Friday, July 22, 2011

Makala maalumu: Wajibu wa kanisa kwa waongofu wapya hususani watu maarufu (Celebrities)

Kanisa lina wajibu mkubwa wa kufanya juhudi kuhakikisha waongofu wapya wanadumu katika wokovu.

Kumekuwepo na nguvu kubwa katika kanisa la leo ya kuhakikisha watu wengi wanafikiwa na injili ya Kristo Yesu, hili ni jema sana kwa kuwa ndio agizo letu kuu “Enendeni ulimwenguni kote mkaihubiri injili kwa kila kiumbe……….” . Changamoto iliyopo ndani ya kanisa leo ni kutokuwepo kwa uwiano kati ya nguvu itumikayo kanisani ya kuwaleta watu kwa kristo na nguvu ya kuhakikisha watu hao wanadumu katika wokovu.

Kanisa la leo yaani jamii ya watu waliookoka ni wazi kuwa mkazo mkubwa ni watu kuokoka kuliko namna ya kuwawezesha waongofu hao wapya wadumu katika wokovu . Sio jambo la kushangaza kuona nguvu  inayotumika ili kuwafikia watu kuanzia mafungu ya fedha kwa ajili ya uinjilisti na umishieni, Muda Maombi kwa ajili ya kuhubiri injili, havifikii hata nusu ya nguvu inayotumika katika kuwajenga kiroho watu ambao wamekata shauri katika harakati hizo za kumtangaza Kristo.

Kristo ndiye mchungaji Mwema naye hatoacha kondoo wake hata mmoja apotee bali humfuatilia hadi ampate
Baada ya watu kuokoka eidha wamehubiriwa au wameamua wenyewe watu hao huamini kuwa kanisani ndio mahali pa kupata faraja na kuanza safari mpya katika maisha yao. Kuna ambao wanakuwa wako vizuri kiafya na kiuchumi na wapo ambao hali yao ni tete mpaka nguo na chakula hutegemea kuvipata kanisani.

Wakati umefika wa kanisa kuanza kujikagua kabla halijatoka na kwenda kuhubiri endapo lina mikakati madhubuti ya kuwalea wachanga hao au la!!  Mengi ya makanisa tofauti na semina au darasa kwa waongofu wapya  pamoja na maombi baada ya mikutano hiyo mambo huishia hapo hapo kisha tunaamini Bwana atawaongoza kujisimamia katika wokovu kitu ambacho ni kigumu kuliko tunavyo fikiria.

Kanisa linaishia kusema wote waliompokea Kristo waende pale na kuorodhesha majina yao na namba zao za simu. Katika uchunguzi wangu nimegundua namba hizo na majina hayo ni mara chache kufanyiwa kazi na hata kama ufatiliaji utakuwepo basi haizidi wiki moja.

Inapotokea mtu akaokoka kisha baada ya muda mfupi kwa sababu yoyote akaachana na wokovu ni wakisto hao hao husema wokovu sio lelemama na maandiko kibao eti waitwao ni wengi lakini wateule ni wachache.
Ni kweli NENO ndivyo linavyosema lakini tumejiuliza kama kanisa Je nguvu tuliyotumia kuwajenga kiroho inazidi ile nguvu inayowashawishi kurudia dhambi? Na kwa nini watu tuliookoka tuaze kuwajudge waliorudi nyuma kama wasaliti kupindukia kanakwamba sisi tunaendelea na wokovu kwa nguvu zetu wenyewe  na si kwa NEEMA ya Kristo?

Utasikia flani karudi nyuma, flani nae karudi nyuma lakini tujiulize ni kwa kiasi gain tumewasaidia kusonga mbele? Na hata kama tumewasaidia ni kwa kipimo chetu au tumefikia vipimo vya Mungu katika kuwasaidia watu hao? Na kama mtu uliyeokoka unajisikiaje kusikia flani kaacha wokovu? Je Moyo unauma! au Unaona kawaida!

Kanisa kama mwili wa Kristo lahitaji kuwa na umoja kristo akasema kondoo mmoja akipotea mchungaji mwemahuwaacha wengine na kwenda kumtafuta aliyepotea.  kanisa halina budi kubuni namna mbalimbali ya kuwawezesha waongofu wapya wadumu katika imani.


