KANISA la Baptisti Galilaya Iringa limeeleza kusikitishwa na migomo mbali mbali ya wanatalum ukiwemo ule madaktari unaoendelea hapa nchini kuwa ni migomo yenye lengo la kuwatesa watanzania masikini na hivyo kuwaomba wanataluma hao wakiwemo madaktari na walimu ambao wametishia kugoma kutanguliza hofu ya Mungu katika shughuli zao na kuachana na mpango huo kama njia ya kumpunguzia mzigo wa mawazo Rais Jakaya Kikwete.
Mch Mpeli Mwaisumbe |
Mbali ya kuwaomba madaktari kufanya kazi kwa kutangulia hofu ya Mungu na kuwaonea huruma watanzania wasio na kipata ambao ndio wanateseka na migomo hiyo bado aliwataka watanzania zikiwemo taasisi za dini nchini kuendelea kumwombea afya njema mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari nchini Dkt Steven Ulimboka na kuiombea serikali ya Rais Kikwete ili isiendelee kuandamwa na jinamizi la migomo isiyo na tija katika maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa jana na mchungaji wa Kanisa hilo Mpeli Mwaisumbe(Pichani) wakati wa ibada maalum ya kumsimika mchungaji mpya wa kanisa hilo Hebron Mwakamwamba ibada iliyomshirikisha pia askofu wa kanisa hilo Agripa Kyamajoli .
Alisema kuwa sifa ya amani ya Tanzania na upendo imeanza kutoweka katika kipindi hiki kutokana na wajuaji kuwa wengi na watu ambao ni tegemeo katika Taifa wakiendelea kugeuka kuwa tishio kwa watanzania wanyonge kwa kutangaza migomo mbali mbali kwa ajili ya kuangalia maslahi binafsi zaidi badala ya kuwasaidia watanzania wanyonge kuweza kunufaika na elimu zao.
Mwaisumbe alisema kuwa pamoja na mazuri ambayo Rais kikwete amekuwa akiyafanya ila kutokana na kuongezeka kwa matukio mengi ya migomo ya wanatalum ,Rais amejikuta akiwa katika mzigo mkubwa wa mawazo kila kukicha akiwaza ni wapi na kundi gani litaibuka na mgomo jambo ambalo wao kama kanisa wanaona migomo kama hiyo inazidi kumtesa Rais na hivyo kuna haja ya makundi hayo ya wanatalum kujaribu kumfanya Rais kupumzika na kushughulikia maendeleo ya watanzania kwa ujumla badala ya kila wakati kuzungumzia migomo ya madaktari na walimu.
" Ndugu zangu waumini hawa madaktari na walimu ni waumini wetu ambao tumekuwa tukisali nao kila jumapili na watoto wanaowafundisha na wagonjwa wanaowatibu madaktari ni miongoni mwa waumini wa taasisi zetu za dini na watanzania wenzao ....sasa leo tunaposikia daktari anagoma kumtibu mgonjwa ambaye ni mlalahoi mwenzake ama mwalimu anagoma kufundisha watoto wetu ....kweli hawatutendei haki sisi watanzania wanyonge hata kama wana hoja juu ya madai yao ila ni vema kutafuta njia nzuri isiyo mnyanyasa mwingine kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi badala ya kukimbilia kugoma .....naomba sana wataalam wetu wanapofanya kazi zao watambue kabisa Mungu ndie anayewaongoza katika shughuli zao hivyo kabla ya kukimbilia kugoma basi kutanguliza hofu ya Mungu ambaye amewapa uwezo wa kuwa katika nafasi hizo kuliko kuwanyanyasa watanzania " alisisitiza mchungaji Mwaisumbe
Kuwa mambo saba katika Kanisa la kwanza yalikuwepo kwa sasa yameanza kutoweka na watu kuanzisha mambo yao wenyewe kwa kuwatenda vibaya wengine huku hata baadhi ya nyumba za ibada na watumishi kugeuza nyumba hizo za ibada kuwa ni sehemu ya kutafutia utajili binafsi ama kutafuta umarufu wa kisiasa badala ya kuifanya kazi ya Mungu.
" Leo katika Makanisa baadhi ya wahubiri wamekuwa wakiingiza siasa ya Chadema ama CCM na kutaka kila jambo ambalo wao wanalitaka lifanyike lifanyike hivyo ....nasema watumishi wenzangu tunalikosea kanisa na tunakwenda kinyume na maandiko matakatifu kwa kuchanganya siasa na dini katika nyumba hizi za ibada na ndio sababu kila kukicha Taifa limekuwa likiingia katika migomo na matukio ya ajabu ambayo awali hayakuwepo"
Hivyo aliwataka waumini wa kanisa hilo ambao ni wasomi kuacha kuingiza usomi wao katika nyumba ya ibada na badala yake kutanguliza maombi kwa kila jambo ili kulisaidia Taifa kuepukana na matukio ya migomo isiyo kuwa na kikomo inayoendelea hapa nchini.
Mwaisumbe aliwataka waumini wa kanisa hilo kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania chini ya Rais Jakaya Kikwete ,kuwaombea wabunge na spika wa bunge ili bunge liweze kurejea katika misingi yake ya kutunga sheria na kuwa ni chombo cha kuwawakilisha wananchi badala ya sasa chombo hicho kinavyotumika kama sehemu ya vijembe na malumbano yasiyo na tija kwa watanzania.
Huku askofu wa kanisa hilo Agripa Kyamajoli akiwataka watanzania kuendelea kumwombea afya njema Dkt Ulimboka ili apone na kuja kuungana na madaktari wenzake kuwatumikia watanzania .
Pia alitaka mambo zaidi kwa kila mtanzania kwa ajili ya kukemea na kupambana na watu wanaojihusisha na matukio ya kinyama kama hilo la Dkt Ulimboka ili washindwe na kuregea na kuachana na vitendo hivyo vya kinyama.
Na Francis Godwin
No comments:
Post a Comment