Wednesday, June 27, 2012

Jifunze Kumiliki Majibu Ya Maombi Yako 2 -Mwl Sanga



Njia ya nne: Kumiliki muujiza kwa kuwatunza watumishi wa Mungu na kuchangia huduma mbalimbali.

Yoshua 12:1-3 kwenye ule mstari wa pili Biblia inasema “Basi wakamwandalia karamu huko naye Martha akamtumikia na Lazaro alikuwa mmoja wapo wa wale walioketi chakulani pamoja nao.

Hii pia ni habari nyingine inamhusu Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua baada ya kuwa amekufa kwa siku nne. Sasa Lazaro aliumiliki muujiza wake wa kufufuliwa kwa kumtunza Yesu pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Hii ina maana Lazaro pamoja  na dada zake waliingia gharama kwa ajili ya kuwatunza Yesu pamoja na  wanafunzi wake, Kwa siku zote ambazo Yesu alikaa kwa Lazaro, Lazaro alihakikisha hawalali njaa, anawapa mahali pa kulala nk.


Sasa unaweza kumiliki muujiza wako kwa kuruhusu watumishi wa Mungu wakae nyumbani kwako. Huenda wamekuja kwenye mkutano au semina kwa wiki moja au mbili itoe nyumba yako itumike, kufanya hivyo ni kumfanya Mungu aendelee kukulinda wewe na yale aliyokupa maana anajua hutamnyima siku moja atakapohitaji kuvitumia. Wapo wengine wanaomiliki kwa kutoa magari yatumike kipindi chote cha mikutano, unaweza pia  kumiliki kwa kuchangia gharama za mikutano  si lazima pesa lakini hata kufanya kazi mbalimbali katika mkutano huo, huenda  ni  usafi,  kubeba vyombo, kufanya usafi walikofika watumishi, kuombea huo mkutano au semina nk. Nakuambia unaweza ukaona kama ni vitu vidogo lakini ndivyo mujibu ya maombi yanavyomilikiwa bila kujali Mungu amekutendea nini.

Nija ya tano: Kumiliki muujiza kwa kufanya  maamuzi ya kuokoka endapo Mungu alikufanyia huo muujiza kabla hujaokoka, na kuwaambia wengine habari ya Yesu aliyekuponya.

Ukisoma ile sura nzima ya 9 ya kitabu cha Yohana utakutana na habari ya kipofu mmoja tangu kuzaliwa kwake  ambaye Yesu alikuwa amemponya. Ule mstari wa 39 unasema “akasema,Naamini, Bwana akamsujudia” Ukisoma vizuri habari hii utagundua baada ya mahojiano marefu kati ya mafarisayo na yule kijana kuhusu uponyaji wake ndipo Yesu akamwuuliza je unamwamini mwana wa Mungu? Yule kijana akamwuliza ni nani huyo nipate kumwamini? Kwa kifupi Yesu akamjibu unayezungumza naye. Ndipo yule kijana  akasema, naamini Bwana akamsujudia.

Mtu mwingine ni Naamani ambaye tumekwisha ona habari zake, kitendo cha yeye kusema toka leo sitatoa sadaka kwa miungu  ya shamu ila kwa Bwana  ni dalili  ya kuonyesha kumwamini Mungu wa Israel. Hivyo hata leo wapo ambao Mungu anawatendea mambo mengi hata kabla hawajaokoka sasa ili kumiliki  hayo ambayo Mungu amekufanyia mwamini Yesu ndio huo muujiza utadumu. Wapo watu leo wanafunguliwa kwenye nguvu za mapepo huo ni  uponyaji. Sasa badala ya kuwasaidia watu wamwamini Yesu tunawaacha, nakuambia pepo watarudi kwa huyo mtu wenye nguvu zaidi kuliko yule wa kwanza.


Pia ukisoma vizuri habari hiyo hiyo utagundua kwamba huyu jamaa alimiliki uponyaji wake kwa kuwaambia wengine habari za Yesu na kukiri kwamba  mponyaji ni Yesu na si mtu mwingine, nakuambia  kufanya  hivyo ni kujihakikishia kudumu kwa huo muujiza na Mungu ataendelea kuutunza huo muujiza  maana wewe ni chombo chake. Mungu akikuponya au kukubariki usinyamaze kimya waambie wengine habari za Yesu aliyekuponya. Jifunze kutoka kwa mwanamke msamaria. Uponyaji wa nafsi yake ulipelekea watu wengi wa mji wa Samaria kuokoka. Soma kile kitabu cha Yohana sura ya nne mistari 30 ya kwanza utaiona habari hii.

Mpenzi msomaji wangu mpaka hapa naamini utakuwa umepata kitu cha kukusaidia labda nikuambie hivi  siri kubwa ya mafanikio ni kuliweka neno la Mungu kwenye matendo, si unajua imani pasipo matendo imekwisha kufa katika nafsi ya huyo mtu mwenye imani hiyo. Nimeamua  kuandika ujumbe  huu baada ya kuona wana wa Mungu wengi imefika mahali  wanakuta yale ambayo Mungu aliwapa kama majibu ya maombi yao yameshaharibiwa na shetani, wapo waliozaa watoto wao wakafa na walimuomba sana Mungu kuhusu hao watoto nk. Sasa  ni imani  yangu kwamba tangu sasa jambo lolote ambalo Mungu atakupa kama jibu la maombi yako utalimiliki.
Ndimi katika huduma

Mwl Patric Sanga

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...