WATU MAARUFU (CEREBRITIES) NA WOKOVU

Inapotokea watu maarufu Cebrities wakaamua kumpokea Kristo jamii ya watu waliookoka hufurahi pasipo kujiuliza nini wajibu wao katika kuhakikisha Cebrities hao wanadumu katika wokovu. Tumeshuhudia Cerebrities wengi Duniani na Afrika mashariki wakiokoka na wengi wamedumu katika wokovu na wengne wameshindwa kuendelea na wokovu.

Wajibu wakanisa kwa waongofu wapya wakiwemo ma Celebrities ni kuwaombea siku zote wasimame katika wokovu pasipo kukata tamaa Luka 18:1

Ifuatayo ni orodha ya watu maarufu hapa nchini na nchini Kenya waliokata shauri na kutangaza kuwa wameokoka. Wapo ambao wanaendelea na wokovu lakini pia wapo ambao kwa namna Fulani wamekwama njiani.



Linah Sanga

Linah Sanga
Huyu ni Binti aliyekulia katika mazingira ya wokovu, wazazi wake wameokoka na wanasali katika kanisa la Ufufuo na Uzima chini ya Askofu Gwajima. Kabla hajaingia kwenye bongo flavour alikuwa tayari amesharekodi album yake ya Gospel. Lina akiwa kanisani alikuwa muimbaji katika kikundi cha GROLIA  Singers Kilichopo katika kanisa hilo. Licha ya kuwa muimbaji katika kikundi hicho pia alikuwa mwalimu wa kikundi hicho.


Linah aliwahi kuwa mmoja wa waimbaji wa Remmy Ongala Band iliyokuwa kanisani hapo ikimuimbia Mungu chini ya Marehemu Remy Ongala. Hatujui nini kilimsibu hivyo akaamia kuimba nyimbo za dunia(circular Music) hususan bongo Flavour.


Changamoto iliyopo kwa kanisa ni Je kanisa linamuona Lina kama msaliti kupindukia mfano wa takataka!! Au kanisa(watu waliookoka) bado usiku na mchana linamuombea kwa Mungu pasipo kuchoka ili arudi madhabahuni na kuendelea na wokovu?. Kanisa linaweza mhukumu kwa namna anavyoenenda lakini lisisahau wajibu wake kwake.


Mwanamuziki KIDUMU toka nchini Kenya


Kidumu
Huyu mkaka yeye naye ni kama Linah Sanga, yeye kabla hajaingia kuimba circular musics tayari alikuwa amerekodi album nzima ya nyimbo za Injili. Wakati nyimbo za Injili alizotoa Linah hazikuweza kujulikana sana kwa kidumu yeye ni tofauti. Nyimbo zake za Injili zilikuwa maarufu mno nchini Kenya na zilichezwa sana kwenye vyombo vya habari.


Naye baada ya muda akaibukia kwenye Bongo Flavour. Labda nirudie makala hii haikusudii kulea dhambi bali kulikumbusha kanisa kuweza kujua bado linawajibu juu ya watu hawa.

Ni rahisi sana kwa mtu aliyeokoka kumshangaa Kidumu kwa uwamuzi wake huu na wakati mwingine kumhukumu kwa hilo. Nilichogundua ni kuwa pamoja na lawama zote hizo ni vigumu kwa mtu aliyeokoka kupiga magoti na kuomba Rehema za Mungu juu ya Kidumu, hivyo tunabaki kulaumu pasipo kuwajibika.

Nuruelly

Mimi ni kama nani niseme naringaaaa
Vita uadui kwa wenzangu mi wakati niumbwaaa
Tumeagizwa Upendooo oooh  x 2

Jamaa anaitwa Nuruelly na hiyo nyimbo aliifanya back in Days wakati yupo katika Salvation inaitwa Tumeagizwa Upendo. Nuruelly alimpokea Kristo na kuanza kuishi maisha ya wokovu. Lakini hakuna ajuaye fika nini kilimsibu akaamua kurudi na kuanza tena kuimba nyimbo za Duniani akishirikiana na Swahiba zake Banana Zoro pamoja Ismail chini ya B Band na kutoa nyimbo iitwayo Nzella.


