Wednesday, November 16, 2011

Viongozi wa dini nchini Tanzania waionya serikali na ushoga•  Wasema heri umaskini kuliko fedha chafu

VIONGOZI wa dini nchini wameitaka serikali isithubutu hata kwa sekunde kukubaliana na hatua ya Uingereza ya kutaka nchi za Afrika kuruhusu sheria za ndoa za jinsia moja (ushoga) hata kama taifa litanyimwa misaada kutoka Ulaya.

Wakizungumza na Tanzania Daima jana kwa wakati tofauti, viongozi hao walisema Tanzania iko tayari kukosa kila senti inayotoka Ulaya, kuliko kukubali kuruhusu ushoga, ambao ni kinyume cha maadili ya tamaduni za Kiafrika.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Mussa Salum, alisema kuwa serikali inapaswa kuwa imara katika suala hilo na ikiwezekana itoe kauli ili kupingana na unyanyasaji huo unaoendeshwa na Uingereza.

Rais wa Tanzania Dr Jakaya Mrisho Kikwete
Mwanzoni mwa mwezi huu Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, akihutubia katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola unaofanyika mjini Perth, Australia, alitishia kusimamisha misaada kwa nchi zinazopinga haki za mashoga na kuzitaka zile zinazopokea misaada kutoka nchini humo ikiwamo Tanzania zikubaliane na sharti hilo.
“Ni bora tukose misaada yao kwa kuwa hatukuzaliwa kwa ajili ya kuwategemea Waingereza, maana tunafahamu kuwa Mungu yupo ambaye atatupigania katika hilo,” alisema Sheikh Salum.

Alisema Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wataendelea kulipinga na kulilaani suala hilo hadi mwisho wa kiama, na akawataka Watanzania kuungana kwa pamoja bila kujali tofauti za kiimani kupinga kwa nguvu zote shinikizo hilo.
“Sisi hatukubaliani na kauli ya Cameron, kwa vile yeye si Mungu ambaye anatoa riziki na tunajua katika hilo yapo mataifa mengi yanayomjua Mungu ambao ni wahisani wanaoweza kuendelea kuisaidia Afrika na wanaopingana na jambo hilo la kishetani,” alisisitiza.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron
Naye Katibu wa Baraza la Maaskofu nchini (TEC), Padri Antony Makunde, alisema ni aibu kwa Uingereza kutaka kutumia umaskini wa Waafrika kuleta sera za kishetani na kuongeza kuwa nafasi ya Wakatoliki katika suala hilo ipo wazi, si kwa hapa nchini tu, bali hata kwingineko ambapo hawakubaliani na utamaduni huo.
Alisema mila na tamaduni za Kiafrika haziruhusu jambo hilo, hivyo Uingereza wasitumie umaskini wa Waafrika kulazimisha suala hilo.

“Wakitaka kutupa msaada watupe, lakini si kwa masharti hayo ya kuunyanyasa utu wetu wa Afrika ili tukubaliane na utamaduni wao,” alisema Padri Makunde.
Alisema ni heri Waafrika wakaendelea kuwa maskini na kulinda utu na heshima waliyonayo lakini si kutaka kudhalilishwa kwa ajili ya misaada iliyojaa laana ya ushoga na usagaji.

Hadi jana nchi mbalimbali zimepinga kauli hiyo ikiwamo Ghana, ambayo imewataka wananchi wake kuhakikisha wanasimamia thamani yao na kutokubali kuingiliwa na nchi nyingine yoyote.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...