Tuesday, September 4, 2012

Wachungaji wa Anglikan Mwanza wamkataa Askofu


Askofu mkuu wa Anglikan nchini Askofu Valentino Mokiwa
Wachungaji  24 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyaza (DVN) mkoani Mwanza wametoa tamko la kumkataa askofu wa kanisa hilo mkoani humu, Boniface Kwangu, kwa madai kuwa ni mshirikina, fisadi na analiendesha kanisa hilo kwa chuki na ubabe.

Katika tamko lao lililosomwa na Mchungaji Marco Iseke ndani ya Kanisa la Anglikana jijini Mwanza juzi Jumapili, wachungaji hao   wamemtaka Askofu Kwangu ajiuzulu wadhifa wake mara moja na kuikabidhi Dayosisi hiyo mikononi mwa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Valentino Mokiwa.

Wachungaji hao wamedai kuwa Askofu Kwangu ameonyesha kila dalili ya kwamba ni mshirikina, baada ya kuwataka wahudumu wa kanisa kuondoa zuria (carpet) lililokuwa madhabahuni kwa madai kwamba lilikuwa limewekewa hirizi.
Aidha, wamedai kuwa Askofu Kwangu amebadili taratibu za ibada za kanisa hilo na kuingiza ibada za kipentekoste na pia kuwaweka wakfu wachungaji ambao tayari wamewekwa wakfu na kutoa cheo cha u-canon kwa wachungaji pasipo kufuata utaratibu.

Mathalani, walidai kuwa Askofu Kwangu alimzawadia cheo cha u-canon mchungaji aliyekuwa anastaafu baada ya kukosa zawadi ya kumpatia.
Kuhusu ubadhirifu, walidai kuwa katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2010, askofu huyo ameuza magari matatu kwa ajili ya kugharimia safari yake ya kwenda kutalii Israel na katika mahubiri ya Mwakasege huko Morogoro na pia kumwezesha mkewe kwenda kutalii Korea Kusini.

Waliendelea kudai kuwa askofu huyo amekarabati nyumba anayoishi kwa Sh. milioni 60 wakati gharama halisi iliyoidhinishwa ni Sh. milioni 20.
Pamoja na mambo mengine walidai kuwa Askofu Kwangu amekuwa akienda benki kuchukua fedha bila idhini ya wazee wa kanisa kuu, na pia amekuwa akisubiri wazee wamalize kuhesabu pesa mara tu baada ya ibada na kuchukua fedha hizo na kuondoka nazo.

“Ana mpango wa kuuza nyumba za kanisa zilizopo mitaa ya Bwiru na Nela. Ameshindwa kuonyesha vyeti vya elimu ya shahada ya pili aliyodai kuwa amesoma,” wamedai katika tamko lao.
Waliongeza kuwa Askofu Kwangu ameharibu uhusiano wake na wachungaji kwa kuwaita wajinga, wasio na akili na kwamba hawajui kutafuta pesa.

“Askofu Boniface Kwangu ameshindwa kuiongoza Dayosisi ya Victoria Nyanza kwa kuwa amekosa sifa zinazoelezwa katika Timotheo 3:1-7 na Tito 1:7-9, sawa sawa na kanuni ya pili C ya Katiba ya Jimbo,” wamefafanua wachungaji hao.
Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia tuhumza hizo, Askofu Kwangu alisema kwamba hajaliona wala kukabidhiwa kiofisi kwa sababu yuko vijijini anakoendelea na shughuli za kidini.

“Niko vijijini kwa huduma, sijaliona hilo tamko kwa hiyo siwezi ku-comment (kusema) chochote, nikirudi nikaliona basi nitatoa clarification (ufafanuzi),” alisema Askofu Kwangu kwa ufupi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...