Nuruelly baada ya kuokoka alitoa album ya injili iliyoenda kwa jina Hilo Tumeagizwa upendo. Maadamu Bado Nuruelly anapumua inamaana Neema ya Wokovu ingali ipo ikimuangazia. Hivyo kanisa pasipo kuchoka linawajibu wa kumrudisha madhabahuni kwa upendo ingawa si jambo jepesi ila inawezekana.


Ummy Wenceslaus (DOKII)


Ummy - Dokii
Huyu ni msanii mkongwe wa maigizo hapa nchini, kabla hajatangaza kuwa ameokoka baada ya kuugua kwa muda mrefu alikuwa Muislamu. Baada ya kuokoka na kuanza kusali kanisa la Universal lililoko maeneo ya mnazi mmoja jijini Dar es salaam, Dokii aliwahi kutoa album ya nyimbo za injili na alifanikiwa kuzunguka mikoani akiinadi album hiyo na akitangaza matendo makuu ya Kristo Yesu.

Wengi wamesema mengi juu ya wokovu wa Dokii, ila kilichonifanya nimuweke hupa Dokii tofauti na wasanii wengine ni kauli zake juu ya wokovu. Pamoja na yote anayopitia Dokii anakiri wazi kuwa ameokoka. Celebrities’ wengine waliowahi kutangaza kuwa wameokoka wakiulizwa swali hilo hupiga chenga.


Haijalishi anapitia nini Maadam bado ndani yake anatamani kuendelea kusimama zaidi, kanisa halina budi kumsemea positive na kumsaidia na sio kumpiga vijembe eti ooh alidhani wokovu ni lele mama, mara hajafunga mkanda Yuleee!, wengine ooh hakuhesabu gharama!. Lugha hizi kwa kanisa si sahihi kwa kuwa changamoto anazokutana nazo Dokii na Celebrities wengine ni kubwa hivyo anahitaji wapambanaji(kanisa) watakaoingia vitani pamoja nae kwa utukufu wa Mungu.


Cosmas Chidumule, Mzee Makasy na Dr Remmy Ongala

Hawa wote ni watanzania wenye asili ya Kongo Kinshasa, Chidumule na Makasy ndio waliokuwa wa kwanza kufika nchini. Baada ya muda mzee makasi alirudi kongo zamani Zaire ili kusalimia, akiwa huko alimshawishi Ramadhani Mtoro(Dr Remmy) kuja nchini na kufanya muziki wa Dansi.

Mzee Makasy
Dr Remmy alikubali na hivyo wakaja nchini miaka hiyo ya themanini. Katikati ya miaka ya tisini kila mmoja kwa wakati wake Chidumule na Makasi waliyakabidhi maisha yao kwa Yesu. Baada ya kufika Dr Remmy alikuwa maarufu sana na baada ya kuugua kwa muda mrefu nayee aliyakabidhi maisha yake kwa Kristo na kuanza kusali katika kanisa la Ufufuo na Uzima mpaka alipofariki mwaka jana 2010.


Dr Remmy, Mzee Makasi na Chidumule ni mfano wa kuigwa kuweza kuona kumbe hata masupester wanaweza kudumu katika wokovu. Makasi na Chidumule ni zaidi ya miaka kumi kwa Neema za Mungu wako bado ngangari katika wokovu.



Renee Lamira

Renee Lamira
Mwanadada huyu ambaye alikuwa mwanamuziki wa nyimbo za Kizazi kipya(Bongo Flavour), kwa sasa ameolewa. Baada ya kuokoka Renee miaka takribani mitano iliyopita alikuwa akisali katika kanisa la Living Water Kawe makuti.

Wengi walitegemea kuwa baada ya kuokoka Renee atafanya muziki wa Injili, Lakini baada ya kuokoka Renee amekuwa kimya akifaya mambo yake huku akimtumikia Mungu.



