Tuesday, October 11, 2011

Maamuzi Unayofanya Katika Kutafuta Mwenzi Wa Maisha Yasiharibu Kusudi La Mungu Kwako.


Isaya 55: 8 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana”.



Najua yamkini umeusoma au kusikia na hata kuufundisha sana huu mstari. Lakini leo katika kona  hii ya ndoa nataka nikuonyeshe tafsiri ya huu mstari kwa kadri ya neema ambayo Bwana amenijalia kwenye hili eneo. 

Ukisoma vizuri huu mstari utagundua kwamba kulikuwa na ushindani/ kutofautiana kimawazo kati ya Mungu na hawa watu anaowasema hapa. 

Yeremia 29:11 inasema “maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi asema Bwana….” Sasa ukiunganisha maneno ya Yeremia 29:11 na yale ya Isaya 55: 8 utagundua kuna mawazo na njia za kutekeleza hayo mawazo  ambazo Mungu alikuwa nazo juu ya maisha ya hawa watu.

Sasa tatizo na wao kuna mawazo na njia walikuwa nazo juu ya maisha yao ambazo hazikuwa sawasawa na zile za Mungu. Na ndiyo maana akasema mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu. Kwa lugha rahisi Mungu alikuwa akisema geukeni/acheni hayo mawazo (mipango) na njia zenu tekelezeni mawazo yangu na njia zangu ndipo mtafanikiwa. Mungu alisema hayo maneno bada ya kuona matokeo ya mawazo na njia zao ni mabaya, kwa kuwa yalikuwa nje ya kusudi lake juu yao.

Ukitaka kuthibitisha kauli hii soma ule mstari wa 7 katika Isaya 55 Biblia inasema “Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake; na amrudie Bwana naye atamrehemu, na arejee kwa Mungu wetu naye atamsamehe kabisa”.
Anaposema mtu mbaya/asiye haki anamaanisha mtu ambaye anataka kutekeleza mawazo na njia ambazo zipo kinyume na mawazo na njia za Mungu juu ya maamuzi/suala/jambo lolote linalomkabili huyo mtu.

Maana yake nini mambo haya?

Katika maamuzi ya kupata/kutafuta mwenzi wa maisha najua kabisa  kuna mambo/vitu ambavyo ungependa huyo mwenzi wako awe navyo. Kuna namna fulani ungetamani awe kiumbile, kiumri, kikabila, kielimu, kiutajiri, nk, kwa kifupi tuseme haya ni mawazo yako juu ya mwenzi wako wa maisha . Niseme kwamba ni kweli haya ni mawazo yako lakini usifikiri Mungu naye hana mawazo ya nani anastahili/anafaa kuwa mwenzi wako wa maisha. Hakika Mungu anayo  mawazo tena mazuri kabisa juu ya nani anafaa kuwa mwenzi wako.


Hii ni  kwa sababu yeye ndiye aliyekuumba na ndani yako ameweka kusudi lake ambalo anataka litekelezwe kwa njia au mikakati yake. Moja ya mikakati hiyo ni kuhakikisha unoa au kuolewa na mtu aliyemkusudia yeye.
Jifunze kuruhusu mawazo ya Mungu na njia za Mungu zitekelezwe katika maisha yako,  ili kusudi lake liweze kufikiwa.

 .
Kumbuka Mithali 16:1 inasema, maandalio ya moyo ni mwanadamu, bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana. Unaweza kupanga au kuamua aina ya  mwenzi unayemta na ukaweka sifa/vigezo kadha wa kadha lakini  Kibiblia/Ki- Mungu SI LAZIMA iwe kama ulivyopanga kwa sababu mwenye kutoa jawabu la ulimi juu ya maandalio ya moyo wako ni Mungu.

Nimalizie kwa kusema kazi ya Roho mtakatifu ni kukushauri na kukuongoza  na si (kukulazimisha) katika yaliyo mapenzi ya Bwana. Hivyo hata katika suala la mwenzi wako yeye atafanya wajibu wake ikiwa utamruhusu. Maamuzi yanabakia kwako kutekeleza mawazo na njia zake kwako, ukikakataa uwe na hakika umekaribisha  mabaya na kutotendewa haki katika ndoa yako sawasawa na Isaya 55:7 na mwisho wenu ni majuto.

Mpendwa wangu angalia sana maamuzi unayotaka kufanya, hakikisha yamepata kibali cha Bwana ukikumbuka haya ni maamuzi makubwa na yanagharimu sana.

Na Patrick Sanga

1 comment:

  1. BLESS YOU...Hakika mawazo na njia za MUNGU ni KWELI NA HAKIKA.

    ReplyDelete

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...