Tuesday, June 7, 2011

MAASKOFU WA TANZANIA (CCT), WAMPA RAIS KIKWETE MASAA 48 KUTHIBITISHA UKWELI WA KAULI YAKE


Tarehe 5/6/2011 RAIS Jakaya Kikwete aliwaonya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini kuacha tabia ya kushiriki biashara ya kuuza dawa ya kulevya na badala yake
washirikiane na viongozi wa serikali katika kudhibiti biashara hiyo haramu.

Kauli hiyo ilitolewa na Rais Kikwete wakati akihutubia waumini wa dhehebu la Kanisa Katoliki jimbo la Mbinga kwenye ibada maalum ya kupewa daraja la Uaskofu na kusimikwa kwa Mhashamu Askofu John Ndimbo wa jimbo hilo katika kanisa la kiaskofu la mtakatifu Killian.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Rais Mstaafu Benjamini Mkapa.

Rais Jakaya Kikwete akiwa na kadinali Pengo kushoto pamoja na Mhashamu askofu John Ndimbo
Rais Kikwete alisema kuwa baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakishiriki biashara ya dawa za kulevya kwa kuwafanya mipango ya kuwatafutia vijana hati za kusafiria kwenda nchi za nje kufanya biashara hiyo.
Kutokana na hali hiyo aliwataka viongozi wa dini kukemea biashara hiyo na kujenga uhusiano mzuri na vyombo vya dola kuhakikisha biashara hiyo haramu inakomeshwa kwa kuwafichua wahusika wanaofanya biashara hiyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Inasikitisha sana na kutisha biashara hii haramu sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu, Taifa letu litaharibika tusipokuwa makini katika hili, baadhi yenu tumewakamata”,
“Kauli zenu kemeeni jambo hili kwa kuelimisha jamii hususani vijana waweze kuepuka na matumizi ya dawa ya kulevya,” alisema Rais Kikwete.

MASAA 48  YA KUTHIBITISHA UKWELI WA KAULI YAKE

Jana 6/06/2011 Jumuiya ya Maaskofu wa makanisa ya Kikristo Tanzania(CCT) walimpa Rais Kikwete saa 48 za kuwataja kwa majina viongozi wote wa Dini anaowatuhumu kuhusuka na biashara haramu ya madawa ya kulenya "unga".Maaskofu hao wamesema endapo Rais atashindwa kufanya hivyo, basi itachukuliwa kwamba siyo mkweli. Mkutano huo baina ya vyombo nya Habari na CCT ulionyeshwa pia kwenye taarifa ya Habari ya saa mbili usiku katika kituo cha Television cha ITV.

Agizo la CCT lilitolewa na Mwenyekiti wake taifa, Askofu Peter Kitula jijini Dar es Salaam  katika mkutano na waandishi wa habari linasema, “Tunampa saa 48 rais awataje kwa majina viongozi hao ambao yeye anadai wanajihusisha na kuuza dawa na kama atashindwa kufanya hivyo tunamtafsiri ni mwongo na mzushi... Tunasikitishwa na kushangazwa kwa kauli hiyo na tunamheshimu kama kiongozi wa nchi, hivyo tunampa masaa hayo awataje kwa majina” alisema Kaimu Mwenyekiti wa CCT, Askofu Mokiwa akichangia hoja.

Wakahoji, ikiwa Rais anawafahamu viongozi wa dini wanaohusika na biashara ya kuuza "unga" iweje ashindwe kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwakamata na kufunguliwa mashitaka?
Askofu Valentino Mokiwa wa Kanisa la Anglikan nchini ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Jumuiya ya Maaskofu wa makanisa ya kikristo Tanzania (CCT)

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...