Tuesday, June 19, 2012

Jifunze Kumiliki Majibu Ya Maombi Yako


Yoshua 13:7
Utangulizi,Katika dunia ya leo  watu wengi sana wamekuwa wakitumia muda wao mwingi ikiwa ni pamoja na kufanya maombi ya kufunga na kuomba ili kumuomba Mungu awabariki, awaponye, awalinde kwa kifupi awajibu mahitaji yao waliyonayo mbele zake siku zote. Wapo waliokuwa hawazai wamezaa, vipofu wameona, wasioajiliwa wameajiliwa, biashara za wengi zimefanikiwa, ndoa nyingi Mungu ameziponya, wapo waliotaka kuolewa au kuoa na Mungu amewapa waume na wake wazuri.


Sasa hao hao watu ambao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi katika kuomba Mungu awatendee miujiza katika maisha yao, imefika mahali wanaona yale ambayo yalikuwa ni majibu ya Moambi yao shetani ameyavamia na kuleta balaa zaidi na limekuwa pigo kubwa sana  kwa wana wa Mungu. Na kwa sababu hiyo wamejikuta wakimlalamikia Mungu kama vile wana wa Israeli na imefika mahali  pa wengine  kuona kama Mungu  hawezi na hivyo kumuacha.

Tatizo  la haya yote ni kwamba wakristo wengi hawana tabia ya au mazoea ya kumiliki mujibu ya maombi yao toka kwa Mungu. Huenda ulikuwa huna mtoto na Mungu amekupa kuzaa mtoto, sasa  huyo mtoto ndiyo jibu lenyewe kutoka kwa Mungu. Sasa ni lazima ujifunze kumiliki  huo muujiza wa mtoto, sasa si mtoto tu bali ni pamoja na ajira, ndoa, uponyaji, kanisa, Nchi, Biashara nk.

Kusudi la waraka huu mfupi ni kukufundisha njia zitakazokusaidia kumiliki majibu ya maombi yako na kukupa maarifa yatakayokusaidia kuwa makini na majibu ya Mungu katika maisha yako.Tafsiri ya Kumiliki, Neno kumiliki linapozungumziwa kibiblia lina maana ya kukiweka kitu au jambo fulani chini ya utawala wako, maana yake unakuwa na nguvu au umri juu ya hicho kitu. 

Una hakikisha  hakiwezi kutoka kwako. Kumiliki siku zote kunahusisha mapambano makali Sasa mimi sijui Mungu amekutendea nini? Ila ninachojua kwa namna moja au nyingine lazima kuna mambo ulikuwa unamuomba Mungu  akufanyie na mengine tayari ameshakufanyia na mengine ndiyo anayafanya na bado kuna mengi atafanya.sasa katika hayo aliyokwisha kufanya huenda amekupa mke au mme mtarajiwa, huenda ameiponya ndoa yako, nafsi yako, mwili wako, Afya yako, Huenda amekupa mtaji, amekupandisha cheo, amekupa mtoto, amepanua  mipaka ya huduma yako .

Katika lolote ambalo amekufanyia unatakiwa kulimiliki kwa maombi. Kama shetani alikuwa hataki uzae usidhani atamfurahia mtoto uliyemzaa. Kama alishindwa kumzuia asizaliwe usidhani atakubali aendelee kuishi. Shetani atafanya kila  analoweza kuua huyo mtoto au kuharibu chochote kile ambacho Mungu amekutendea kama jibu. Sasa kwa sababu hiyo ni lazima uzijue njia za Kibiblia zitakazokusaidia kumiliki hayo majibu ya maombi yako kutoka kwa Mungu.

Huenda zipo njia nyingi zifuatazo ni sehemu na ni za msingi kati ya hizo nyingi.
Njia ya kwanza, kumiliki kwa kuupigania na kuujenga huo muujiza au jibu lako toka kwa Mungu.

Yoshua 13:1-7, 2 Samwel 2:1-7.Ule mstari wa kwanza wa kitabu cha Yoshua katika kitabu Yoshua 13 unasema “Basi Yoshua alipokuwa mzee na kuendelea sana miaka yake BWANA akamwambia wewe umekuwa mzee na kuendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi  nyingi sana bado kumilikiwa” Kumbuka katika ile sura ya kwanza  ya kitabu cha Yoshua Mungu anamwambia Yoshua uwe Hodari na moyo wa ushujaa maana ni wewe utakayewarithisha watu wa nchi hii. Na ukisoma vizuri kitabu chote cha Yoshua unaona kabisa Yoshua alitekeleza agizo la kuwarithisha wana wa Israel nchi ya ahadi.

