Sunday, July 8, 2012

Sunday Sermon:USIKUBALI KUFA KIFO CHA KIPUMBAVU.


2Samweli 2:31-34 na Zaburi 14:1 ‘Mpumbavu amesema moyoni, mwake hakuna Mungu…..’ Mpenzi msomaji naamini unaendelea vema kwa ujumla kimwili na kiroho. Katika mwezi huu nataka niseme nawe juu ya kifo cha kipumbavu.
Mpumbavu ni nani? Kibiblia ni mtu yoyote aliyekataa kuwa na ufahamu au elimu ya Mungu ndani yake. Mtu aliyekataa uwepo wa Mungu au kuwa na Mungu maishani mwake.

Hivyo basi kifo cha mpumbavu ni kifo cha mtu ambaye moyoni mwake amesema hakuna Mungu.Mauti inayomkuta mtu ambaye amekana elimu au ufahamu au uwepo wa Mungu katika maisha yake. Mauti inayommkuta mtu kabla hajakubali uwepo wa Mugu katika maisha yake. Kifo kinachomkuta mtu ambaye hajampa Mungu nafasi ya utawala moyoni mwake.


Tujifunze kwa Abneri. 2Samweli 2:22-39 ukisoma vema hapa utaona habari za shujaa mmoja aliyeitwa Abneri. Kwa kifupi Abneri alikuwa;
Kiongozi wa majeshi ya Sauli, mpinzani mkubwa wa Daudi, baadaye alipelekea Daudi kuitawala Israeli yote, Alimwua Asaheli shujaa wa Daudi ndugu yake Yoabu, kiongozi wa majeshi wa Daudi. Na mwishowe Yoabu ndiye aliyemwua Abneri ili kulipiza kisasi cha kifo cha nduguye.

Sasa baada ya kifo cha Abneri, ndipo Daudi akamlilia Abneri akasema, ilimpasaje Abneri kufa afavyo mpumbavu?, mikono yako haikufungwa wala miguu yako haikutiwa pingu; aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka.
Ukiendelea kusoma habari hii utaona kwamba siku ile Daudi alikataa kula akimliilia Abneri, akisema hamjui ya kuwa mkuu mmoja, naye ni mtu mkubwa ameanguka leo katika Israeli?

Je kwa mazingira ya leo, mtu anawezaje kufa kifo cha kipumbavu?Unaposhindwa kutumia fursa zilizopo kuiponya nafsi yako matokeo yake ni kifo cha kipumbavu. Abneri hakufungwa mikono wala miguu lakini aliuawa. Daudi alikuwa akimuuliza Abneri kwa nini usitumie mikono na miguu yako kuiponya roho yako? .

Katika Zaburi 14;1 TUMEONA MPUMBAVU NI MTU YULE AMBAYE MOYONI MWAKE AMESEMA HAKUNA MUNGU, kwa lugha nyepesi amekataa kuwa na Mungu moyoni mwake na kwa sababu hiyo amekataa uongozi wa Mugu katika maisha yake.
Kibiblia mtu wa namna hii anapokufa anaenda kuzimu na si paradiso au mahali pema peponi. Kumbe kwa lugha nyepesi mtu ambaye anakufa katika dhambi zake wakati fursa ya kuzitubu au kuziacha kabisa ilikuwepo ndiye anakuwa amekufa kifop cha kipumbavu.

Mpango wa Mungu ni kukuokoa kutoka katika dhambi ili usije ukafa kifo cha kipumbavu na ukaenda kuzimu kwenye mateso makali. Yohana 3:16 inasema ‘kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipoteee bali awe na uzima wa miele.

Neno ‘asipotee’ linawakilisha kifo cha kipumbavu . Mungu alimtoa Yesu ili wewe usife kifo cha Kipumbavu, kifo cha bila kumpa Mungu nafasi katika maisha yako.
Hivyo basi, Yesu ni fursa ya wewe kuitumia ili usife kifo cha kipumbavu. Kwa nini ufe katika dhambi yako, wakati Yesu yupo tayari kuiokoa nafsi yako isiangamizwe? Je ndugu yangu itakufaa nini kuupata ulimwengu wote na mali zake zote huku ukiaangamiza nafsi yako mwenyewe?

Abneri alishindwa kutumia mikono na miguu yake kama fursa iliyokuwa mbele yake kwa wakti ule, akafa kifo cha kipumbavu. Usiwe kama Abneri itumie fursa ya kuja kwa Yesu vema, fanya maamuzi ya kumwamini kama Bwana na mwokozi wako.
Baba yangu, mama yangu, kaka yangu, dada yangu, na rafiki yangu nakuomba kwa jina la Bwana usikubali kufa kifo cha kipumbavu, usikubali mauti ikukute kabla hujampa nafasi Yesu ya kutawala maisha yako. Mshahara wa dhambi ni mauti na baada ya kifo ni hukumu, je utakuwa mgeni wa nani siku ile?

Mungu ameniongoza nikuandikie ujumbe huu maana yeye hafurahii kifo cha mwenye dhambi, kwa sababu mtu anapokufa katika dhambi yake anatengwa na Mungu milele kwa sababu hakuna kuokoka baada ya kufa, ni hukumu tu tena ya kutisha. Siku ya kufa kwako ndiyo mwisho wa dunia kwako.

Usikubali kufa kifo cha kipumbavu , maana mpumbavu amesema hakuna Mungu katika moyo wake, bali wewe moyoni mwako mpe Mungu nafasi katika Jina la Yesu atawale maisha yako
Ikiwa umeguswa na ujumbe huu na unataka kuokoka bonyeza category ya wokovu utapata maelekezo ya nini cha kufanya.

Mwl Patrick Samson Sanga 
0755816800

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...