Tuesday, June 5, 2012

Ujumbe kutoka kwa Mwl Mwakasege - Ikimbieni Zinaa 3


 Mwl Mwakasege

Ushindi dhidi ya dhambi
Uhusiano wako na dhambi unakuwaje baada ya kuokoka, na kufanyika kiumbe kipya ndani ya Kristo? Watu wengi wakiisha-okoka, huwa bado wanasumbuliwa na kuanguka katika dhambi mara kwa mara, na hasa katika zinaa. Na hii inatokea kwa kuwa hawapati mafundisho ya kutosha ya neno la Mungu juu ya jinsi wanavyotakiwa kuenenda katika maisha mapya waliyopita.

Kaini aliambiwaje na Mungu? Bwana alimwambia hivi; “ kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa UISHINDE” (Mwanzo 4:7)
Na ndivyo ilivyo hata sasa. Bado tumo ulimwenguni humu, ingawa aliyezaliwa mara ya pili yeye si wa ulimwengu huu (Yohana 17:16). Lakini kwa kuwa bado  tumo katika ulimwengu uliojaa dhambi inayotutamani kila siku, na tusije tukajisahau. Inatupasa tuishinde.

Yanenaje maandiko?
Imeandikwa katika kitabu cha (Warumi 6:12-14)
“Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake; wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi, bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi, bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki. Kwa maana DHAMBI HAITA WATAWALA NINYI, kwa sababu hamuwi chini ya sheria, bali chini ya neema”.

Ikiwa tunaambiwa ya kuwa “Dhambi haitawala ninyi …….” inakuwaje basi wengine wanatawaliwa nayo? Inakuwaje mtu wa Mungu, aliyepakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu aanguke katika zinaa? Kitu gani kinampofusha macho ya rohoni?
Je! Ni halali kwa mtu anayekaa ndani ya Kristo kutenda dhambi?

Yanenaje maandiko?
“Kila akaaye ndani yake (Yesu Kristo) HATENDI DHAMBI; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtamua….atendaye dhambi ni wa ibilisi; kwa kuwa ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” (1 Yohana 3:6,8)

Je! Unaona maneno haya yalivyoandikwa kwa ajili yetu? Sidhani kama unapenda tena kuwa Ibilisi kwa kuwa “Apendaye dhambi ni wa Ibilisi” Kwa hiyo ni muhimu ujilinde usitende dhambi.

 “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu UZAO WAKE WAKAA NDANI YAKE; WALA HAWEZI KUTENDA DHAMBI KWA SABABU AMEZALIWA KUTOKANA NA MUNGU.” (1 Yohana 3:9)
Ikiwa umezaliwa mara ya pili kwa Roho wa Mungu, ujue hakika UZAO WA MUNGU unakaa ndani yako. Na uzao huu wa uungu ni Mtakatifu, na unakaa ndani yake bila kutangatanga unakuwezesha kuishi bila kutenda dhambi.
Je! Si jambo la kumshukuru Mungu hilo. Si kwamba anatuambia tusitende dhambi bila kutupa njia ya kutusaidia. Anajua sisi wenyewe hatuwezi kuishinda dhambi, BALI YEYE AKIKAA NDANI YETU NA SISI NDANI YAKE TUNAWEZA KUISHI KATIKA USHINDI DHIDI YA DHAMBI NA MITEGO YAKE YOTE.

Tena imeandikwa;
“Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu HATENDI DHAMBI; bali yeye aliyezaliwa na Mungu HUJILINDA, wala yule mwovu HAMGUSI.” (1 Yohana 5:18)
Ee, mtu wa Mungu, jilinde basi kwa kuwa umezaliwa na Mungu, kwa nini tamaa ya uasherati ikusonge? Je?! umesahau ni uzao wa namna gani ulio ndani yako?
Ni kweli kwamba mtu akitenda dhambi na akatubu, Bwana atamsamehe, (1 Yohana 1:9). Lakini hatutakiwi kutenda dhambi. Ndiyo maana imeandika; “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba MSITENDE DHAMBI”…. (1 Yohana 2:1)

Sasa naona unaweza kuelewa kwa nini inashtusha na kusikitisha unaposikia mtu wa Mungu ameanguka katika dhambi ya zinaa. Ikiwa maisha ya wokovu yatakuwa ni ya kuanguka na kusimama, halafu tena kuanguka na kusimama mara kwa mara; basi ina maana ya kuwa ushindi wa kutosha haukupatikana pale msalabani.

Lakini nataka nikuambie hivi, ushindi kamili ulipatikana pale msalabani bila kubakiza kitu! Ndiyo sababu Yesu Kristo alikuwa na ujasiri wa kusema ‘IMEKWISHA’ pale msalabani.
Tunachotakiwa kufanya ni kuwa watendaji wa neno; na ndiyo ushindi huo utadhihirika katika maisha yetu. Usidhani ya kuwa mapokeo ya wanadamu yanaweza kukusaidia kuishinda dhambi; la hasha! Yesu Kristo peke yake akikaa ndani ya   moyo wako, na neno lake ukilitii, ndiko utapata ushindi halisi na halali dhidi ya dhambi.

Swali la kujiuliza
Idadi ya wakristo waliookoka wanaoanguka katika dhambi ya zinaa inaongezeka siku baada ya siku. Na wengine wameanguka dhambini moja kwa moja, hata haja ya kutaka kusimama upya katika Bwana imepotea. Wanaona aibu! Na wengine wanaanguka na kusimama, halafu tena wanaanguka na kusimama. Na kwa sababu hiyo hawana ushuhuda mzuri mbele za watu. Hawaaminiki tena.

Lakini je! Unadhani Mungu atatuambia tuishinde dhambi wakati anafahamu ya kuwa hatuna uwezo huo? La hasha! Mungu wetu tunayemwamini katika Kristo Yesu si dhalimu kiasi hicho.
Jambo ninalofahamu ni kwamba ametuambia tuishinde dhambi kwa kuwa ndani yetu sisi tuliompokea, ametupa UWEZA WA KUISHINDA DHAMBI – kwa namna gani?
“Kwa sababu UZAO WAKE WAKAA NDANI YAKE (YETU) WALA HAWEZI (HATUWEZI) KUTENDA DHAMBI KWA SABABU AMEZALIWA (TUMEZALIWA) KUTOKANA NA MUNGU”.(1Yohana 3:9)
Uzao wako si uzao wa kuanguka dhambini, bali ni uzao wa kushinda dhambi, kwa kuwa Kristo anakaa ndani yako!

Mwisho

Na Mwl C.Mwakasege

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...