Wakati Mungu anamwambia Yoshua bado inabaki nchi yaani maeneo mengi sana ambayo bado hayajamilikiwa tayari Yoshua alikuwa ameshapiga zaidi ya wafalme 32 na kuiteka miji yao, lakini bado Mungu anamwambia bado nchi nyingi inasalia. Kitu gani Mungu anataka tujifunze hapa? Sikiliza Yoshua alipewa kuwarithisha wana wa Israel nchi hii lakini sio kuwamilikisha. Suala la kumiliki lilikuwa kwa yule aliyekabidhiwa nchi  au mji lakini sio kwa Yoshua. Sasa ndiyo maana Mungu akamwambia Yoshua kwa sababu wewe  ni mzee igawanye  hiyo nchi kwa wana wa Israeli kwa kufuata kabila zao ili waweze kumiliki. Maana yake waingie kwenye mapambano ya kile ambacho Mungu amewapa kupitia Yoshua.


Niseme hivi chochote unachokipata kwa njia ya maombi kinamilikiwa kwa njia ya maombi, jifunze kukipigania na kukijenga yaani kuendelea kukiri uwepo wa hicho kitu siku zote. Mfano kama uliomba mke au mme na Mungu amekupa usipunguze kuomba maana shetani usidhani anafurahia ndoa au uhusiano wenu. Ukiendelea  kusoma zile  sura zinazofuata za kitabu cha Yoshua ndipo utakapoona makabila yalivyopambana ili kumiliki jibu lao toka kwa Mungu la nchi.

Njia ya Pili; Miliki majibu yako kwa kutafuta maarifa zaidi ya kutunza huo muujiza.
Hosea 4:6a inasema “Watu wangu wanaangamizwa  kwa kukosa maarifa”.Sikiliza  muujiza au jibu lolote lile ambalo Mungu amekujibu au amekutendea una maarifa yake ya kuutunza. Maarifa hayo yanaweza kuwa ndani ya Biblia na hata katika vitabu vingine nje ya Biblia. Mfano umemwomba Mungu akupe mtaji uanze biashara na Mungu amekupa, sasa huo mtaji una namna zake za kuuendesha ili uweze kuzaa kwa faida. 

Kuna namna fulani ambayo ukiwekeza utapata faida nzuri. Sasa maarifa hayo ya kuwekeza yapo mengine kwenye Biblia lakini mengine ni kupitia watu wenye uzoefu katika hilo eneo, vyombo vya habari, kuna semina za kiserikali kuhusu biashara nenda huko ufuatilie ili  ujue zaidi, maana apendaye mafundisho hupenda maarifa. Huenda ulikuwa hujaoa au kuolewa na sasa uko kwenye ndoa. Hudhuria semina za ndoa na kusoma vitabu husika ili upate maarifa yatakauokusaidia kuishi katika ndoa vizuri.

Umezaa watoto wengi wanakufa kwa malaria halafu watu wanasema ni shetani tu wakati mwingine si shetani  ila ni wewe ulimweka mwanao katika mazingira  ya  kuumwa  na mbu vizuri ndio maana akafa. Soma habari za matumizi ya ngao, chandarua yanayotolewa na serikali hujui kwamba serikali yoyote ile imewekwa na Mungu. Kwa kifupi muujiza wowote amabo Mungu amekutendea una maarifa yake ya kuutunza na chanzo kikubwa cha maarifa ni neno la Mungu. Hivyo lisome likae kwa wingi ndani yako.

Njia ya Tatu; Miliki majibu yako kupitia shukrani, sadaka au utoaji wa aina  yoyote ile.
2Wafalme 5:17”Naamani akasema kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili, kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA.

Hizi  ni  habari za Namani Jemedari  wa jeshi la shamu alikuwa na Ukoma. Alipokwenda Istraeli  kwa nabii Elisha ili aombewe kuhusu tatizo la ugonjwa wake Elisha alimpa maagizo ya kutekeleza kuwa akajichovye / akajizamishe ndani ya mto Yordani mara saba na ndipo atapona. Baada ya Namani kutii maagizo Biblia inasema alipona na ngozi yake ikatakasika ikawa kama ya mtoto mchanga.Baada ya jibu  hilo kwanza Namani alimshukuru Mungu wa Elisha na kisha akasema tangu siku ile hatatoa tena sadaka kwa miungu yao kule shamu isipokuwa kwa Mungu wa Elisha pekee.

Unapomshukuru Mungu kwa lile alilokutendea ni ishara ya kupokea kwa kuonyesha kujua nani aliyekutendea hilo jambo na  hivyo kumrudishia yeye utukufu. Pia unaweza kumiliki majibu ya maombi yako kwa njia ya kutoa sadaka kwa yatima, wajane na pia unaweza kumshukuru Mungu kwa kushuhudia kwa wengine nini Mungu kakutendea au kutoa sadaka ya shukrani au utoaji kwa makundi mengine yasiyojiweza  katika jamii.

Na Mwl Patric Sanga

1 comment:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...