Basil Kashumba K´ Basil
Watanzania wengi wanamfahamu K´ Basil baada ya kufanya nyimbo ya RIZIKI akimshirikisha mwanamama Stara Thomas wakati akisoma chuo kikuu cha Dar es salaam(UD). Ni miaka takribani miwili kama sio mitatu tangu K Basil alipompokea kristo. Tofauti na Ma Celeb wengine K Basil yeye baada ya kuokoka ameamua kuwa mtumishi wa Mungu.

Basil ambaye anatumika katika kanisa la Ufufuo na Uzima lililo chini ya Askofu Gwajima. Kitendo cha kumlea muongofu mpya hadi aelewe na kupanda viwango hadi kuwa mchungaji sio kazi ndogo. Pongezi za pekee ziwaendee kanisa hilo kwa namna walivyomkuza Basil kwa utukufu wa Mungu. Hivi sasa K Basil amesharekodi album nzima ya nyimbo za injili aliyoipa jina la “Ahsante Yesu”


Joseph Kelvin Mapunda Q-Jay

Joseph Mapunda Q jay
Kijana huyu alikuwa mmoja wa wanamuziki wa kundi la Wakali Kwanza. Alilipotiwa kumpokea Kristo januari mwaka huu. Q – JAY ni mchanga katika wokovu na wengi wanamuona kama anajaribisha maisha ya Wokovu.


Changamoto iliyopo ni kuwa ikiwa watu wengine wanamuona ni kama anajaribu, je kanisa linamchukuliaje? Na kumsaidia vipi katika safari yake ya wokovu.

Q  Jay baada ya kuokoka alisema hatoingia studio na kuimba nyimbo za injili mpaka baada ya miezi sita kwa sasa ameoa na anendelea na wokovu.

DNA Banjuka

DNA
Kijana huyu kutoka nchini Kenya alifahamika sana Afrika Mashariki na Kati baada ya kutoa nyimbo yake iitwayo BANJUKA. Mwaka mmoja baada ya kutoa album yake ikiwa na nyimbo yake hiyo aliamua kumpokea Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake.

Katika Interview mbalimbali DNA haachi kusema wakati wote huo kabla hajaokoka alikuwa mlevi kupindukia.Kwa sasa huu ni mwaka wa pili DNA akiendelea na wokovu. Kwa sasa licha ya kuimba nyimbo za Injili DNA ni mtangazaji wa kituo kimoja cha Redio ya Kikristo jijini Nairobi.


Stara Thomas

Stara Thomas
Mwanamama huyu ni maarufu mno Afrika Mashariki kwa uimbaji wa muziki wa kizazi kipya hususani muziki wa Zouk. Mwaka huu mwanzoni alilipotiwa kumpokea kristo kama Bwana na Mwokozi wa Maisha yake.

Unaweza usikubali ila ukweli unabaki pale pale kuwa kusimama katika wokovu kwa Stara Thomas na maceleb wengine kwa namna moja au nyingine huimarisha fikra za watu kuwa kuokoka inawezekana, na wachanga katika wokovu huwajenga sana kifikra na kiimani kuona wamechukua uamuzi sahihi.

Hivyo ni jukumu la kanisa kuwaombea maceleb kama huyu kwa kuwa kusimama kwao katika imani huimarisha viroho vya wengine.



Emmanuel Myamba

Katika wasanii wa maigizo nchini huyu mtumishi ni mmoja kati wa watu waliosimama kwenye wokovu. Ameokoka siku za nyuma wakati akiwa A Level pale Jitegemee sekondari. Tofauti na wengine yeye aliokoka kabla hajawa celebrity na ni mhitimu wa Chuo kikuu cha Dar es salaam alikochukua masomo ya Sosholojia.

Myamba kwa sasa anakampuni yake ya kutengeneza Filamu iitwayo Born again Films. Mtumishi huyu ni mfano wa kuigwa kwa wasanii wa Filamu na maigizo nchini. Ameweza kuonyesha kuwa unaeweza kuwa superstar wa Filamu na usilewe sifa bali ukatumia Filamu katika kumtangaza Kristo, kwa sasa anasali kanisa la Living Water Centre chini ya Apostle Ndegi.



Jacob Stephen JB

Jacob Stephen JB
Huyu ni mcheza Filamu maarufu hapa nchini na ni mmoja ya watu waliotangaza kuwa wameokoka miaka kadhaa iliyopita na mpaka sasa anaendelea na wokovu,  JB anasali Mikocheni B Assemblies of GOD kanisa lililo chini ya Mch Mama Getrude Rwakatare.




