikisha kusudi lake.

Huwezi kufikia kiwango cha juu cha mafanikio yako kiroho na kimwili kama hautajua au kuwa na nidhamu ya kutumia vema fursa zote ambazo Mungu anakupa maishani mwako. Kumbuka kwamba fursa ni nafasi inayojitokeza kama mlango/njia ya wewe au wengine kupita kutoka kwenye eneo ambalo ulikuwa umekwama na pia ni nafasi inayokuja kukuonyesha mlango wa kupita siku utakapokuwa kwenye eneo ambalo huna msaada.   

Hebu tuutazame mfano huu wa nabii Ezekiel;
Katika Ezekiel 33:1-9  Biblia inasema “Neno la Bwana likanijia kusema, Mwanadamu sema na watu wa watu wako, uwaambie hapo nitakapoleta upanga juu ya nchi, watu wan chi hiyo wakimtwaa mtu mmoja na kumweka awe mlinzi wao…” Tafadhali pata muda usome mistari yote tisa mimi nimenukuu miwili ya mwanzo.

Katika habari hii Biblia inazungumzia habari za mlinzi ambaye jukumu lake ni kutoa taarifa kwa wale anaowalinda wasipatwe na mabaya.Biblia inasema kama mtu atakufa wakati mlinzi alishatoa taarifa ya hatari basi damu ya huyo mtu itakuwa juu yake, lakini kama atakufa kwa sababu mlinzi hakutoa taarifa basi damu ya huyo mtu itakuwa juu yake huyo mlinzi.

Katika mfano tunagundua kwamba kumbe kuwa “mlinzi” ni fursa.  Mlinzi anatoa nafasi ya mtu kujiaandaa kwa jambo linaloweza kuja mbele yake. Uzima na mauti wa wale anaowalinda ulikuwa kinywani mwake na pia kwa yeye kuwa macho kulinda, maana kama angelala asingeona hatari na kuwapashwa walengwa habari.


Sasa kumbuka kila mtu aliyeokoka ni mlinzi wa mtu/watu/eneo ulilopo na nchi yako kwa jinsi ya rohoni. Nikuulize swali? Je ni kweli uko macho kufanya hiyo kazi ya ulinzi kwa hao watu na maeneo uliyopo? Na je hata ulipoona hatari umetoa taarifa kama mlinzi ili watu/taifa lisije angamia?

 Sasa kuwa mlinzi ni eneo mojawapo la fursa, lakini fursa ni nyingi sana kama nilivyoainisha awali. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unaitumia vizuri kila fursa ambayo Bwana Mungu yu akupa ili usiathiri kusudi lake kwako na kwa wengine ambao wapo ‘connected‘ kwako kiroho na kimwili. Kufanikiwa kwa kusudi la Mungu kunategemea utiifu wako kwa Mungu na zaidi namna unavyozitumia fursa ambazo Mungu anazileta maishani mwako.

 Sehemu kubwa ya maisha ya uonevu ambayo watu wa Mungu wanayapitia leo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na wewe kutokuzitumia vizuri fursa ambazo Mungu amekupa maishani mwako. Watu/ndoa/familia ngapi leo zimeingia kwenye shida na wewe umejisahau na kufanya mambo yako tu na kuona kwamba hauwajibiki wala kuhusika na hao watu.

Badilika, imetosha hasara uliyoileta kwenye ufalme wa Mungu kwa kutotumia vizuri fursa alizokupa Mungu.Tangu sasa hakikisha kila fursa inayokuja unaitumia kwa utukufu wa Mungu. Kumbuka pia kwamba kila fursa inayokuja ni jibu kwa changamoto iliyopo au inayotaka kuja kwako au kwa wale waliounganishwa kwako.
  
Kumbuka mambo haya matatu kwamba;
Kufanikiwa kwa kusudi la Mungu kunategemea namna unavyotumia fursa anazoleta Mungu maishani mwako.
Kufanikiwa kwa maisha yako binafsi kunategemea namna unavyotumia fursa anazoleta Mungu maishani mwako.

Kufanikiwa kwa maisha ya watu wengine kupitia wewe kunategemea namna wewe unavyotumia fursa ambazo Mungu analeta maishani mwako. Hii ni kwa sababu Mungu ametuumba kwa namna ambayo mtu hawezi kuishi peke yake bali anahitaji kutegemea mtu mwingine. Na hasa inapokuja kiroho maana sisi tu viungo katika mwili wa Kristo.

Ni jukumu na uamuzi wako sasa kutumia vizuri yaani kwa utukufu wa Mungu kila fursa ianayopita miashani mwako, angalia usifanye makosa kama ya yule mama kwenye ndoto.
 Bwana akubariki na kukulinda.

Na: Patrick Sanga

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...