Biblia katika kitabu cha
Mwanzo 2:18 inasema ‘Bwana
Mungu akasema, si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana
naye’. Ni kusudi na mpango wa Mungu watu waoe na kuoana. Hii ni
kwa sababu kufanikiwa kwa kusudi la Mungu duniani kunategemea ndoa au wanandoa
pia. Naam kwa Mungu ni muhimu sana kujua nani anakuwa mwenzi wako wa maisha
tegemeana na kusudi lake la kukuumba.
Tunapoenda kufunga mwaka
nimesikia ndani kuweka ujumbe huu kwenye blog hii nikiamini utawafaa wengi.
Jambo la msingi ambalo nataka ulipate ni kuhusu uhusiano uliopo kati ya ‘uhuru’ wa
kumtumikia Mungu na ndoa yako. Pengine si wengi wanaojua
umuhimu wa mahusiano mzuri baina yao kama wanandoa na kumtumikia Mungu. Naam
ndiyo maana kuna ujumbe huu kwa ajili yako.
Watumishi wengi katika nyakati
za leo hawajawapa heshima na nafasi ambayo wenzi wao wanaistahili. Baadhi ya
wanaume wameona kupata mke ni sehemu ya kukamilisha sifa za utumishi wao kama
wanandoa bila kujua kwa nini ameunganishwa na huyo mwenzi wake. Wengine
wamekuwa wakiwapuuza wake au waume zao na bado madhabahuni wanalihubiri neno.
Na kuna baadhi yao hawana upendo kwa wake zao, wake nao si watiifu kwa
waume zao, ni watu wa kugombana, wenye uchungu ndani yao nk, naam bila
kutengeneza au kumaliza tofauti zao hizo utawakuta madhabahuni wakihudumu
kwa raha kabisa. Je, jambo hili ni sahihi kweli? Je ni jambo la kumpendeza
Bwana?
Fahamu kwamba ‘uhuru wako katika
kumtumikia Mungu kwenye nafasi aliyokupa katika mwili wake, ipo kwa mwenzi wako
wa maisha’. Ilikuwa Desemba 28, 2010, Bwana Yesu
aliponifundisha jambo hili. Naam uhuru wako wa kumtumikia Mungu upo kwa
mke/mume wako. Hivyo
kama mahusiano yako na mwenzi wako si mazuri huwezi kutumika katika mapenzi
yake. Naam uhuru wa wewe kusikia na kupokea kutoka kwa Mungu unategemea sana
mahusiano yako na mwenzi wako.
Nilipofuatilia tafsiri ya neno
hili uhuru (freedom) niligundua zipo tafsiri nyingi lakini nikachukua hizi tatu
kwa kuwa zinaendana na ujumbe huu. Tafsiri moja wapo ya ‘Oxford
dictionary’ inasema uhuru ina maana ya ‘special privilege or right of
access’. Na tafsiri ya neno hilo kutoka katika ‘Encarta dictionary’ ni
‘right to use or occupy a space’ na pia tafsiri nyingine ni ‘ease of
movement’.
Naam mahusiano yako na mwenzi
wako yanapokwa mazuri jambo hili linakupa haki, kibali, nafasi na mpenyo wa
kumtumika Mungu katika kiwango alichokusudia na zaidi katika mapenzi yake.
Jambo
hili linakupa mpenyo wa kusikia, kuhoji na kusemezana na Mungu juu ya kile
ambacho anataka uwafundishe watoto wake ama ukiwa madhabahuni, au kwa njia ya
kuandika, kushuhudia nk. Naam kwa hiyo mahusiano mazuri kati yako na mwenzi
wako ni ufunguo wa wewe kumtumika Mungu.
Si hivyo tu bali mahusiano
yako na mwenza wako yanapokuwa mazuri utapata wepesi wa kutembea na kutumika
katika kusudi la Mungu. Naam ndivyo unavyopata haki ya kutumia kila ambacho Mungu
ameweka ndani yako kwa utukufu wake, naam ndivyo unavyokuwa na nguvu ya utawala
kwenye nafasi na eneo lako la utumishi katika ulimwengu wa roho.Biblia inasema katika 1Petro
3:7 ‘Kadhalika
ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo
kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu
kusizuiliwe’.
Naamini umeona kile kipengele
cha mwisho kinavyosema. Hii ina maana kama mwanaume atashindwa kukaa na mke
wake kwa akili na kumpa heshima, maombi yake yatazuiliwa. Sasa fikiri mwanaume
huyu ni mtumishi yaani Mchungaji, Mwalimu, Nabii nk nini kitatokea kwa wale
anaowachunga au kuwahudumia? Naam
mahusiano yako na mwenzi wako ni ya maana sana kama unataka kutumika katika
mapenzi ya Mungu. Mahusiano mazuri baina yenu yanaleta mawasiliano mazuri baina
yako kama Mtumishi na Mungu wako. Hivyo msingi wa mawasiliano mazuri na Mungu
wako, upo kwa mwenzi wako.
Ni vizuri ukafahamu kwamba
bila kuwa na mahusinao mazuri na mwenzi wako wa maisha, utumishi wako ni bure.
Naam uhuru wako katika kumtumika Mungu unategemea uhusiano wako na mwenzi wako.
Si rahisi kwa Mungu kusema na wewe kama mahusiano yako na mwenzi wako si
mazuri, matokeo yake utawasikizisha/hubiri/fundisha watu mawazo yako na pengine
ya adui, zaidi utahudumu kwa mazoea bila uwepo wa Bwana, au chini ya kiwango
cha upako uliokusudiwa, tena ni kwa sababu Mungu anawaonea huruma watu wake.
Jifunze kufanya tathimini ya
mahusiano yako na mwenzi wako mara kwa mara, na kuhakikisha unayaboresha, naam
jambo hili ni muhimu sana kwenu binafsi na zaidi kwa Mungu ili kupata uhuru wa
kusikia kutoka kwake kila wakati kwa ajili yenu na wale ambao amekupa
kuwahudumia.Nakutakia utumishi mwema
katika nafasi yako pamoja na mwenzi wako, mwenzi wako ni wa muhimu sana, mpe
nafasi yake, utaona mabadiliko kwenye utumishi wako.
Na Mwl Patrik Sanga
0755816800
No comments:
Post a Comment