Sunday, September 9, 2012

Sunday Sermon:Kwa Nini Mungu Anataka Watu Wake Wawe Matajiri?



Ile mwanzo 12:2 neno inasema “nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako, nawe uwe baraka”. Na Mwanzo 13:2 inasema“Naye Abramu alikuwa ni tajiri  kwa mifugo, na kwa dhahabu”.

Hapa tunaona jinsi Mungu anavyoweka ahadi ya kumbariki Abramu na kumfanya kuwa taifa kubwa. Kwenye sura ya 13 tunaona tayari Mungu ameshaanza kumbariki inasema alikuwa tajiri kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Bado katika 3Yohana 1:2 Mungu anasema “mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo .


Mpaka hapa tunaona kabisa ni mpango wa Mungu kutufanikisha katika mambo yote, hii ni pamoja na mafanikio ya kifedha. Na utajiri ambao Mungu anataka tuwe nao sio utajiri mdogo .Sasa swali ni kwamba kwa nini Mungu anataka tuwe matajiri? Maana kuwa tajiri bila kujua sababu za kuwa na huo utajiri utashindwa kujizuia kwenye matumizi mabovu ya huo utajiri (Fedha). Huenda zipo sababu nyingi, lakini mimi nataka nikuonyeshe sababu tatu za kibibilia.

Sababu ya kwanza , kulinda mawazo na mikakati ya Mungu kwa watu wake.
Yeremia 29:11. Mhubiri 7:12 “Kwa maana hekima ni ulinzi kama vile fedha ilivyo ulinzi na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliyo nayo” Mithali 18:11 “ Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake .
Kwenye kitabu cha Yeremia 29:11 

Mungu anasema nayajua mawazo ninayowawazia, si mawazo mabaya, ni mawazo ya amani ………..Sasa ukiunganisha mawazo ya mhubiri 7:12 na mithali 18:11 utupata sentensi hii. Mungu anapokupa utajiri (fedha), anakutajirisha ili kulinda mawazo (mipango) na mikakati ya Mungu ambayo anakupa kabla ya kukupa hizo pesa kwa watu wake. Fedha yoyote ambayo Mungu anaileta mikononi kwako kumbe ina makusudi, mipango ya Mungu ndani yake.


Mungu anayo mipango na njia za kuwafanikisha watu wake kiuchumi, kimwili, kibiashara, kimaisha  n.k. sasa hii mipango inalindwa na nguvu ya fedha. Maana kama watu wake watakuwa masikini basi mipango aliyo nayo juu ya kanisa, familia, nchi n.k. basi si tu haitatekelezeka vizuri bali pia itanunuliwa na shetani kwa fedha yake. Hii ina maana Mungu anataka tuwe na nguvu ya kimaamuzi na ya utawala kwa yale anayotuagiza Mungu kwa sababu kwa fedha.

Sababu ya pili , Ili kuliimarisha agano lake.
kumbukumbu 8:18 Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri, ili ALIFANYE imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.
Hapa tunaona wazi kabisa kwamba Mungu anasema ninakupa huo utajiri ili kulifanya agano lake kuwa Imara. Je agano hili ni lipi? Yeremia 31:31 inasema “Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, …. Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaindika; nami nitakuwa Mungu kwao, nao watakuwa watu wangu.

Agano ambalo Mungu anataka uimarishe kwa fedha anayokupa ni la yeye kukaa na watu wake. Maana yake tumia fedha anayokupa kujenga na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Yesu na watu wake.Uhusiano wa Yesu kama mwokozi, Rafiki, mpanyaji, Bwana n.k kwa watu wake maana yake ni hii, tumia fedha kufanya jambo lolote maadamu una hakika litapelekea uhusiano wa mtu (watu) na Yesu kuimarika na jina la Yesu kutukuzwa. Na kwa sababu hiyo utukufu wa mwisho wa nyumba hii/agano hili utakuwa ni mkuu kuliko ule wa kwanza, Hagai 2:8

Sababu ya tatu, ili tukopeshe na sio kukopa .
Kumbukumbu la Torati 28:12 inasema Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri … Nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe .Sikiliza tumeshaona katika mithali 18:11 kwamba mali ya mtu tajiri ni mji wake wenye nguvu… kwa lugha nyepesi maana yake fedha ya mtu tajiri ni nguvu ya huyo mtu kwenye mji aliopo/ au ambao yupo. Kwa kuwa akopaye ni mtumwa wake akopeshaye, hivyo utakapokopesha maana yeke utakuwa na nguvu juu ya maamuzi na hisia za huyo au hao watu uliowakopesha.

kama tukibakia kukopa tutakuwa watumwa na kwa sababu hiyo ndiyo maana Mungu anatupa utajiri kwa mtu mmoja, familia, kanisa, nchi n.k
Naamini sehemu ya kwanza ya somo hili litakusaidia katika matumizi ya utajiri ambao Bwana Mungu amekupa.

Na.Mwl Patric Sanga

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...