KATIKA
miaka ya nyuma muziki wa Injili ulidharaulika sana na mtu alipoonekana akiimba
muziki huo alionekana kama kituko kwa sababu hakuna aliyekuwa anaguswa na
nyimbo hizo.si kwamba kipindi hicho hapakuwa na waimbaji wazuri wa muziki huo,
la hasha walikuwepo tena waliokuwa wanafanya vizuri pengine kuliko waimbaji wa
leo wanaoimba nyimbo za Injili.
Katika
miaka hiyo kulikuwa na waimbaji kama Ephraim Mwansasu, Faustine Munishi, Mungu
Four, Ency Mwalukasa, Jeniffer Mgendi na baadaye akajitokeza mwimbaji kama
Cosmas Chidumule aliyekuwa anapiga muziki wa dunia kabla hajageuzia kibao
kwenye nyimbo za injili.
Miaka
hiyo ilikuwa ni mara moja sana kusikia muziki wa injili ukipigwa katika kumbi
za starehe kama baa, kwenye harusi na mahali pengine kwenye starehe.
Lakini
leo hii upepo umebadilika ndivyo alivyoanza kusema mwanamuziki mahiri wa muziki
wa injili nchini, David Robert, aliyeibuka katika anga la muziki huo mwaka 2002
na albamu ya Baba.
Katika
albamu hiyo Robert ambaye ana sauti nzito alishirikiana vema na Gama pamoja na Godwin
Gondwe mtangazaji wa ITV ambaye naye ana sauti ya zege au sauti nzito lakini
yenye mvuto sana na kuifanya albamu hiyo kuwa na mvuto wa kipekee na kuweka
imara katika anga la muziki huo.
David Mwamsojo Robert |
Albamu
hiyo iliyokuwa na nyimbo kumi iliwashika wengi na kila mpenzi wa nyimbo za
injili kupenda kusikiliza nyimbo zilizokuwemo. Baadhi ya nyimbo zilizokuwamo
katika albamu hiyo ni Baba, Niongoze, Ngulujangu iliyoimbwa kwa kinyakyusa na
nyinginezo.
Kufanya
vizuri sokoni kwa albamu hiyo kulikuwa kama kumemtoa kimasomaso Robert kwani
mwaka 2003 aliingia studio na kufyatua albamu ya pili inayojulikana kwa jina la
Kiganjani pa Mungu.
Albamu hiyo ambayo nayo ilibahatika nayo kufanya vyema
katika tasnia ya injili na hivyo ikamlazimu Robert kurekodi video ambayo nayo
ilibamba.
Albamu
yake ya tatu ni Adui yangu ilikuwa na nyimbo nane, hakuna asiyejua kila kitu
kinachotengezwa kwa ubora, hutumia gharama kubwa kukikamilisha.Hata hivyo
Robert alikaa na kutafari, kwa makini jinsi gani anaweza kurekodi video ambayo
inaweza kuwa tofauti na video zilizotangulia. Jibu lake lilionekana kuwa ni
kujiweka sawa katika fungu la fedha.
Robert
aliamua kuzichambua nyimbo zilizo katika albamu hizo mbili na kufanikiwa
kurekodi albamu moja aliyoipa jina la 'The Best Of David Robert'.
Mwanamuziki
huyo anaeleza kuwa albamu hiyo ilirekodiwa katika mandhari ya kuvutia na
mtaalamu wa masuala ya filamu kutoka nchini Ujerumani Daniel Uphaus kwa
kushirikiana na Sye ambaye ni mtaalamu wa kuongoza filamu.
David Robert |
Wataalamu hao
waliirekodi kwa makini albamu hiyo hali iliyopelekea kukubalika katika soko la
kimataifa, ambapo tayari vituo vya Chanel O na Mtv Base waliiomba kwa ajili ya
kuirusha katika runinga zao.Ubora
wa albamu hiyo ya The Best of David Robert umetokana na maandalizi ya miaka
mitatu aliyoyafanya kabla ya kuchukua uamuzi wa kuingia studio na kutoa kitu
hicho ambacho kinamvuto mkubwa.
