Sunday, September 9, 2012

Wachungaji wamtaka Rais Jakaya Kikwete achukue hatua


Rais Jakaya Kikwete
WACHUNGAJI wa makanisa ya kipentekoste wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kuacha kuwa kimya wakati huu ambapo taifa lipo katika majonzi na badala yake achukue hatua ya kuwawajibisha viongozi wakuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani kutokana na kushindwa kuiongoza wizara hiyo na kusababisha vifo vya raia wasio na hatia.

Wakizungumza jana na Tanzania Daima Jumapili, wachungaji hao walisema kuwa ni aibu kwa taifa ambalo limekuwa likihubiri amani na demokrasia likimwaga damu za watu wasiokuwa na hatia.

Mchungaji Onesmo Mwakyambo wa Kanisa la Agape RHEMA, lililopo mkoani Morogoro, alisema kuwa viongozi hao wameshindwa kujiwajibisha wao binafsi, hivyo kutokana na katiba kumpa mamlaka rais, anapaswa kuchukua hatua dhidi yao.
“Dhana ya uwajibikaji imeshindwa kufanyika hapa nchini hasa kwa viongozi wa sasa…tunakumbuka Rais wa awamu ya pili Ally Hassan Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani aliwajibika binafsi kutokana na kutokea kwa vifo, hivyo tunashangazwa na kitendo cha Waziri Emmanuel Nchimbi na naibu wake kuendelea kung’ang’ania madaraka,” alisema.

Alisema kuwa hatua ya kuendelea kulisifu taifa hili kuwa ni la amani haipaswi kuvumiliwa kwa kuwa polisi wamekuwa wakipindisha sheria kwa makusudi huku wakijiona kuwa wapo juu ya sheria.

Mchungaji Mwakyambo alisema kuwa hatua ya Rais Kikwete kuamua kuwa kimya na kushindwa kukemea vitendo hivyo sio tu kunajenga taswira mbaya kwa Watanzania bali pia hata yeye binafsi anachafuka kutokana na matukio hayo ya mauaji, likiwemo la mwandishi wa habari wa kituo cha Televisheni ya Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi aliyeuawa mkoani Iringa mwanzoni mwa wiki hii.

“Nchi hii haipo kwa ajili ya kundi fulani bali kwa ajili ya Watanzania wote, hivyo hatua ya rais kushindwa kuzungumza neno juu ya matukio hayo jamii inamshangaa na haimwelewi hasa kutokana na yeye kuwa ndiye kiongozi mkuu wa serikali,” alisema.
Alisema serikali haiwezi kuwadanganya Watanzania katika mauaji hayo yanayoonekana kufanywa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya maslai ya watu wachache.

Huku akinukuu kifungu cha maandiko matakatifu ya Biblia Mithali 14:34 inayosema haki uinua taifa bali dhambi ni aibu kwa watu wote, alisema kuwa hatua ya kukaa kimya kwa Rais Kikwete inazidisha laana ndani nchi.Naye Mchungaji Isaack Kalenge, alisema kuwa hawapo tayari kuona taifa hili likiingia katika machafuko hivyo wanatarajia kuandaa kongamano la kuiombea nchi ili amani iliyodumu iendelee kuwepo.

Kalenge alimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa, kutumia hekima na busara katika kuongoza vyama hivyo la sivyo kauli zake zinaweza kuleta mvurugano zaidi miongoni mwa jamii.

1 comment:

  1. If a ruler hearken to lies, all his servants are wicked. -Proverbs 29:12

    ReplyDelete

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...