Sunday, August 14, 2011

Sunday Sermon: Jinsi Ya Kujua Mawazo Ya Mungu Ya Kukuondoa Kwenye Shida Uliyo Nayo.


Kile kitabu cha Yoshua 1:8 Biblia inasema” kitabu hiki cha Torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo, maana ndipo utakapoifanikisha njia yako; kisha ndipo utakapostawi sana” 

Kwenye kile kitabu cha Yeremia  29:12, tumeona mawazo ya Mungu kwetu ni mawazo ya amani (kutufanikisha) tena ni yenye kutupa tumaini siku zetu za mwisho. Siku zote mawazo ya Mungu juu yako familia yako, kazi yako, kanisa lako, nchi yako, Biashara yako, ni  mazuri, anawaza kukufanikisha. Tatizo kubwa linalowakabili watu wengi ni kwamba moja hawaelewi nini mawazo ya Mungu juu
yao na hata 


kama wanajua kugundua mikakati ya kutekeleza hiyo mipango ni shida.  Mawazo ya Mungu ya kukufanikisha na njia zake pia yamo ndani ya neno lake. Musa alipokufa Mungu alikuwa amemuandaa Joshua ili kutekeleza Neno lake/kusudi lake la kuwafikisha wana wa

Israel kwani tunaona katika ile Joshua 1:8, Mungu anamsisitiza Joshua kwa habari kuhakikisha kila siku Joshua anasoma ile Torati, anatafakari anachosoma na kukitendea kazi ndipo atakapofanikiwa na kustawi
sana. 

Kwa lugha nyepesi Mungu alimwambia Yoshua kufanikiwa kwako na kustawi kwako katika njia unayoindea kunategemea
sana bidii yako katika kulitafakari na kulitenda neno langu usiku na mchana.
Tumeona kwamba Mungu ndiye mwenye mawazo ya kutufanikisha na kutuondoa kwenye shida tulizo nazo. Sasa kwa namna gani tutaelewa hayo mawazo, ni kwa njia zifuatazo. Moja: kwa kulisoma, kulitafakari na kulitenda neno la Mungu kila iitwapo leo.

Sikiliza, Biblia ni kitabu kilichokamilika ndani yake kimebeba kila namna ya mawazo na njia za Mungu za kukufanikisha, ndani yake kuna mawazo ya kibiashara, kisiasa, kiuchumi (kifedha), kimahesabu, kimahusiano, kiroho, kindoa, kikanisa n.k. kwa lugha nyepesi hakuna shida, tatizo litakalokukabili wewe ambalo jibu lake halipo kwenye Biblia au tunaweza kusema Jibu la kila shida ulionayo lipo kwenye neno la Mungu (Biblia).

Sasa ni jukumu lako wewe kutafakari kila siku na kuhakikisha unajifunza neno lake
na kuyaweka kwenye matendo yale unayojifunza. Mfano: kama wewe ni mwanasiasa na unataka kufanikiwa kisiasa basi ndani ya Biblia kuna ahadi nyingi na mistari mingi inayozungumizia mambo ya siasa, soma tafakari weka kwenye matendo nakuambia utakuwa mwanasiasa wa aina yake, yamkini wewe ni mfanya biashara nakuambia ndani ya Biblia kuna mistari mingi sana inayozungumzia mambo ya biashara, jukumu lako ni kuomba uongozi wa Roho mtakatifu katika kusoma na ktafakari neno lake. Kwa hiyo Mungu anakushirikisha mawazo yake kwa njia ya neno lake. 

Nimalizie kwa mfano huu huenda wewe ni mchungaji mwalimu au kiongozi wa kikundi fulani cha kidini, sikiliza ndani ya Biblia kuna mipango mingi na njia nyingi
sana za namna ya kuchunga au kuongoza hao watu, namna ambavyo kanisa au kundi lako linaweza likaongezeka kiroho, na kiidadi pia.

Namna kanisa lako linaweza kufanyika baraka pale ulipo na uchaotakiwa kufanya ni kusoma hiyo Biblia yako kwa jicho la  kutafakari unachokisoma na kuweka kwenye matendo misitari unayoipata. Jifunze kanisa la kwanza lilifanya nini. Pili: unaweza ukaelewa mawazo ya Mungu kwa kusoma vitabu mbalimbali vya watunzi mbalimbali vinavyozungumza habari za yale yanayokutatiza.

Lakini viwe katika mpango wa Mungu, yaani mawazo yake mle ndani yawe ni mazuri, sio yawe ya kukuongoza utumikie njia ambazo unajua hazimbariki Mungu. Wewe kama ni mfanyabiashara jifunze mfumo wa uchumi wa sasa, usome njia na mazingira ya kiuchumi tendea kazi, soma vitabu vya aina zote maadamu mawazo ya mle ndani yanakuongoza katika njia bora za kutekeleza; kwa hiyo njia ya pili ni vitabu vya aina mbalimbali. 

Tatu: unaweza kupata mawazo ya ki-Mungu ya kukuondoa kwenye shida ulionayo kupitia watu wengine ambao unajua wamefanikiwa katika eneo ambalo wewe linakusumbua; tafuta mtu unayejua amefanikiwa katika eneo  ambalo unataka kufanikiwa si lazima awe ameokoka japo kuna baadhi ya shida ni lazima uwaone watu waliookoka hasa zinazohusiana na mambo ya kiroho. 


Nne: kupitia semina, mikutano na mafundisho mbalimbali yanayofanyika katika eneo ulilopo au nje ya eneo ulilopo. Zipo semina mbalimbali nyingine ni za kiserikali zinalenga wafanyabiashara, wakulima, viongozi, wanafunzi pia zipo za kidini (kiroho) zinazolenga watu wote, wanandoa, cha kufanya nenda huko kajifunze mawazo ya Mungu ya kukufanikisha si unajua serikali inavyokuwa madarakani imewekwa na Mungu na hivyo wao pia watumishi wa Mungu, hivyo nenda huko jifunze kupitia wao. 

Tano: kupitia vyombo mbalimbali vya habari,
kama redio, Tv na computer (internet), magazeti. Vipo vipindi na ratiba mbalimbali vya kidini kwenye Tv vya watumishi wa ndani na nje ya nchi pia, fuatilia, kutoka kwao nunua kanda zenye mafundisho katika eneo unalolihitaji wewe kufanikiwa, sikiliza, tazama, yatendee kazi hayo mawazo. Hivyo ndivyo Mungu pia anavyowashirikisha watu wake mawazo yake. 

Njia ya mwisho ni kujifunza kupitia sauti ya Mungu na kuyatekeleza mawazo na maagizo anayokuletea. Unajua Mungu anazo njia mbalimbali anazoweza kutumia ili kukushirikisha mawazo yake, anaweza  akakuletea wazo fulani la kibiashara, kiuchumi kindoa nk. Chakufanya hakikisha unatekeleza, anaweza akasema nawe kwa njia ya ndoto, maono, kwa sauti yate nk. Zaidi jifunze kutii na kutekeleza kile unachojifunza kwa kusoma, kusikia au kuona. Usipuuze unachojifunza utafanikiwa
sana. Mtegemee Mungu na sio akili zako. 

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na ikae nanyi siku zote. 

Na: Patrick Sanga.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...