Kukamilika
kwa albamu hiyo kulichukua miezi minne na baada ya kurekodiwa aliipeleka kwa
wataalamu wengine kabla ya kuingia sokoni. Katika kuhakikisha albamu hiyo
inakuwa tofauti na albamu nyingine hasa za muziki wa injili nchini, Robert
alisafiri mikoa mbalimbali kwa ajili ya kupata picha nzuri kutokana na ujumbe
wa nyimbo husika.
Mikoa
aliyofanikiwa kwenda kurekodi albamu hiyo ni Morogoro, Iringa, Arusha, Moshi,
Pwani na Dar es Salaam.
Robert
aliyezaliwa Machi 18, mwaka 1978 Mabatini, jijini Mbeya anasema kuwa huduma ya
uimbaji alianza tangu akiwa mtoto, alipokuwa shuleni, ambapo aliifanya kwa
nguvu zote kwa kutembelea shule mbalimbali kwa lengo la kutoa injili kwa njia
ya nyimbo hiyo ikiwa mwaka 1998 wakati akisoma Shule ya Sekondari ya Jitegemee,
jijini Dar es Salaam.
Pamoja
na kuipenda huduma hiyo wapo waimbaji waliomvutia akiwamo Mchungaji Ephraim
Mwansasu, Mchungaji Daniel Richard Mwansumbi na Cosmas Chidumule hao ndio
waliompa hamasa kubwa Robert kujikita katika anga la muziki huo wa injili.Waimbaji
hao ndio walikuwa wakimvutia kutokana na sauti zao kuwa nzuri pamoja na ujumbe
wa nyimbo uliokuwamo ndani ya nyimbo zao na mitindo waliyokuwa wakiitumia.
Kwa
upande wa mafanikio kupitia muziki huo wa Injili Robert anaseama: “Nimefanikiwa
kujenga nyumba nzuri ya kisasa, kumiliki gari lakini mafanikio mengine ni
pamoja na kupata mtandao mzuri wa marafiki ndani na nje ya nchi na kuwa na
miradi mbalimbali inayonisaidia kuendesha maisha yangu ya kila siku,” anasema.
Kwa
upande wa changamoto, mwanamuziki huyo anasema kuwa anakabiliwa na mtaji mdogo
wa kuitangaza huduma ya Mungu ndani na nje ya nchi, kutumia gharama kubwa katika
kurekodi albamu na mwisho wa siku anajikuta mfukoni hana kitu, wapiga picha
kuchelewesha kazi, ambapo kama alikuambia anakupa baada ya wiki mbili basi
atakupa baada ya miezi miwili, masta hazina ubora na teknolojia kuwa chini,
isiyokidhi ubora wa kimataifa na matatizo ya umeme usio wa kudumu pia huchangia
kazi kusuasua.
Anasema
kuwa anakerwa sana na waimbaji wanaokimbilia katika muziki huo kwa
kuangalia
masilahi ya pesa zaidi kuliko huduma.Ambapo watu wengi wamekuwa wakijikuta
wanashindwa kufanya vema kazi ya Mungu pindi wanachokitarajia kinanapokosekana.
Mwimbaji
huyo mwenye mke na mtoto mmoja anasema wazi bila kificho kuwa muimbaji mwenzake
anayetamba na albamu yake mpya ya ‘Nipe macho’, Christina Shusho, ndiye
anayemvutia zaidi kutokana na nyimbo zake kuwa na ujumbe mzito ambao mara
nyingi nyimbo hizo hugusa maisha anayopitia.
Kwa
upande wa matarajio anasema kuwa anatamani kufanya mapinduzi makubwa katika
muziki wa injili kwa siku za usoni. Mbali na hilo anatamani kuona muziki wa
injili ukisambaa kimataifa zaidi na waimbaji wazalishe kazi zenye ubora wa hali
ya juu.
Na Happiness Mnale
0712
00 35 39
No comments:
Post a Comment