Thursday, July 7, 2011

Kanisa na mtindo wa kuwatangazia watu vifo



Katika siku za hivi karibuni hapa nchini kumetokea na tabia au hali ya baadhi ya watumishi kuwatangazia vifo watu mbalimbali kulingana na mazingira fulani fulani Tumeshuhudia watumishi kadhaa wenye majina makubwa wakijitokeza hadharani au kupitia madhabahu ya makanisa yao na kutangaza vifo kwa watu wengine.

Wengi tuliona namna watumishi hao walivyosisitiza kuwa Sheikh Yahaya ni Lazima afe, na msisitizo huu ulitawala kwenye vyombo vingi vya habari mwisho wa siku mwaka huu mwezi uliopita(wa sita) sheikh huyo alifariki. Wiki mbili zilizpita kuna mtumishi wa Mungu tena, amemtangazia kifo mtoto wa Sheikh Yahaya ambaye ndiye mrithi wa Sheikh huyo. Kama vile haitoshi kuna watumishi wengine wamesimama kidete wakisema Babu wa lolindo ni lazima afe na wamekuwa wakivunja na kupigiza kazi za babu huyo.

Mimi sina ugomvi na hilo kwa kuwa watumishi hao kuna maandiko wanasimamia katika kutekeleza jambo hilo, ila kikubwa hapa tuangalie namna ambavyo sheria inavyobainisha kuhusu uhalali wa kumtangazia mwingine kifo. Kwa mujibu wa sheria za nchi hilo jambo si sahihi na anayetangaziwa kifo endapo akienda mbele kwenye vyombo vya sheria anayo haki ya kumshtaki yule aliyemtangazia kifo.  

Kama ambavyo leo mtu anaweza kukutukana na ukaenda mahakamani na kumshitaki na sheria ikachukua mkondo wake ndivyo hivyo watumishi wa Mungu wanaweza na kujikuta siku moja katika vizimba vya mahakama kwa kosa la kumtangazia mtu mwingine kifo.

Lengo kubwa la makala hii ni kuwakumbusha watumishi mbalimbali kuwa kama Kanisa la Tanzania litaendelea na utamaduni huu wa kutangaza vifo kwa watu badala ya kufikiri namna ya kuziokoa roho zao lazima tukubali kuwa kuna mahali tumepungua, Hii ni kwa kuwa hata kristo hafurahii kifo cha mtu mwenye dhambi ikiwa atakufa pasipo kumjua yeye .

Kama kanisa ni jukumu letu kuendelea kufanya kazi ya Mungu tu pasipo kulumbana sisi kwa sisi, au sisi na upande wa giza. kwa kuwa katika kufanya kwa ufanisi ile kazi ambayo Mungu alituitia yeye Mungu hufurahi(Nehemia 8:10) na hushuka kutupigania hivyo vita si vyetu bali vita ni vya Bwana kwa kuwa ndiye aingiaye vitani na si maneno yetu,  umati wa washirika wetu, wala heshima tuliyo-jilimbikizia kutokana na huduma tunazozifanya.

Naheshimu sana kazi za watumishi hawa na namna ambavyo wamekuwa mstari wa mbele katika kuujenga na kuuimarisha mwili wa Krist hapa nchini. Idadi ya watu walio nyuma yao(waumini) inaweza kuwa ni ishara tosha katika kulithibisha hilo kuwa Mungu amekuwa akiwatumia katika kuziponya Roho za wengi.

Tunapomtangazia mtu kifo inamaana unamfanya aishi maisha ya wasiwasi au woga, hivyo hatari na uvunjifu wa amani inaweza  tokea pindi aliyetangaziwa kifo ataenda mahakamani na kushitaki. Endapo leo mtumishi yeyote akishitakiwa kwa kosa hilo huku nyuma wafuasi wa mtumishi huyo wanaweza andaa mgomo au maandamano kupinga mtumishi wao kufikishwa mahakamani. 

Hadi hapo unaweza kuona namna ambavyo kauli hizi zinavyoweza kuleta kama si kuamsha machafuko baina ya pande zote mbili.

Endapo itajatokea kuwa aliyetangaziwa ni wa dini nyingine kama ilivyo kwa Sheikh Yahaya, na upande wao nao wakatoa matamko kama hayo dhidi ya watumishi wa Mungu. Hapo unahisi nini kitatokea na hali ya amani itakuwaje baina ya pande zote mbili ?

Changamoto iliyoko hapa ni kuwa toka huu mtindo wa kutangaza vifo uanze hakuna aliyetangaziwa kifo aliyekwenda mahakamani kushitaki, ila ipo siku atatokea atakwenda ndipo mabishano makali ya kiimani na kisheria yatatokea ambayo kimsingi yangeweza kuepukwa kwa mtumshi kukaa kimya pasipo kutangaza wazi, ila akadeal na mtu huyo katika ROHO kwa kuwa ndiko vita Yetu iliko na si katika mwili wala kupitia Press Conference.
  
Pamoja na Kristo kuuona udhaifu wa Petro kuwa hakufanya kulingana na mpango wa Mungu juu yake(kristo), lakini bado YESU hakumfukuza Petro na hakumuondoa katika orodha ya wanafunzi wake, bali alimwambia kwa  upendo kuwa rudi nyuma.  Kristo alifanya hivyo kwa kuwa yeye mwenyewe kwenye Luka 9: 55- 56 anasema “Mwana wa Adam hakuja kuziangamiza Roho za watu bali kuziokoa” 

Mimi nafikiri sisi kama watumishi wa Mungu tuendelee na mikakati ya kuzidi kupeleka injili vijijini na sehemu mbali mbali, ili kuziponya Roho za watu kwa kuwa huo ndio wito wetu mkuu ambao Kristo alituachia, na kama ipo vita itakayoinuka dhidi yetu, yeye tunayemtumikia atainuka na kutupigania kwa kuwa vita sio vyetu vita ni vya Bwana.

Mboya V

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...