Monday, October 15, 2012

Mshindi wa Bongo Star Search 2009 Paschal Cassian, aelezea namna alivyokataa kujiunga na Freemason baada ya kufuatwa



“Nimekuwa maskini baada ya Freemason kunifilisi na kuniletea mabalaa mengi katika familia yangu.” Hivyo ndivyo anavyoanza kuzungumza Mshindi wa Bongo Star Search (BSS)mwaka 2009 Paschal Cassian.Cassian ambaye ni muimbaji wa muziki wa injili, anaeleza mkasa mzima kuwa baada ya kutoka BSS alipigiwa simu na watu waliomtaka akutane nao ili wazungumze.Anasema alionana na watu hao na katika vikao vyao, ndipo walipomueleza azma ya kumtaka kujiunga na Freemason.

Anasema, alikaa vikao na hao na kufika eneo ambalo hukutana na ambapo alipokutana na Watanzania wengi wakiwemo wacheza filamu, wachungaji na manabii.Anasema alipewa mikataba mbalimbali na alitakiwa kutoa kafara wazazi wake ndipo alikataa.Kwa mujibu wa Cassian, walimpatia nafasi ya kuchagua kitu anachotaka kutoka nacho ambacho kitampa umaarufu, lakini sharti likiwa kuua wazazi wake ndipo alipokataa.

Madaam Ritha akikata utepe wakati wa uzinduzi wa album ya Gospel ya Paschal Cassian.Madaam Ritha alitoa kiasi cha shillingi Million 10 ili kufanikisha malengo ya Cassian
Anasema kama angekubali angeingizwa katika chumba maalum alichooneshwa ili kufanya kafara hizo.Cassian anasema, anamjua Mungu na anamuamini na kama isingekuwa hivyo asingeweza kutoa siri za Freemason kwani ukisema siri zao kwa ujasiri hawakudhuru, lakini ukionesha hofu watafanya hivyo.

Anasema baada ya kukataa kutoa kafara alivamiwa mara nne katika studio yake aliyoifungua iliyokuwa ikiitwa Matunguri Fleva akiibiwa vitu vyenye thamani ya sh milioni 12 na yeye kupigwa mara nyingi hata kufikia hatua ya kulazwa mara kwa mara tena akiwa hoi.Anasema, kitu ambacho hatasahau ni matukio ya mara kwa mara ikiwemo kukumbwa na mafuriko na kupoteza vitu vyote alivyonunua na vingine maji yaliviondoa vitu vyote vya ndani na familia yake ilisaidiwa na watu kuiokoa.

Matukio anayoyapata anasema yanatokana na yeye kuachana na Freemason.“Wanakuja kiroho na wakikushidwa wanakuja kimwili kwani wanakuwa na watu wengi, malengo yao ni kukamata dunia nzima na wanawawezesha kifedha huku wachungaji wakiwawezesha nguvu za kufanya miujiza kwa baadhi yao.

“Wapo watu wengi, wachungaji, watu maarufu na marafiki zangu wapo na wengine waliokuwa washiriki Bongo Star wana magari kwasasa yaani watu wanaibuka tu na utajiri usiofahamika wala kueleweka.“Unapatiwa nguvu hata za miujiza kutoka kwao kwani wao wanauwezo wa shetani kuwatambua kwa nembo zao,” anasema.Anasema kuwa ujio wa filamu yake mpya itafunua mambo yote ya Freemason kwani yeye alishajiunga na watu hao.

Cassian anasema, filamu yake itakuwa tofauti kwani itahusiana na maisha ya watu wa ndani na mambo aliyokutana nayo huko ikiwa ni pamoja na wachungaji walioko Freemason na masupastaa.Cassian aliyezaliwa miaka 24 iliyopita mkoani Mwanza,Wilaya ya Kwimba, anasema kabila lake ni mMsukuma na katika familia yao, wapo watoto wengi sana zaidi ya 100 kwani baba yake ameoa wake wengi sana, lakini kwa mama yake ni mtoto wa mwisho kati ya watoto nane.

Martha Mwaipaja akiimba wakati wa uzinduzi wa album ya Paschal Cassian iitwayo Yasamehe Bure katika maeneo ya uwanja wa Fisi jijini Dar es salaa.Kwa mujibu wa Cassian moja ya malengo yake ni kukusanya Milion 30 zitakazotumika kuwasaidia kina dada wanaofanya biashara ya kuuza miili yao.

Kuhusu harakati za uimbaji, anasema alizianzia shuleni baada ya hapo anasema kuwa alienda kusoma muziki Uganda kwa miaka miaka miwili na kurudi jijini Mwanza kwaajili ya kufundisha kwaya mbalimbali za mjini humo.Kutokana na kutaka kujulikana ulimwenguni, ndipo akajiunga katika mashindano ya kutafuta vipaji yaitwayo bongo Star Search kwa mara ya kwanza na kuibuka mshindi.Anasema kuwa, alikuwa muumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato kabla hajaokoka na awali alikuwa muislam akiitwa Mohamed.

Akiwaelezea waimbaji wa injili anasema: “Waimbaji wa injili wengi wananichukia kwa mtindo wangu hasa waliotangulia waimbaji wengi hawana roho ya Mungu kwani kukupokea ni ngumu na hata kukuelekeza pia ni ngumu,” anasema. Anaendelea kusema kuwa, mwimbaji aliyeonesha ushirikiano wakati anatoka BSS ni Bony Mwaitege ambaye aliwahi kumpa ushauri.

Pia anadokeza kuwa amekuwa akisikia kwa watu kuwa Mwaitege analalamika kuiga mtindo wake wa uimbaji, lakini haamini jambo hilo kwani Mwaitege ndiye amekuwa mshauri wake katika uimbaji.

Akiizungumzia albamu yake mpya anasema yenye nyimbo nane, ikiwemo ‘Wasamehe bure iliyobeba albamu hiyo, lakini pia kuna nyimbo inayokamata mashabiki inayoitwa ‘Chuki ya nini’? Anasema, ameimba huo kwa sababu haoni kwanini wanachukiana wakati wote wanafanya huduma ya kumtumikia Mungu.

Albamu hiyo anasema amerekodi katika studio ya Feature Sound japo alishatapeliwa na baadhi ya mameneja hali iliyofanya aamue kusimama yeye kama yeye.Kuhusu ushauri wake kwa waimbaji wenzake, ni kutiana moyo hasa waimbaji wakubwa kwani wao wametangulia wasifanye muziki kama pesa, vipaji ni vingi ikiwemo kuacha visingizio vya kutowapa tafu chipukizi.

Paschal Cassian enzi za Bongo star search 2009
Akiwaasa wanamuziki wengine wanaoingia kwenye Gospel Music Cassian alisema“Watu wasije kwenye nyimbo kwa ajili ya pesa kwani huu ni wito na kuna changamoto nyingi sana, wasitarajie kupata pesa kwa haraka bali wajipange kimungu zaidi na wajitoe katika roho.

Cassian ameoa na ana watoto wawili Ritha na Anitha huku akitaja mafanikio aliyoyapata ni kumjengea mama yake nyumba. Zaidi ya hilo amejenga nyumba yake kwa milioni 18, iliyopo jijini Mwanza pia akimiliki studio huku akifahamika ndani na nje ya Tanzania.Anasema, amefahamiana na viongozi mbalimbali kiasi kwamba anaingia sehemu yeyote na kusikilizwa shida yake akisema yote hayo ni baada ya kukutana na Madam Ritha.

Na  Happiness Mnale

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...