Saturday, July 16, 2011

Ripoti Maalumu: Uliwahi kumsikia Nabii Eliya Msangi toka same aliyekuwa na wake kumi na Watoto hamsini?

Mwanzoni mwa miaka ya sabini katika kitongoji cha Igongwe kijiji cha Mbwamkeni wilaya ya same mkoa wa Kilimanjaro, alikuwepo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Nabii Eliya Msangi. Nabii huyo inayesadikika na wanakijiji nhaokuwa kuwa alikuwa akimtumikia Mungu aliishi katika kijiji hicho huku akiwa na wake kumi na watoto wapatao Hamsini(50).

Katika moja ya Malengo ya nabii huyo ni kuhakikisha wananchi wa kijiji hicho wanaishi kama familia moja mithili ya kijiji cha ujamaa huku akisisitiza upendo kati ya wanakijiji wa kijiji hicho. Habari ya maisha ya kijiji hicho zilienea sehemu mbalimbali na hivyo kuna watu wengi walianza kufurika kijijini hapo na kuishi maisha kijamaa ya dini ya kikristo iliyoanzishwa na nabii huyo.

Kitongoji hicho chenye ukubwa wa Ekari zaidi ya 40 awali kilijulikana kwa jina la Shina la chama cha Tanu, baadaye watu walipoanza kuishi chini ya Nabii huyo  kilianza kupata maendeleo kwa kasi kubwa hali iliyopelekea watu mbalimbali mashuhuri kufunga safari na kwenda kutembelea kijiji hicho akiwemo Augustine Mrema, pamoja na Mh  John Malechela aliyewahi kuwa waziri mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 1978 Afisa maendeleo ujamaa na Ushirika aliwaandikia barua ya pongezi kwa  wanakijiji wa kijiji hicho kwa jitihada zao za kuzalisha mazao mbalimbali. Kisha  serikali iliingilia kati na kuamua kuwapa usafiri baada ya kuonekana mazao yao
mbalimbali yalikuwa yanaharibikia mashambani kwa kuwa yalikosa soko ya kwenda kuuzwa.

Mnamo tarehe 03 Mwezi wa nne mwaka 1996 nabii Eliya Msangi alifariki, miaka sita baadaye mmoja kati ya wake wa nabii huyo aitwaye upendo Msangi alipeleka shauri mahakamani ili aweze kupewa kibali cha kuwa msimamizi wa Mirathi ya Nabii huyo. Ikimbukwe kuwa baada ya watu mbalimbali kuhamia na kuanza kuishi walitoa nguvu zao na mali zao zikawa za jumuiya zikiongozwa na nabii Eliya.


Baada ya mke huyo kupeleka shauri hilo mahakamani lakini shauri hlo lilipingwa baada ya kuwekewa pingamizi, kisha Bi Upendo alikata rufaa na kulipeleka shauri hilo Mahakama ya wilaya ya same ambapo shauri hilo lilitupwa. 

Wakati wa uhai wa nabii huyo Nabii Eliya alitaka kijiji hicho cha Mbwamkeni kisajiliwe kama chama cha kidini kiitwacho Hema la Sayuni ombi ambalo lilikataliwa na msajili wa vyama  wizara ya mambo ya ndani  tarehe 03/02/1072.

Maisha Baada ya Kifo cha nabii Huyo

Baada ya kufariki kwa nabii huyo kijiji hicho kimeingia katika mvutano mkubwa wa kimaslahi kati ya watoto wa Nabii huyo pamoja watu wazima ambao kwa imani zao waliuza mali zao na kutoa mashamba yao kisha kuhamia katika kijiji hicho. Baadhi ya watoto hao wanadai wanahaki na mali za baba yao na wanawataka watu wote waliofika kwa ajili ya imani ya baba yao waondoke na kurudi walipotoka.

Aidha mgawanyiko huo upo pia miongoni mwa wake wa Nabii huyo kwa baadhi yao kuungana na watoto wa nabii huyo kutaka kuwa wasimamizi wa Mirathi. kitendo hicho ni kinyume cha makubaliano ya kikao cha wanakijiji wapatao 37 waliokaa na kumchagua mwanakijiji mwenzao Bw Augustino Ngalaba kuwa mkuu wa jamii hiyo na mwenye kusimamia mali hizo akisaidiwa na Bw Joram Kibaja.
,
Wanajamii hao walioishi kwa pamoja na ushirikiano kipindi cha uhai wa nabii huyo, kwa sasa wamegawanyika kiasi cha kufikia hatua ya kushikiana silaha za jadi hali ambayo inatishia amani katika kijiji hicho. Aidha uongozi wa kijiji hicho chini ya mzee Ngalaba umefungua kesi dhidi ya baadhi ya watoto wa Nabii huyo,hi ni baada ya kuvunja na kuchukua mali pamoja na nyaraka mbalimbali katika chumba kilichokuwa kinatumiwa na wazee hao.
Mmoja wa watoto wa Nabii huyo ajulikanaye kama Uzima Msangi kwa niaba ya watoto wenzake zaidi ya kumi anasema kwa sasa kwenye mji huo hakuna msemaji rasmi na mwenye kutatua matatizo yao, watoto waliopo wanapata shida na hawajui nani wamkimbilie huku wazee hao wakijiita ni wasimamizi wakitumia mali zilizopo ikiwemo nyumba vibanda vya biashara na mashamba yaliyopo mjini same kwa faida yao.

Uzima aliendelea kusema, “Ninachojua mimi dini ya Baba yangu haikusajiiwa na serikali  hapa nilipo siwezi kugusa mali yoyote ya baba yangu kuna miti mingi ukikata mti unafunguliwa mashitaka ni bora mali zigawanywe kila mtu na mama yake achukuwe chake ”

Tamko la Serikali juu ya Kijiji hicho                      

Mkuu wa wilaya ya Same Mh Ibrahimu Marwa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo  anasema, suala hilo ni lakifamilia zaidi na huwa linaibuka na kupoa na washawaweleza kuwa kama itatokea kutokuelewana wafike kwenye vyombo vya dola.

“Ni suala la Kifamilia zaidi kwa kuwa kuna watoto hawataki kuishi kwewnye kitongoji hicho wanataka mali zigawanywe na serikali haiwezi kuingilia kwa kuwa ni familia inagombana ” alisema mkuu huyo wa wilaya.


Source: Salome Kitomari Same.

Katika Ulimwengu wa leo kanisa linakabiliwa na changamoto nyingi kulingana na Kuongezeka kwa imani tofauti tofauti. Hivyo ni jukumu la kila mkristo kuiifahamu kweli, hii itasaidia kuepukana na matatizo ambayo yanatokea kila siku ambayo kimsingi yanaweza kuepukwa kwa urahisi pindi kweli inapotuweka huru na kutupa upeo wa kuchambua mambo kabla hatujachukua hatua yeyote - Hosanna Inc.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...