Thursday, July 5, 2012

‘Arusha wasema Ukimya wa Wakristo si ujinga au woga wao’





TAMKO la Umoja wa Makanisa Jiji la Arusha na Kanda ya Kaskazini limedai ukimya wa kistaarabu unaoendelea kuonyeshwa na Wakristo nchini usitafsiriwe kama ni ujinga au woga.
Hayo yalibainika jana mjini hapa, wakati wa Kikao cha Umoja wa Makanisa jijini Arusha na Kanda ya Kaskazini juu ya vurugu na vitisho dhidi ya Wakristio na Ukristo nchini.

Tamko hilo lilikwenda mbali na kuilaumu Serikali kwa kushindwa kuchukua hatua zozote madhubuti kudhibiti hali hiyo isiendelee.Akisoma tamko hilo, Askofu wa Kanisa la Mennonite Arusha, Joseph Metorera, alisema kwa nyakati tofauti baadhi ya Waislamu kupitia mihadhara na baadhi ya vyombo vya habari wamekuwa wakitoa maneno ya uchochezi na kashfa dhidi ya Ukristo na Wakristo.

“Hali hii ya uchochezi na vitisho imekwenda mbali zaidi hadi kuingia katika uharibifu wa mali na kutishia uhai wa watu wa Mungu.“Angalia uchomaji wa Makanisa na uharibifu wa mali Zanzibar Mei 26, 27 na 28, mwaka huu. Kifo cha Mwinjilisti Mto wa Mbu Februari 24, Mwaka 2011,” alisema Askofu Metorera.

Alisema kusimamia sheria na taratibu za nchi ni wajibu wa Serikali, hivyo kunapoonekana baadhi ya makundi yakiendelea na harakati zao za kuvuruga amani na kusababisha hofu bila hatua zozote madhubuti kuchukuliwa kunaleta hisia kuwa baadhi ya viongozi wa Serikali wanakubaliana na hali hiyo.Alisoma tamko hilo kwa kubainisha kuwa haki na amani ni vitu visivyotenganishwa (Zaburi 85: 10b).

Alisema kwa sababu Serikali ndio yenye dhamana ya kuhakikisha haki inatendeka na inaonekana ikitendeka, “tunaitaka ichukue hatua stahiki kwa wakati dhidi ya wahusika wote kabla ya mambo kuharibika.

“Tunatoa wito kwa Wakristo wote nchini kusimama katika zamu zao, kumuomba Mungu aliye hai, kuutafuta uso wake bila kuchoka na kwamba kusudi lake likasimame katika yote,” alisema Askofu Metorera.Umoja huo unaundwa na Kanisa la Romani Catholic (RC), Kanisa la Pentecostal Tanzania (FPCT), Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanisa la Anglikana Tanzania (ACT), Kanisa la Babtist, Kanisa la Mennonite na Kanisa la African Inland Church (AIC).

Baadhi ya viongozi wa makanisa hayo waliohudhuria kikao hicho ni Mchungaji Willson Kimaro wa Pentecostal, Askofu Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikana, Joseph Moterera wa Kanisa la Mennonite.Wengine ni Aloyce Mabere wa AIC, Padri Tengesi, Askofu Thomas Laizer wa KKKT, Mchungaji Mathias Mushi wa KKKT ambaye ndiye Mwenyekiti wa Umoja huo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...