GAZETI LA
TUHUMA ZA KUNASWA NA FREEMASONS
Askofu Mwasota Avunja Ukimya
Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste nchini askofu David Mwasota amevunja ukimya wa tuhuma za kuwa amenaswa na kundi la FreeMasons.Akiongea na Gazeti la JIBU LA MAISHA Mchungaji Mwasota amesema “ Ndugu yangu haya ni Mahsambulizi, nimezushiwa mengi achilia mbali haya yaliyoandikwa na magazeti, jumbe zimesambazwa kwa watumishi wa Mungu (wachungaji) wakae mbali na mimi eti nimekuwa Freemason lakini haya yote ni mashambulizi tu”
Askofu David Mwasota akiwa na Mkewe |
Akaendelea kusema “ Nakwambia ukweli kutoka moyoni simjui hata kiongozi mmoja wa Freemasons wala sijui hata hekalu lao liko wapi, mimi nilikuwa nafundisha kanisani nikawaonya wapentekoste wakae mbali na watu wasiowajua kwa kuwa wengine ni waabudu shetani.
Nikatoa mfano nikasema niliwahi hudhuria semina fulani baada ya kukamilika nilipewa NISHANI ambayo baadaye nilikuja kubaini kuwa ilikuwa na nembo nisizozijua nikaamua kuitupa, Jambo la kushangaza nikaona waandishi wakaamua kunimaliza.
Wewe ndio mwandishi wa kwanza kuja kuonana nami uso kwa uso na kulizungumza suala hili kwa kina, wengine walinipigia simu tu nikawaambia waje ofisini sikuwaona lakini nikashitukia habari kubwa imeandikwa hii inaniuma sana alisema mtumishi Mwasota.
Mchungaji asema tunahitaji M4C(Movement for Change) ya Kiroho
Wakristo wote nchini wametakiwa kufanya mabadiliko katika ulimwengu wa ROHO ili nchi iweze kumgeukia Kristo, hayo yalibainishwa na wiki iliyopita ma mchungaji Joseph Marwa wa kanisa la TAG Uwanja wa ndege kisiwani Zanzibar wakati akihubiri kwenye kongamano la mpenyo la siku tano lililofanyika katika kanisa la TAG Sinza Refuge Centre.
Mch Marwa alisema “ watumishi wa Mungu wakati wa Biblia walipoona maovu yamezidi waliamua kuleta vuguvugu la mabadiliko katika ulimwengu wa Roho na lilileta matokeo Halisi kiasi cha kusababisha wimbi kubwa la uamsho.Sambamba na hilo mtumishi huyo alisema Mungu anatafuta mtu mmoja atakayesimama kuhakikisha kwamba Tanzania inapata mageuzi ya kweli kwenye ulimwengu wa ROHO na si watu wanaositasita kwenye njia mbili.
Kanisa la Tanzania lapeleka Injili Msumbiji
Kanisa la TAG Ubungo(Ubungo Christian Centre) limegusa ufalme wa Mungu kwa kipekee kwa kukubali kwenda pamoja na mmishonari Teddy Komba wa Tanzania nchini Msumbiji kutekeleza agizo kuu la Yesu la kwenda dunianai kote kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wake.Mch Kiongozi wa Ubungo Christian Centre Rev Paul Mulokozi amesema hayo katika Ibada ya kumuaga mmishonari huyo iliyofanyika kanisani hapo wiki iliyopita na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu.
Ndondoo zilizomo ndani ya Jibu la Maisha
†Mchungaji asisitiza utoaji wa Maoni ya katiba
†Wanawake wataka wanaume kuhudhuria mafunzo ya ndoa
†Ni nani ambao hawataonja Mauti mpaka wauone kwanza Ufalma wa Mungu?
†Jinsi ya Kufundisha Neno kwa ufanisi
†Lini wakina Mrisho Ngassa watavaa viatu vya wanyama!
Gazeti la
Nyakati
Kakobe akataa Usuluhishi
August 30 Kesi inayomkabili Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship Askofu Zacharia Kakobe ilisikilizwa na Jaji August Shangwa.Katika kesi hiyo waliokuwa wachungaji wa kanisa hilo wapatao wanne walifungua kesi mahakamani wakidai Askofu Kakobe ametumia vibaya fedha za Kanisa hilo jumla ya shilingi bilioni 14.Baada ya kesi hiyo kufunguliwa askofu Kakobe kupitia wakili wake Miriam Majamba aliweka pingamizi mahakamani hapo akitaka kesi hiyo itupiliwe mbali kwa madai kuwa wanaomshtaki sio watumishi wa Kanisa hilo kwani alishawafukuza.