Ndubagwe Misayo (THEA)

Mdada huyu nguli katika Tasnia ya Filamu na maigizo nchini, ameokoka ingawa wengi wanaweza wasiliamini hilo. Kwa mujibu wa watu wake wa karibu wameithibitishia Hosanna Inc kuwa ni kweli Thea ameokoka na anahofu ya Mungu.

Mwanzoni kabisa wakati anaanza wokovu alikuwa akisali kanisa la Ephata Mwenge lililo chini ya Prophert Josephat Mwingira. Changamoto iliyopo kwa kanisa ni pale tunapomtaka mtu mchanga kiroho baada ya kuokoka aache kila kitu pasipo kumpa muda.


Nakumbuka Apostle Danstan Maboya aliwahi toa ushuhuda huu, kuna siku alipokuwa akihuhiri injili kuna jamaa mmoja tajiri alikata shauri na kuokoka, na Siku hiyo ndio alikuwa akimaliza mkutano wake wa injili. Yule jamaa akamuomba Maboya kesho yake waonane na kweli wakaonana. Walipoonana Maboya alimuuliza ulipotoka Mkutanoni jana ilikua je? Jamaa akasema nilifika nyumbani nikaoga kisha nikapiga bia zangu mbili then nkaenda kulala.


Thea Kulia akiwa na Kanumba
Huyo jamaa leo ni mtumishi wa Mungu, wokovu ni Process, tunaamini mapungufu yapo kwa kila mtu ili kufikia kimo cha Ukamilifu wa Kristo. Hatuna budi kuwaombea wengine ili waukulie wokovu kwa kuwa ni kwa Neema ya Mungu tunatoka kiwango mpaka kiwango katika wokovu.



James Temu (Jimmy)
Huyu Brother ni Muigizaji wa Filamu hapa nchini na pia Jimmy ni mtangazaji wa Praise Power Radio. Ameshiriki katika movie nyingi. Jimmy Ameokoka na anasali katika kanisa la Mtume Kingu lililoko jijini Dar es salaam. Ni mmoja kati ya waigizaji wa Filamu ambao wameokoka  na wako serious kwenye wokovu.

Bro Jimmy akiwajibika katika Filamu


Emmanuel Mgaya (Masanja Mkandamizaji)

Masanja Mkandamizaji akisikiliza Neno la Mungu katika Semina ya Mwl Mwakasege viwanja vya Biafra jijini Dar es salaam
Huyu jamaa ni KWELI ameokoka na ni mmoja wa maceleb ambao wamemaanisha katika wokovu. Yapata takribani mwaka sasa toka masanja aamue kumpokea Kristo na amekuwa akizunguka sehemu mbalimbali huku akihubiri Neno la Mungu.

Licha ya kuhubiri pia anayo album yake inayoitwa Hakuna jipya na alishiriki kuimba mara kadhaa katika mkutano wa Askofu Moses Kulola uliomalizika hivi karibuni katika viwanja vya jangwani jijini Dar es salaam

Kwa sasa Masanja anasali katika kanisa la EAGT Mito ya Baraka lililoko Jangwani jijini Dar es salaam chini ya Askofu Bruno Mwakiborwa. Tofauti na mastaa wengine Masanja toka aokoke hajawai kupata kashfa yeyote juu ya wokovu wake.




Hitimisho
Kanisa bado linawajibu wa kuwaombea na kuwafundisha waongofu wapya kwa upendo, na tusitake mtu afundishwe kuendesha gari leo kisha kesho awe dreva mzoefu, bali tuwape muda na kuwaelekeza kadri ambavyo Roho anatusaidia kuwaelekeza kwa utukufu wa Mungu.

Kwa kuwa Kwa Neema ya Kristo atawawezesha kusimama, Efeso 3 :20 “Na atukuzwe yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu mno kuliko yale tuyaombayo au tuyawazayo” hivyo Kristo yupo kuwapa nguvu ya kuendelea mbele na wokovu.


By Mboya V

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...