Saturday, October 13, 2012

Vurugu za jana katika eneo la Mbagala baada ya mtoto kudaiwa kuinajisi Quraani

Vurugu za Mbagala
Vurugu zimeibuka jana katika eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam na kusababisha kuvunjwa kwa makanisa matatu kutokana na watu wanaodaiwa kuwa waumini wa Kiislamu kukosa uvumilivu baada ya kuelezwa kuwa mtoto mmoja amekojolea kitabu kitakatifu cha Waislamu, Qur'an.

Aidha vurugu hizo zilisababisha kuvunjwa kwa vioo vya magari, madirisha ya makanisa pamoja na kuibwa kwa vifaa vya kwaya katika makanisa hayo ambayo ni ya Anglikana, Wasabato na Pentekoste.

Akielezea tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema tukio hilo lilitokana na kuwepo kwa taarifa za mtoto mmoja wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) kukojolea kitabu hicho wakati alipokuwa akitaniana na mwenzake mwenye umri wa miaka 12 (jina linahifadhiwa) juu ya maajabu ya kitabu hicho.
Alisema tukio la kukojolea kitabu hicho lilitokea Oktoba 10 katika eneo la Chamazi saa 10 jioni wakati watoto hao wakiwa katika ‘kijiwe’ chao cha kuchezea mpira, ambapo hukutana hapo mara kwa mara kwani ni marafiki.

"Siku hiyo kijana mmoja alikuwa amekwenda madrasa na akawa amerudi na kitabu cha Kurani ambapo alimkuta rafiki yake akicheza mpira katika eneo hilo ambapo kama kawaida yao walianza kulumbana kwa mambo mbalimbali," alisema Kova na kuongeza.
"Baadaye malumbano yao yalifikia kwenye Kurani ambapo aliyekuwa ametoka madrasa alimwambia mwenzake ukikojolea kitabu hiki utageuka kuwa panya au nyoka…mwenzie alibisha na hatimaye akathubutu kukikojolea," alisema Kova na kuongeza kuwa, aliyefanya kitendo hicho hakudhurika.

Hata hivyo, alisema baada ya tukio hilo mtoto ambaye Kurani yake ilikojolewa alikwenda kushitaki kwa baba yake ambapo wazazi wa pande zote mbili walikutana katika kulipatia suluhu jambo hilo na kabla maafikiano hayajafikiwa, baba huyo aliamua kulipeleka polisi.
"Alipofika katika Kituo cha Polisi Chamazi, askari waliokuwa pale walimwelekeza kulipeleka kituo cha Mbagala ambapo alipofika alitakiwa kuandika maelezo ndipo makundi tofauti tofauti ya waislamu yalianza kuingia kituoni hapo wakitaka kuelezwa zaidi kuhusu tukio hilo na mtoto aliyehusika," alisema Kova.

Aidha alisema kundi lingine lilikosa uvumilivu na kuanza kusababisha vurugu katika eneo hilo kwa kuanza kufanya fujo, kuvunja vioo na kupanga mawe jambo ambalo lilisababisha kuvunjwa kwa kioo cha gari la OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya).
"Hata walipotangaziwa watoke katika eneo hilo wapo waliokubali na wengine walikaidi huku wakitaka wamchukue huyo mtoto aliyehusika ndipo polisi ilipolipua mabomu ya machozi na kuwasambaratisha waumini hao wengine wakielekea makanisani na kufanya uhalifu huo.

Kamanda Kova alisema katika upelelezi wa awali wamebaini kuwa tukio hilo ni la kitoto lisilokuwa na njama zozote za kutumwa kwa kijana huyo na kuwataka waumini hao kuiacha polisi kufanya kazi yake.

Kwa upande wake Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema ni vyema waislamu kufahamu kuwa kudhuru wengine huo si uislamu na kwamba labda kikundi kilichohusika kina mambo mengine nyuma ya pazia.
Alisema tukio hilo halihitaji jazba na kwamba hata katika Uislamu kuna mistari inayosisitiza Waislamu kutizama jambo linalotokea wakibainisha umri na mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema hayo yalikuwa ni mabishano ya watoto wenye umri mdogo na kwamba si kitendo cha kiungwana wala cha maendeleo kwa waumini hao kuzua vurugu.

"Chokochoko za kidini mwisho wake si mzuri, tuwe na subira na tusifikie mahali pa kukosa uvumilivu na kufikia hatua kama hiyo… watakaobainika kusababisha uchochezi na chuki vyombo vya dola viwachukulie hatua stahiki," alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...