Wednesday, August 24, 2011

Kufanikiwa Kwa Kusudi La Mungu Kunategemea Namna Unavyotumia Fursa Ulizopewa (Part1)


“ Naam jifunze kutumia vizuri fursa anazokupa Mungu maishani mwako, ili usiathiri/usikwamishe kusudi la Mungu kwako na kwa wengine”
 Isaya 53:3-6

Kwetu Wakristo majira ya Pasaka ni kipindi cha muhimu maana lengo la Mungu kumtuma Yesu ndiyo lilitimia hapa. Kupitia kifo cha Yesu tumeupata wokovu na ushindi dhidi ya nguvu zote za Shetani.

Katika kipindi hiki nimeona ni vema nika-kutafakarisha mstari huu wa Isaya 53:5 unaosema “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu, Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”.


Katika fungu hili la maneno nataka tutazame zaidi sentensi hii inayosema ‘adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake’. Je, umeshawahi kutafakari sentensi hii ina maana gani? Huenda zipo tafsiri nyingi tegemeana na namna unavyotazama na pia unalenga nini katika kujifunza. Baada ya kutafakari sana niligundua mambo mawili yafuatayo;
Jambo la kwanza;
  • Ilimlazimiu Yesu  kuteseka ili sisi tupate amani
Mpenzi msomaji wangu ukweli ni kwamba kwa dhambi zetu ilibidi sisi (wanadamu) kuadhibiwa. Lakini kutokana na upendo wake alikubali kubeba adhabu yetu ili sisi tupate amani.  Yohana 15:3 “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”. Na ni matarajio yake kwamba gharama kubwa ya kifo chake ni kwa ajili yetu tupate amani, na anatarajia tuitumie vizuri amani aliyotuletea tokana na kifo chake.

Wakolosai 1:20 ‘Na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake’…
Wakolosai1:20 ‘Kwa njia yake Mungu alivipatanisha naye vitu vyote naam, viumbe vyote mbinguni na duniani; alileta amani kwa damu ya Kristo msalabani” (Tafsiri nyingine).
 Jambo la pili;
  • Adhabu yake ilitokana na mwanadamu kutumia vibaya amani aliyopewa/iliyokuwepo.
Moja ya kazi au faida kubwa ya kifo cha Yesu pale msalabani ni “kurejesha/kuleta amani duniani na pili ni kuukomboa wakati ambao ulikuwa umetekwa”. Hii ni kwa sababu mwanadamu alitumia vibaya amani   aliyopewa. Sasa naamini unajua palipo na amani ndipo penye maendeleo.

Hivyo tunapoendelea na somo hili naomba itazame amani kama fursa (opportunities) za mtu kufanya vitu/mambo mbalimbali ili afanikiwe. Ili kufanikisha kusudi lake Mungu amemuwekea mwanadamu fursa tofautitofauti ili  azitumie. Ni jikumu la mwanadamu kuzitumia vizuri na akifanya hivyo kusudi la Mungu litatimia kwake na kwa wengine.
  
Hebu tutazame  na kujifunza kutoka katika habari hii ya Luka;

  Luka 19:41-44 inasema“Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua hata wewe ,katika siku hii yapasayo amani, lakini sasa yamefichwa machoni pako, kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke, watakuzingira na kukuhusuru pande zote, watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako”.
 
 Tafsiri nyingine ya Kiswahili inasema “Luka 19:42 inasema: “Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo amani... na pia mstari wa 44 inasema …kwa sababu huku-utambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa…”

Toleo la ASV mstari wa 42  inasema “If thou hadst known in this day, even thou, the things which belong unto peace! but now they are hid from thine eyes”.                                                                                                      Toleo la DARBY kwenye mstari huo linasemaIf thou hadst known, even thou, even at least in this thy day, the things that are for thy peace: but now they are hid from thine eyes”.
 Sasa kutoka kwenye tafsiri hizi nne utagundua;
 Kilichowaingiza kwenye shida hawa ndugu (mji) ni kutokujua yapasayo/yaletayo amani na pia kutotambua majira ya kujiliwa kwao. Hii ina maana hawakujua amani yao imeshikilwa/inaletwa/inatokana/ inategemea nini?. Kutokujua kwao kuliwafanya washindwe kuidumisha amani iliyokuwepo. 

Kwa kifupi Yesu alimaanisha amani yenu imeshikiliwa na vitu fulani ambavyo mnatakiwa kuvilinda, kuvitunza nna kuvizingatia vinginevyo uharibifu mkubwa utawajia. Yesu alitaka wajue amani haiji yenyewe, bali kuna vitu vinavyoileta amani, kuna vitu vimeishikila amani, au hadi amani ije inategemea vitu fulani. Kwa hiyo ni mpaka mvitafute/mvitazame/mvizingatie vinavyoleta au vinavyshikilia amani.

Hebu soma mstari huu Waebrania 12:114 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote…”. Amani yako na watu wengine inategemea vitu fulani, mojawapo ya hivyo vitu au nguzo ni fursa, namna unavyotumia fursa ulizopewa zitaamua amani au mafarakano. 

 Sikia kanisa, hawa ndugu hawakujua kwamba amani yao imeshikiliwa na ‘namna wanavyotumia fursa walizopewa’. Wakitumia vizuri amani yao itadumu na wakitumia vibaya amani yao itaondoka. Na hivyo kufanikiwa kwa kusudi la Mungu katika maisha yao kulitegemea namna wanavyotumia fursa walizopewa na Mungu.

 Hata leo, ni kwa sababu ya wanadamu kutokutumia vizuri fursa ambazo Mungu amewapa katika maisha yao ndio maana wanatahiri kusudi la Mungu kwenye maisha yao na kwa wengine. Fursa ambazo Mungu angetegemea zitumike vizuri, watoto wake wanazitumia vibaya na hivyo kukwamisha kazi yake. Kanisa sikia  hakuna kitu Kinamuuma Mungu kama watu kushindwa kutumia vizuri fursa alizowapa”. 

Jambo hili linamuumiza kiasi cha kumrudisha msalabani mara ya pili. Amani aliyokupa kama fursa kwa wewe kuitumia vibaya inamuingiza kwenye gharama kubwa na kumuumiza sana.

Na: Patrick Sanga

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...