Askofu Zacharia Kakobe |
Julai 17 mwaka huu Jaji Shangwa alitaka suala hilo limalizwe kwa usuluhishi hivyo aliwataka walalamikaji siku ya August 30/2012 walete maaskofu watakaoshirikiana na jaji huyo katika kufanya usuluhishi na akatoa angalizo maaskofu hao ni lazima wawe na maelewano mazuri mtumishi Kakobe.Walalamikaji hao waliwaomba Askofu Philemon Tibanenason(KLPT),Katibu mkuu wa baraza la makanisa ya kipentekoste nchini Askofu David Mwasota na askofu wa kanisa la Menonite nchini stephen Man’gana.
Mnamo August 30 Askofu mwasota alifika mahakamani hapo huku Askofu Tibanenason na Man’gana wakitoa udhuru.Jaji shangwa alimuuliza wakili wa mtuhumiwa kwa nini Askofu Kakobe hajafika Mahakamani na wakili huyo alijibu kuwa hakufika kwa kuwa haoni Jambo la Kusuluhisha.Baada ya majibu hayo Jaji huyo aliwageukia walalamikaji na kuwaambia nadhani mmesikia majibu ya Kakobe haoni sababu ya Usuluhishi.Kwa mujibu wa Jaji Shangwa atachokifanya sasa ni kulirudisha jalada la kesi hiyo kwa jaji mfawidhi ili apange lipangiwe upya jaji atakayeanza kuzishindanisha pande hizo.
Kanisa linalopinga wautoaji Sadaka lakosa waumini
Kanisa la “Waabuduo Halisi” lenye makazi yake Kigamboni mjimwema jijini Dar es Salaam limekuwa na washirika watano toka kanisa hilo lianzishwe miezi sita iliyopita.Matarajio ya kanisa hilo juu ya ufunuo wa kiongozi wa kanisa hilo kuwa waumini wasitoe sadaka ungewavutia watu wengi yamakuwa kinyume toka kanisa hilo lianzishwe November mosi mwaka jana.
Akiongea na gazeti la Nyakati msemaji wa kanisa hilo mtendakazi Melkizedeki Marwa alisema hali hiyo imetokana na mambo mawili, Kwanza kuwepo na upinzani kutoka watumishi wanaodai huduma yake imegusa huduma au makanisa wanayoyaongoza, pili kanisa lake limesajili idadi hiyo ya waumini katika kipindi hicho kwa kuwa kanisa lao halitaki waumini wa ushabiki bali linataka waumini wanaomaanisha.
Njia nyembamba Apata Jiko
→ Ni yule mtumishi anayehubiri mitaani hususani Posta jijini Dar es salaam
Baada ya kuishi kwa muda mrefu maisha ya Ubachela, mtumishi wa Mungu Lucas Paul Nchimbi maarufu kama Njia nyembamba amefunga ndoa na kuwataka vijana ambao hawajaoa au kuolewa kutokata tamaa katika kusubiri mwenzi kutoka kwa Bwana.Tofauti na ilivyozoeleka kuwa ndoa hufungwa kanisani, ndoa ya njia nyembamba ilifungwa nyumbani kwa Bi Harusi Kigamboni Eneo la msikitini mnamo juni 24 Mwaka huu na ndoa ilifungwa na Askofu Edmund Kiame wa kanisa na Udugu.
Njia nyembamba alipoulizwa kwa nini amefunga ndoa nyumbani kwa bi harusi alisema huo ni ufunuo “Mungu alinifunulia akanieleza ndoa hiyo tuifungie nyumbani kwa mke wangu ili tuwahubirie waliokata tamaa waweze kuokoka,tulitumia tukio hilo ili tuwafundishe wengine juu ya uvumilivu na kusubiri”.Kwa sasa njia nyembamba ana umri wa miaka 62 na aliokoka tangu mwaka 1980.
Ndondoo kutoka Nyakati
†Wahesabu sensa wahofia Simba
†Vita vya Kiroho
†Mbinu za Kuwa mhubiri mzuri
†Maombi ya kinamama yamnasa Sangoma wa kike Dodoma
No comments:
Post a Comment