Monday, September 26, 2011

Kwa nini tatizo la fedha limekuwa sehemu ya maisha ya wakristo?


 
Biblia imeshaweka wazi katika Yerema 29:11 na 3 yohana 1:2 kwamba mawazo aliyonayo Mungu juu yetu ni mawazo/mipango ya kutufanikisha, si hivyo tu bali anataka tufanikiwe katika mambo yote. Pia tunajua kwamba fedha na dhahabu ni mali ya Bwana si hivyo tu bali sehemu kubwa ya Biblia imejaa ahadi za Mungu za kutufanikisha kifedha na mafundisho mengi ya pesa.

Sasa licha ya haya yote na ukweli kwamba tumemwamini huyu Yesu lakini bado maisha ya mkristo mmoja mmoja, wakristo wengi, kanisa kwa ujumla, kwaya, makundi ya kiroho na huduma mbalimbali hali yake ya kifedha ni ngumu. Kila mtu analalamika juu ya pesa, mpaka imefika mahali tatizo la fedha limekuwa sehemu ya maisha.


Mikutano, semina tumeshindwa kufanya kisa fedha, vijana wameshindwa kuoa kisa pesa, kwaya hazirekodi kisa fedha. Kitu gani kimetokea kwa wakristo. Wazungu wanasema “Something must be wrong some where” maana yake lazima kuna kitu hakijakaa sawasawa mahali fulani.

Kusudi la waraka huu mfupi ni kukuelezea sababu ambazo zimepelekea tatizo la fedha kuwa sugu na kwa sehemu ya maisha kwa wakristo wengi. Sababu hizo ni ;
Moja, kukosa maarifa (mafundisho) ya kutumia fedha ki-Mungu.

 Hosea 4:6a Fedha ina kanuni zake za matumizi. Hivyo kushindwa kujua kanuni hizo na namna ya kuzitumia hizo fedha ki-mungu basi tatizo litaendelea kuwapo.

Mbili, matumizi ya fedha ya Mungu nje ya kusudi lake.
Hagai 2:8, Sikiliza fedha ni mali ya Bwana, hata ikiwa mikononi mwako bado ni ya Bwana, hivyo ni lazima itumike kwa mapenzi yake, maana kila pesa anayokupa ndani ina kusudi fulani au anakupa kwa lengo fulani.

Tatu, Roho ya mpinga kristo inafanya kazi ndani ya fedha.
 2 wathesalonike 2:7, sikiliza, shetani anajua ukiwa na fedha yeye atakuwa na hali ngumu sana maana utaituma hiyo fedha kuimarisha agano la Bwana, hivyo ameweka Roho ya mpinga kristo ndani ya fedha ila kupinga  fedha isiende kwa watu wa Mungu ili washindwe kumtumikia Mungu.

Nne, kukosa nidhamu katika matumizi ya fedha.
Tito 3:14 Watu wengi hasa waliokoka, hawana nidhamu katika matumizi ya fedha pindi inapofika katika mikono yao. Hawana malengo mazuri katika mtumizi ya fedha na kwa sababu hiyo wanajikuta fedha wanayoipata inatumika kienyeji na kwa sababu hiyo tatizo la fedha lina baki palepale.

Tano,Ufahamu mdogo wa Neno la Mungu kuhusu fedha.
 Wakristo wengi sana wanayo mistari mingi sana inayozungumza uponyaji na kutoa mapepo, na hata imani yao imeongezeka kwenye maeneo hayo. Lakini kwenye eneo la pesa ufahamu wao ni mdogo sana, si wengi wanaopata mafundisho katika nyanja ya fedha ya kutosha.


Sita, Kuwategemea wanadamu na si Mungu .
Katika Yeremia 17:5 Mungu ametoa ole kwa wale wanaowategemea wanadamu.Hii pia imekuwa sababu kubwa sana ya tatizo la pesa kuwa sugu. Ni kweli watu wanamuomba Mungu awabariki, lakini mioyo yao inawategemea wanadamu na tayari ole imeshatiliwa kwa mtu anayemtegemea mwanadamu ki-mafanikio.

Mwisho, ni vifungo na laana za kifamilia, kiuokoo, kitaifa nk.
Kwenye eneo la pesa, kuna baadhi ya watu wamefungwa wasifanikiwe kifedha katika ulimwengu wa kiroho. Hili ni tatizo la kiroho zaidi na pia wengine ni laana zinazotokana na kushindwa kulijua neno la Mungu. Soma kumbukumbu 28:15-60.
Ni maombi yangu kwamba Mungu akusaidie kuwa na mahusiano mazuri na yeye hasa kwenye eneo la fedha ili uone baraka zake.

Na: Patrick Samson Sanga.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...